UN yaenzi kujitolea na ujasiri wa walinda amani

27 Mei 2021

Mchango wa vijana katika kuleta amani haupingiki na kuanzia Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR hadi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC mpaka Lebanon, walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanafanya kazi na vijana kupunguza machafuko na kudumisha amani, ikiwemo upokonyaji wa silaha, kuwakusanya na kuwarejesha tena katika jamii na kuwaingiza katika program za kupunguza machafuko katika jamii.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres leo katika hafla ya kuweka shada la maua kuwakumbuka na kuwaenzi walinda amani wa Umoja wa Mataifa waliopoteza maisha kazini ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya walindamani duniani.

Ameongeza  kuwa walinda amani vijana huleta mawazo mapya, matumaini na nguvu kwa shughuli za Umoja wa Mataifa kwa kujishughulisha vyema na jamii za watu wanaowahudumia, na kuchangia kuboresha utendaji wa jumla na utekelezaji wa majukumu yao. 

"Tunaenzi kujitolea na ushujaa wa walinda amani wetu wote wanawake na wanaume, vijana na watu wazima na tunashukuru kwa huduma yao na kujitolea kwao", amesisitiza mkuu wa Umoja wa Mataifa. 

Ameongeza kuwa "Wanastahili msaada wetu kamili, na lazima tuendelee kushirikiana ili kufanya kila tuwezalo kuboresha usalama wao na ulinzi wao na kuwapa zana zinazohitajika ili waweze kufanikiwa".

Ikiadhimishwa kila mwaka 29 Mei, siku ya walinda amani inatoa fursa ya kutoa heshima kwa mchango muhimu ambao wafanyikazi haom wanaovalia sare na raia hutoa kwa kazi za shirika na kuwaenzi wale ambao wamejitolea maisha yao katika mchakato huu.

Daima wataenziwa

Awali Katibu Mkuu aliweka shada la maua kwenye makumbusho ya walinda amani yaliyoko kwenye makao makuu wa Umoja huo mjini New York Marekani kwa kuwaenzi walinda amani zaidi ya 4,000 wanawake na wanaume waliopoteza maisha yao tangu mwaka 1948 hadi sasa wakati wakihudumu chini ya bendera ya Umoja wa Mataifa.

Mashambulizi ya makusudi, ajali na maradhi ikiwemo ya COVID-19 vyote vimekuwa mwiba kwa walinda amani wa kijeshi na kiraia katika mwaka uliopita amesema Katibu Mkuu akitoa pole kwa familia za wa;liopoteza maisha na kusisitiza kuwa “Daima tutakuwa na deni nao. Kujitolea maisha yao hakutosahaulika na daima watakuwa katika mioyo yetu. Changamoto na vitisho vinavyowakabili walinda amani ni vikubwa na ninajivunia kazi kubwa wanayoifanya.”

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter