Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mawaziri wa afya wa Kikanda wakutana kusaidia kukomesha mlipuko wa polio Gaza: WHO/UNICEF

Huko Gaza, watu wengi ambao wamekimbia makazi yao wanaishi kwenye mahema.
© UNRWA
Huko Gaza, watu wengi ambao wamekimbia makazi yao wanaishi kwenye mahema.

Mawaziri wa afya wa Kikanda wakutana kusaidia kukomesha mlipuko wa polio Gaza: WHO/UNICEF

Afya

Mawaziri wa afya kutoka eneo la Mashariki ya Mediterania wameungana kushughulikia dharura ya polio katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwenye Ukanda wa Gaza.

Haja ya dharura ya uratibu, na hatua ya pamoja ya kikanda ili kupambana na lahaja ya aina ya 2 ya polio (cVDPV2) katika Ukanda wa Gaza ndio lilikuwa lengo la mkutano wa 11 wa Kamati Ndogo ya Kikanda ya Kutokomeza Polio na Milipuko wa ugonjwa huo kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani WHO na lile la kuhudumia watoto UNICEF.

Mkurugenzi wa WHO wa Kanda ya Mediterania Mashariki Dkt. Hanan Balky aliitisha mkutano huo, uliofanyika jana tarehe 25 Julai 2024 kwa njia ya mtandao.

Uthibitisho wa virusi vya polio unaongeza vitisho vingi vinavyowakabili leo watoto katika Ukanda wa Gaza, ambao walikuwa na upatikanaji wa huduma za chanjo za kawaida kabla ya vita na kuibua wasiwasi juu ya uwezekano wa kuenea kwa virusi vya polio na ugonjwa wa kupooza wakati inakadiriwa  kuwa asilimia  99 ya watoto katika eneo linalokaliwa la Palestina walipokea dozi yao ya tatu ya chanjo ya polio mwaka 2022, idadi hiyo ilishuka hadi asilimia  89 mwaka 2023 kulingana na makadirio ya hivi karibuni ya chanjo ya WHO na UNICEF.

Hatua za pamoja zinahitajika haraka

Akitafakari kuhusu ziara yake ya hivi karibuni katika Ukanda wa Gaza, Dkt. Balky ametetea hatua za pamoja za kukomesha kusambaa zaidi kwa polio. "Nilishuhudia kwanza hali ya maisha ambayo ni  mazingira mazuri kwa kuenea kwa polio na magonjwa mengine. Huu ni wakati muhimu kwa Kamati Ndogo kuja pamoja ili kuchukua hatua haraka na madhubuti kudhibiti mlipuko huu, kwa watoto wa Gaza.”

Waliohudhuria mkutano huo ni mawaziri wa afya kutoka nchi wanachama wa Kanda ya Mashariki ya Mediterania, washirika wa mradi  wa kimataifa wa kutokomeza polio na wakurugenzi wa UNICEF wa kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini na Asia Kusini.

Washiriki wa mkutano walipews taarif kuhusu hali ya polio katika Ukanda wa Gaza.

Kisha washiriki hao kwa kauli moja walitoa wito kwa wadau na viongozi kote katika eneo la Mashariki ya Mediterania, zikiwemo pande zinazohusika katika mzozo wa ardhi ya Palestina inayokaliwa kutetea kwa nguvu zote na mara moja kuhakikisha kunakuwepo mazingira salama na wezeshi, kwa njia ya usitishaji vita au siku za utulivu ili kuruhusu hatua zichukuliwe kukomesha polio kusababisha kupooza kwa watoto huko Gaza, na maeneo jirani na nchi.”

Hatua za kuchukuliwa

Hatua hizo kwa mujibu wa WHO na UNICEF ni pamoja na ufuatiliaji ulioimarishwa, kampeni nyingi za chanjo ya polio ambazo zinaweza kuunganishwa na utoaji wa huduma nyingine muhimu za afya inapowezekana, na ushirikishwaji bora wa jamii ili kuhakikisha kwamba kila mtoto analindwa.

Dkt. Maged Abu Ramadan, Waziri wa Afya kutoka eneo linalokaliwa la Palestina alikiri kuhusu hatari kwa afya ya watu, haswa watoto, huko Gaza na kuomba uungwaji mkono wa nchi Wanachama katika kujenga uwezo wao wa ufuatiliaji ili kuhakikisha uwepo wowote wa virusi vya polio unagunduliwa mara moja, pamoja na usaidizi wa maabara kwa ajili ya kupima sampuli za mazingira na binadamu katika nchi jirani za eneo la WHO la Mediterania ya Mashariki.

Mawaziri hao wa afya wamesisitiza udharura wa juhudi zilizoratibiwa za kikanda kusaidia htua katika Ukanda wa Gaza na nchi zinazozunguka, ambao utatafsiri kuwa na mpango wa pamoja, thabiti wa kuzuia na kukabiliana na mlipuko wa virusi vya polio.

Matoleo ya msaada wa kiufundi, vifaa na maabara kwa ajili ya vipimo vinayoendelea vya sampuli za binadamu na mazingira kutoka Ukanda wa Gaza yalitolewa na Iraq, Jordan, Ufalme wa Saudi Arabia na Syria.

Kamati Ndogo pia imeshughulikia hitaji la dharura la kukomesha aina zote za virusi vya polio katika Kanda nzima ya Mashariki ya Mediterania ambako ni nyumbani kwa nchi mbili za mwisho duniani zenye maambukizi ya virusi vya polio mwitu Afghanistan na Pakistan.

Nchi za eneo hilo pia zinakabiliwa na milipuko ya virusi vya polio, kama vile Somalia, Sudan na Yemen.

Polio katika nchi moja ni hatari ukanda mzima

Dkt. Salih Ali Al-Marri, Waziri Msaidizi wa Masuala ya Afya aliyezungumza kwa niaba ya Dkt. Hanan Al Kuwari, Waziri wa Afya wa Qatar na Mwenyekiti Mwenza wa Kamati Ndogo, amesisitiza kuwa maadamu polio inaendelea kuenea katika sehemu yoyote ya kanda yetu kila nchi iko hatarini.

"Hatari hizi zinatokana na changamoto zilizo nje ya udhibiti wetu kama vile mienendo mikubwa isiyo ya kawaida ya watu kutoka maeneo yaliyoambukizwa, kama inavyoonekana hivi karibuni nchini Pakistan na Afghanistan, migogoro na ukosefu wa ufikiaji wa kibinadamu na changamoto tunazoweza kushughulikia, kama vile mapungufu katika uongozi wa programu na uratibu. Mikakati yetu sasa, zaidi ya hapo awali, lazima iwe bunifu zaidi kuliko ile ya virusi, "amesema

Nchi Wanachama zinatambua juhudi zinazoendelea za uongozi wa kisiasa na afya kushughulikia mapengo yaliyosalia nchini Afghanistan na Pakistan.

Pia zimebainisha juhudi zinazoendelea kukomesha milipuko hiyo nchini Somalia, Sudan na Yemen.