Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hofu yazidi kutanda uwezekano wa mlipuko wa Polio Gaza - WHO

Zaidi ya tani 330,000 za uchafu zimerundikana katika maeneo mbalimbali Gaza na kusababisha hatari za kimazingira na kiafya. (Maktaba)
© UNRWA
Zaidi ya tani 330,000 za uchafu zimerundikana katika maeneo mbalimbali Gaza na kusababisha hatari za kimazingira na kiafya. (Maktaba)

Hofu yazidi kutanda uwezekano wa mlipuko wa Polio Gaza - WHO

Amani na Usalama

Hofu inaendelea kuongezeka juu ya athari mbaya za uwezekano wa mlipuko wa ugonjwa wa polio huko Ukanda wa Gaza kutokana na mazingira duni ya huduma za kujisafi na watu kushindwa kufikia huduma za afya, limeonya hii leo shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO.

Dkt. Ayadil Saparbekov, kiongozi wa timu ya dharura ya kiafya ya shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO kwenye eneo linalokaliwa la wapalestina, oPt amewaeleza waandishi wa habari hii leo huko Geneva, Uswisi kuwa ana wasiwasi mkubwa juu ya uwezekano wa kusambaa polio na magonjwa mengine ya kuambukiza, hali ambayo inaweza kusababisha watu wengi kufa kwa magonjwa ya kuambukiza kuliko majeraha yatokanayo na vita.

Ugonjwa wa homa ya ini aina ya A au Hepatitis A, tayari ulithibitishwa kwenye Ukanda wa Gaza mwaka jana, amesema Dkt, Saparbekovu akizungumza kwa njia ya video kutokea mji wa Yerusalemu.

“Mfumo wa afya wa Gaza ukiwa umedhoofika, ukosefu wa maji na huduma za kujisafi pamoja na wananchi kushindwa kufikia huduma za afya, hii itakuwa hali mbaya sana,” amesisitiza.

Virusi vya Polio kwenye majitaka

Tarehe 16 mwezi huu wa Julai, WHO ilisema kuwa aina ya polio itokanayo na kudhoofika kwa virusi vilivyoko kwenye chanjo ya polio aina ya pili au (VDPV2) ilibainika kwenye maeneo sita kutoka katika sampuli za majitaka zilizokusanywa tarehe 23 Juni huko Khan Younis na Deir Al-Balah.

WHO ilieleza kuwa aina hiyo ya virusi vya polio inaweza kupatikana kwenye maeneo ambako utoaji chanjo umedhoofu na kuruhusu chanjo hiyo ipatiwayo watu kwa njia ya mdomo kubadilika na kuwa na nguvu zaidi.  

Ingawa hivyo hadi sasa hakuna mtu yeyote Gaza aliyethibitishwa kupooza kutokana na polio.

Utafiti zaidi uliofanywa na Kituo cha Marekani cha kudhibiti magonjwa, CDC, huko Atlanta, Georgia, umedokeza kuwa virusi hivyo vya polio na vile vilivyosambaa Misiri wakati wa nusu ya pili yam waka 2023.

Bado sampuli kutoka kwa binadamu hazijachukuliwa

Kwa mujibu wa Dkt. Saparbekov sampuli bado hazijachukuliwa kutoka kwa binadamu kupima polio kutokana na ukosefu wa vifaa na uwezo wa maabara kuchunguza sampuli.

Timu ya WHO itakwenda Gaza Alhamisi hii ikiwa na vikasha 50 vya kuchukulia sampuli na kisha itatuma sampuli hizo kwenda maabara iliyoko Jordan kwa ajili ya uchunguzi.

Kwa sasa WHO na wadau wake wanafanya uchunguzi wa kitabibu na tathmini ya hatari inayoweza kutokea na kisha pia kubaini chanzo cha virusi hivyo ambavyo viko hatarini kusambaa Gaza na duniani.

Mapendekezo ya kudhibiti yatatolewa lakini changamoto ni usafi

“Kutokana na matokeo ya tathmini hiyo, WHO na Mtandao wa kimataifa wa kukabili Polio, tutaandaa mapendekezo ikiwemo umuhimu wa chanjo kupitia kampeni ya utoaji wa chanjo kwa watu wote,” amesema Afisa huyo wa WHO.

Hali ya huduma za kujisafi Gaza ni duni kwani kwa sasa idadi kubwa ya watu wanaoishi kwenye kambi, choo kimoja kinahudumia watu 600 na penginepo mtu mmoja anapata lita 1.5 ya maji kwa siku ambayo hayatatosheleza mtu kuzingatia mapendekezo ya kiafya.