Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko Rais Touadéra kwa kuanzisha mahakama maalum CAR- Ladsous

Heko Rais Touadéra kwa kuanzisha mahakama maalum CAR- Ladsous

Pakua

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao kuhusu hali ya amani, usalama na kibinadamu huko Jamhuri ya Afrika ya Kati ambapo imeelezwa kuwa mwaka mmoja tangu kufanyika kwa uchaguzi,kumekuwepo na mafanikio hasa kurejeshwa kwa utawala wa serikali kwenye mji muhimu wa Bambari.

Akihutubia kikao hicho, mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa Herve Ladsous amesema kurejea kwa utulivu kwenye mji huo ni kiashiria cha jinsi uwepo wa vikosi vya ulinzi wa amani vya umoja huo, MINUSCA umedhibiti kusonga mbele kwa vikundi vilivyojihami kama kile cha FPRC kilichokuwa kinatishia usalama wa raia.

Amesema anatiwa moyo na azma ya Rais Faustin-Archange Touadéra ya kuwa na mazungumzo ya kina na vikosi vilivyojihami na wakati huo huo kuhakikisha sauti za raia walioathiriwa na mapigano zinasikika.

(Sauti ya Ladsous)

“Kwa mantiki hiyo nakaribisha azma ya Rais Touadéra ya kusaidia kuanzishwa kwa mahakama maalum ya uhalifu na kushughulikia ukwepaji sheria dhidi ya makosa makubwa zaidi.Natiwa moyo zaidi na uteuzi wa mwendesha mashtaka maalum wa mahakama hiyo na napenda kusisitiza umuhimu wa kuchagiza mchakato wa ajira ya mahakimu na polisi wa mahakama na pia kupitisha mkakati wa kulinda wahanga na mashahidi.”

Katika hotuba yake hiyo, Bwana Ladsous amezungumzia pia janga la kibinadamu huko CAR akisema harakati zozote za kukwamua nchi hiyo ziende sambamba na usaidizi wa kibinadamu wakati huu ambapo zaidi ya watu milioni 2.2 nchini  humo wanahitaji misaada.

Photo Credit
Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa Herve Ladsous.(Picha:UM/Manuel Elias)