Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UDADAVUZI: Nyenzo tano zinazohitajika kudumisha amani

Askari wa mpango wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani MONUSCO nchini Congo DRC akilinda wakati helkopta ya WFP ikiwasilisha msaada kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani Ituri
© UNICEF/Diana Zeyneb Alhindawi
Askari wa mpango wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani MONUSCO nchini Congo DRC akilinda wakati helkopta ya WFP ikiwasilisha msaada kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani Ituri

UDADAVUZI: Nyenzo tano zinazohitajika kudumisha amani

Amani na Usalama

Mwaka 1948, Umoja wa Mataifa ulichukua hatua muhimu kwa kupeleka askari wa kulinda amani kusaidia nchi katika safari yao ya kuelekea amani. Tangu wakati huo, zaidi ya watu milioni mbili wanajeshi, polisi na raia wamehudumu katika operesheni zaidi ya 70 za kulinda amani duniani kote, wakitoa msaada huku kukiwa na migogoro inayoendelea au matokeo ya migogoro hiyo.

Juhudi zao zisizochoka zinaanzia kufuatilia mikataba ya kusitisha mapigano hadi kuwalinda raia, kujenga upya miundombinu muhimu na kuwezesha uchaguzi ili kusaidia nchi na jamii kutoka katika vita hadi kuingia kwenye amani. Walinzi wa amani wanaweza kuwa askari, maafisa wa polisi, wahandisi, madaktari, madaktari wa mifugo, maafisa wa haki za binadamu, maafisa wa haki na magereza, watayarishaji wa vipindi vya redio, wanasayansi wa mazingira na wataalam wa ufuatiliaji.

Tunapofikiria juu ya kulinda amani, mara nyingi tunafikiria upatanishi, mikataba na sheria za kimataifa. Hata hivyo, walinda amani hutumia safu pana zaidi ya zana kulinda na kudumisha amani katika baadhi ya maeneo tete duniani. Tunapoadhimisha Siku ya Kimataifa ya Walinda Amani wa Umoja wa Mataifa tarehe 29 Mei, tunaangazia zana tano zisizo za kitamaduni zinazotumiwa na walinda amani kulinda jamii wanazozihudumia.

1. Helikopta

Kila mahali barani Afrika, Amerika, Mashariki ya Kati, Ulaya na Asia, walinda amani wametumia helikopta kushinda vizuizi vya kijiografia na kupanua wigo wa msaada wao kwa jamii katika mandhari mbalimbali.

Helikopta ni zana muhimu ya anga katika operesheni za kulinda amani kwa sababu mbalimbali. Zinasaidia walinda amani kufikia vijiji vya mbali visivyoweza kufikiwa na barabara au njia ya maji, zinaruhusu hatua za haraka na uokoaji wakati wa dharura, kuwasilisha vifaa muhimu na misaada kwa jamii zinazohitaji na kufanya uchunguzi wa angani na upelelezi ili kufuatilia na kukusanya taarifa za kijasusi. Katika baadhi ya matukio, helikopta zenye silaha zinaweza kutumika  kama ngao dhidi ya makundi yenye silaha.

Mlinda amani wa kike toka Senegal akifanyakazi katika helkopta akiwa katika mpango wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati MINUSCA
MINUSCA/Hervé Serefio
Mlinda amani wa kike toka Senegal akifanyakazi katika helkopta akiwa katika mpango wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati MINUSCA

Helikopta pia zimekuwa na jukumu muhimu katika kuwasilisha nyenzo za uchaguzi ili kuhakikisha kuwa watu katika maeneo ya mbali mashinani wanaweza kushiriki katika michakato ya kidemokrasia ya nchi zao. Wakati mwingine, katika maeneo ya vijijini zaidi, walinda amani hutegemea helikopta, zikifuatiwa na kutembea kwa miguu au mikokoteni, ili kuhakikisha vifaa hivyo vinawafikia watu kwa wakati.

Uwezo wake mwingi unabaki kuwa muhimu katika kutoa msaada na ulinzi ambao watu wanahitaji. Hivi sasa kuna helikopta 81 zinazofanya kazi katika operesheni za kulinda amani. Chapa ya Umoja wa Mataifa inaonekana kwenye sehemu ya nje ya helikopta, ikiwa ni pamoja na chini ya tumbo lake, kuashiria kuwa ni msafara wa walinda amani au wa wahudumu wa kibinadamu.

Licha ya hayo, helikopta za Umoja wa Mataifa zimekuwa zikishambuliwa, jambo linaloonyesha jinsi hali ya usalama inavyoweza kuwa tete katika operesheni nyingi na jinsi walinda amani wanavyohatarisha maisha yao kila siku. Mapema mwaka huu, helikopta iliyokuwa ikifanya uokoaji wa matibabu ilishambuliwa na makundi yenye silaha katika jimbo la Kivu Kaskazini Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) katika jimbo la Kivu Kaskazini.

Wakati wa sherehe za kukabidhi medali Sudan Kusini walinda amani walikuwa wabunifu kwa kutumia matingatinga kama pazia kwa ajili ya gwaride
UNMISS/Isaac Billy
Wakati wa sherehe za kukabidhi medali Sudan Kusini walinda amani walikuwa wabunifu kwa kutumia matingatinga kama pazia kwa ajili ya gwaride

2. Matingatinga

Ili kujenga amani ya kweli, ulinzi wa amani unazingatia watu na mahitaji yao. Katika nchi zilizoathiriwa na migogoro, upotevu na ukosefu wa miundombinu muhimu kama vile shule, vifaa vya matibabu, barabara na madaraja huzuia juhudi zozote za kusaidia jamii kujenga amani endelevu. Ndiyo maana wahandisi na wasanifu katika shughuli za kulinda amani ni muhimu katika kusaidia watu kujikwamua na kujijenga upya kutokana na uharibifu wa vita na majanga ya asili.

"Tunaokoa watu sio kutokana na risasi bali pia mafuriko," amesema Kapteni Taimoor Ahmed, mhandisi anayefanya kazi na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS. Kwa kutumia wachimbaji na vifaa vingine vya ujenzi, timu yake ilijenga mitaro kusaidia mamia ya watu waliokwama kutokana na mafuriko makubwa huko Bentiu. Pia walijenga barabara kando ya mitaro ili kuhakikisha kwamba vifaa muhimu vya kibinadamu vinawafikia watu waliotawanywa na janga hilo.

Nje kidogo ya mji mkuu wa Sudan Kusini Juba, walinda amani walijenga madarasa mapya, uwanja wa mpira na uwanja wa michezo kwa ajili ya shule ndogo inayohudumia jamii ambayo inategemea zaidi kilimo cha kujikimu na ina uwezo mdogo wa kupata elimu. Nchini DRC, walinda amani walijenga Kituo cha Matibabu ya Ebola huko Kivu Kaskazini na kukarabati na kupanua barabara hadi kituo hicho wakati wa kilele cha mlipuko wa ugonjwa huo nchini humo.

Picha iliyopigwa kutoka angani au satiliti inaonyesha umati mkubwa wa watu waliokimbia makazi yao wakitembea kando ya Barabara ya Salah al-Din, karibu na Gaza City.
© U.S. Department of State/Maxar
Picha iliyopigwa kutoka angani au satiliti inaonyesha umati mkubwa wa watu waliokimbia makazi yao wakitembea kando ya Barabara ya Salah al-Din, karibu na Gaza City.

3. Picha za satelaiti

Katika miongo miwili iliyopita, upigaji picha wa satelaiti umetumika katika operesheni za kulinda amani ili kutoa muhtasari mzuri wa maeneo yenye migogoro, na hivyo kuimarisha ufahamu wa hali kwa kiasi kikubwa. Askari wa kulinda amani, ambao ni wataalam wa uchunguzi na jiografia, hutumia picha za satelaiti kufuatilia mienendo ya wanajeshi, mwelekeo na mtiririko wa watu kuhama, tishio na mienendo ya vikundi vilivyojihami na athari za majanga ya asili yanayokuja.

Kwa taarifa hizo muhimu, wanaweza kufanya maamuzi sahihi, kupanga doria ipasavyo na kuratibu hatua. Upigaji picha wa satelaiti, ni mojawapo ya zana bunifu zaidi zinazopatikana kwa ulinzi wa amani, husaidia kuongeza ufahamu wa utendaji kazi katika operesheni nyingi, hasa zile katika nchi zilizo na maeneo makubwa, ya mashambani na magumu. Taswira za wakati halisi za maeneo yasiyofikika pia huwezesha walinda amani kutathmini kwa haraka kiwango cha uharibifu au mahitaji yoyote na kutanguliza msaada wao ipasavyo.

Nchini Mali, ambako Ujumbe wa Umoja wa Mataifa MINUSMA ulitumwa kuanzia Aprili 2013 hadi Desemba 2023, picha za satelaiti zilisaidia kutambua njia zinazotumiwa na wasafirishaji haramu wa binadamu kaskazini mwa nchi. Nchini DRC, taswira kutoka angani zinatumika kufuatilia mienendo ya makundi yenye silaha, kufuatilia shughuli haramu za uchimbaji madini na kutathmini athari za migogoro kwa raia.

Nchini Sudan Kusini, takwimu za satelaiti zinatumika kwa madhumuni mbalimbali, kuanzia ufuatiliaji wa kujiandaa, kukabiliana na maafa ya majanga ya asili hadi kufuatilia mifumo ya uhamishaji na mienendo ya watu kuvuka mpaka. Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Cyprus, ambacho kilianzishwa kufuatilia makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya jumuiya za kisiwa cha Ugiriki na Kituruki vya Cyprus, kinatumia takwimu hizo kufuatilia shughuli kwenye eneo la mzozo.

Mtegua mabomu wa UNIFIL kutoka Cambodia akitegua bomu la ardhini kwenye ukanda wa buluu (usio na mapigano) kusini mwa Lebanon.
UN/Pasqual Gorriz
Mtegua mabomu wa UNIFIL kutoka Cambodia akitegua bomu la ardhini kwenye ukanda wa buluu (usio na mapigano) kusini mwa Lebanon.

4. Vitambuzi vya mabomu

Vitambuzi vya mabomu vimechukua jukumu muhimu katika kuokoa maisha ya watu wengi ulimwenguni. Kuanzia Angola hadi Cambodia, mabomu ya kutegwa ardhini yanasalia kuwa urithi wa kutisha wa vita, kuua au kuwalemaza raia wengi. Leo hii, karibu nchi na maeneo 70 yana mabomu ya kutegwa ardhini. Huduma ya Umoja wa Mataifa ya msaada wa uteguzi wa mabomu UNMAS inapeleka wateguzi wa mabomu katika takriban nchi na maeneo 20, ikiwa ni pamoja na katika operesheni za kulinda amani, ili kugundua na kuharibu mabomu hayo.

Usafishaji wa mabomu ya kutegwa ardhini sio tu kwamba huzuia kupoteza maisha ya watu na miguu na mikono yao, pia hufanya ardhi kuwa salama na yenye tija tena, kuruhusu jamii za wenyeji kulima au kujenga shule au hospitali, kimsingi kujenga upya maisha na riziki zao. Kwa bahati mbaya, gharama ya kusafisha mabomu yakutegwa ardhini inaweza kuwa na madhara kwa maisha ya wateguzi. Katika miaka ya hivi majuzi, vifo miongoni mwa wateguzi wa mabomu vimetokea katika maeneo kadhaa, ikiwa ni pamoja na Afghanistan, Sudan Kusini na Syria.

Wateguzi wa mabomu wanajilindaje? Wanavaa vifaa vya kinga za binafsi kama vya suti za mlipuko, helmeti, glavu na buti. Wanatumia vigunduzi vya chuma, na gari za kusafisha mabomu ya kutegwa ardhini kugundua na kuharibu mabomu hayo. Vitambuzi, vinavyotumia mawimbi ya sumaku ya umeme kutambua chuma, ni muhimu katika kupata mabomu ya ardhini yaliyozikwa.

Kuna vikwazo kwa vigunduzi hivyo, lakini kwa ujumla vimethibitishwa kuwa na ufanisi mkubwa katika kupunguza hatari. Tangu mwishoni mwa miaka ya 1990, zaidi ya mabomu milioni 55 ya kutegwa ardhini yameharibiwa, zaidi ya nchi 30 zimekuwa huru dhidi ya mabomu hayo na majeruhi wamepungua kwa kiasi kikubwa.

Katika siku ya Radio duniani 2024 mkuu wa Radio Okapi Joyce Fernandes de Piña na Theresa Kankou meneja mawasiliano ya kijamii wa Radio ya kijamii wakijadili nguvu ya Radio
Radio Okapi
Katika siku ya Radio duniani 2024 mkuu wa Radio Okapi Joyce Fernandes de Piña na Theresa Kankou meneja mawasiliano ya kijamii wa Radio ya kijamii wakijadili nguvu ya Radio

5. Redio

Redio inaweza isiwe kitu cha kwanza tunachofikiria tunapotafuta habari hii leo, lakini inasalia kuwa chombo chenye nguvu cha mawasiliano katika sehemu nyingi za dunia, ikiwemo katika nchi ambako ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa upo.

Redio imekuwa na jukumu muhimu katika operesheni nyingi tangu mwishoni mwa miaka ya 1980. Leo, operesheni tatu za kulinda amani zina vituo vyake vya redio ambavyo ni Radio Miraya nchini Sudan Kusini, Radio Okapi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC na Guira FM nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR. Walinda amani, ambao ni watayarishaji wa vipindi vya redio na wafanyakazi wa mawasiliano, hutumia redio kwa habari muhimu, tahadhari za mapema kuhusu vitisho vinavyoweza kutokea, mijadala kuhusu masuala muhimu na programu za elimu, kuwezesha jamii kufanya maamuzi sahihi. Zaidi ya hayo, hutoa jukwaa muhimu kwa sauti na mitazamo ya wenyeji, kusaidia kukuza upatanisho kati ya jamii zilizogawanyika.

Kwa nini redio inafanya kazi vizuri zaidi kuliko magazeti, televisheni au mtandao? Upokeaji wa vipindi vya redio na masafa ni ya gharama nafuu na vinapatikana kwa wingi, hata katika maeneo ya mashambani zaidi. Katika maeneo yenye viwango vya chini vya kujua kusoma na kuandika, vipindi vya redio vinaweza kufikia hadhira pana zaidi, na hivyo kukuza njia jumuishi zaidi ya kushiriki habari. Redio pia inaweza kutoa habari katika lugha za wenyeji kwa wakati halisi.

Kwa kuzingatia ufikiaji wake, redio ni chombo cha kutegemewa cha kupinga habari potofu na kuondoa uvumi ambao unaweza kudhuru usalama na afya ya watu. Wakati wa janga la coronavirus">COVID-19, Redio Miraya, ambayo inafikia theluthi mbili ya Sudan Kusini, iliendesha programu za kusaidia kukabiliana na upinzani wa wakazi wa eneo hilo kwa umbali wa kujitenga kimwili. Nchini DRC, Redio Okapi ilifanya kazi na Serikali ya Congo kutoa elimu hewani kwa takriban watoto milioni 22 ambao hawakuweza kuondoka nyumbani kwao, wakisambaza masomo muhimu ya Kifaransa, hesabu na kusoma.