Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ulaya yaongeza msaada kupambana na utapiamlo Niger-WFP

Ulaya yaongeza msaada kupambana na utapiamlo Niger-WFP

Pakua

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP leo limekaribisha mchango wa dola milioni 4.5 kutoka kwa tume ya Ulaya ambao utasaidia kuongeza ubora na upatikanaji wa chakula nchini Niger ambako takribani watoto milioni mbili wana utapia mlo.

Fedha hizo kutoka tume ya Ulaya na ushirikiano wa kimataifa wa maendeleo (DEVCO) itairuhusu WFP na shirika la asasi za kiraia la Ufaransa GRET kusaidia uzalishaji wa vyakula vyenye lishe kutoka kwa mashirika ya ndani ya wakulima . Pia utasaidia kubaini njia zitakazowasaidia makundi ya wakulima kuaminiwa na walaji suala ambalo litaongeza pato lao.

Tangu mwaka 2011 WFP nchini Niger imekuwa ikiendeleza mashirika ya wakulima kwa kununua baadhi ya vyakula inavyogawa kama msaada, kuboresha kiwango kinachozalishwa na wingi wa mazao.

Na kwa upande wake GRET imekuwa ikitoa msaada wa kiufundi katika kusaidia kutengeneza unga unaotumiwa kama lishe kwa watoto wachanga. WFP inasema kuboresha lishe Niger ni muhumi sana kwani wanawake na watoto wengi wana matatizo ya upungufu wa damu au anemia, na karibu nusu ya watoto wote nchini humo wamedumaa.

Photo Credit
Picha:OCHA/Franck Kuwonu