Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Machafuko yanayoendelea Kivu Kaskazini yanatia hofu kubwa: OCHA/MONUSCO

Nyiranzaba na watoto wake tisa wanapata hifadhi kwenye hema baada ya kukimbia kijiji chake katika eneo la Rutshuru, jimbo la Kivu Kaskazini, DR Congo.
© UNICEF/Arlette Bashizi
Nyiranzaba na watoto wake tisa wanapata hifadhi kwenye hema baada ya kukimbia kijiji chake katika eneo la Rutshuru, jimbo la Kivu Kaskazini, DR Congo.

Machafuko yanayoendelea Kivu Kaskazini yanatia hofu kubwa: OCHA/MONUSCO

Amani na Usalama

Licha ya makubaliano ya usitisja uhasama uliotangazwa wiki mbili zilizopita kwa minajili ya kibinadamu Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, machafuko bado yanaendelea na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya  kibinadamu na masuala ya dharura OCHA inasema  hilo linatia hofu  kubwa.

OCHA inasema kuwa mashambulizi ya silaha yanayoendelea dhidi ya raia huko Lubero, Kivu Kaskazini, yamezuia ufikiaji wa kibinadamu katika maeneo kadhaa ambapo watu waliokimbia makazi yao wamesaka hifadhi.

Kati ya Machi na mwanzoni mwa Julai mmwaka huu wakati usitishaji wa uhasama kwa ajili ya masuala ya kibinadamu ulipotangazwa, ghasia katika jimbo la Kivu Kaskazini zimewafanya watu 390,000 kuyahama makazi yao katika maeneo ya Rutshuru na Lubero.

Ingawa makubaliano hayo yameruhusu mashirika ya misaada kuanza tena usambazaji wa vifaa vya matibabu na usaidizi mwingine wa kuokoa maisha kwa watu waliokimbia makazi yao na waliorejea Lubero, wengi bado wanahitaji msaada muhimu.

Usitishaji uhasama wakaribishwa

Ili kuwafikia waathirika OCHA inasema, wahudumu wa misaada kama ilivyo kwa raia nchini DRC lazima walindwe.

Kuongezwa muda wa usitishaji uhasama kwa ajili ya misaada ya kibinadamu hadi tarehe 3 Agosti ni hatua ya kukaribisha, lakini ni muhimu kwamba pande zinazohusika katika mzozo zifanye kazi kwa uhakika kukomesha mapigano na kutafuta suluhu endelevu kwa njia ya mazungumzo limesema shirika hilo.

Na kutoka mkoa wa Ituri, wenzetu wa kulinda amani wanatuambia kwamba walijibu milio ya risasi iliyofyatuliwa na wanachama wa kundi la waasi la CODECO katika matukio mawili tofauti yaliyotokea katika vijiji vya kusini mashariki mwa Djugu huko Ituri. Washambuliaji hao waliondoka pale walinda amani walipowasili eneo la tukio.

CODECO wachachafya Ituri

Na katika jimbo la Ituri, mpango wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC ujulikanao kama MONUSCO umesema umlikwenda kusaidia kukabili mashambulizi ya milio ya risasi iliyofyatuliwa na wanachama wa kundi la waasi la CODECO katika matukio mawili tofauti yaliyotokea katika vijiji vya kusini mashariki mwa Djugu huko Ituri. Washambuliaji hao waliondoka pindi walinda amani wa MONUSCO walipowasili eneo la tukio.

Wakati huo huo, MONUSCO umesaidia ujenzi wa kituo cha mafunzo ya ufundi stadi huko Komanda, pia katika jimbo la Ituri.

Kituo hicho kimeanzishwa ili kuwasaidia waliokuwa washiriki wa vikundi vyenye silaha na vijana walio katika hatua za kujiunga tena katika jamii zao na kuwapa vifaa vya mafunzo ya useremala, ushonaji na ufundi makenika.

Mpango huu ni wa kuunga mkono mpango wa serikali wa kuondoa, kupokonya silaha, na kufufua jamii zenye na utulivu kwa wapiganaji wa zamani kutoka makundi mbalimbali yenye silaha.

Kupitia kazi yake, Ujumbe wa Umoja wa Mataifa unachangia kupunguza ukosefu wa ajira kwa vijana, huku ukihimiza amani na maendeleo katika eneo hilo.