Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Amani ni pamoja kuwapatia huduma za afya wananchi DRC- Mlinda amani TANZBATT_8  

Private  Monica Constantino Nyagawa, analinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC chini ya bendera ya Umoja wa MAtaifa. Yeye anatoka Tanzania.
MONUSCO
Private Monica Constantino Nyagawa, analinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC chini ya bendera ya Umoja wa MAtaifa. Yeye anatoka Tanzania.

Amani ni pamoja kuwapatia huduma za afya wananchi DRC- Mlinda amani TANZBATT_8  

Amani na Usalama

Walinda amani wa Tanzania wanaohudumu katika kikosi cha 8, TANZBATT_8 kwenye Brigedi ya kujibu mashambulizi, FIB ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, MONUSCO wamezungumzia kile ambacho wanafanya katika kusongesha jukumu la Umoja wa Mataifa la kulinda amani kwenye taifa hilo lililogubikwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kwa miongo kadhaa sasa.

Walinda amani hao wakiwa na umri wa kati ya miaka 23 na 24, wametoa kauli zao wakati huu ambapo kesho tarehe 29 mwezi Mei ni siku ya walinda amani duniani na ujumbe ukiwa nafasi ya vijana katika amani na usalama duniani; matumizi ya nguvu ya vijana. 

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania wanaohudumu MONUSCO nchini DRC wakizungumza na wananchi wakazi wa jimbo la Kivu Kaskazini.
TANZBATT_8/Kapteni Tumaini Bagambo.
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania wanaohudumu MONUSCO nchini DRC wakizungumza na wananchi wakazi wa jimbo la Kivu Kaskazini.

Kiswahili kinatusaidia sana kwenye doria 

Private Stephano Odhiambo akizungumzia uwepo wake DRC anasema, “jukumu letu kubwa ambalo ni la msingi sana ni ulinzi wa raia. Ulinzi wa raia tunaufanya kwa kushiriki katika doria mbalimbali, ambazo kuna za kila siku, za kila wiki, doria tofauti tofauti za miguu tukishirikiana na jeshi la serikali ya DRC, FARDC. Lugha yetu ya Kiswahili imekuwa ni lugha ambayo inatusaidia katika kufanya majukumu yetu ya kila siku na kupata taarifa za adui sehemu tofauti tofauti.” 

Akizungumzia mafanikio kutokana na doria wanazofanya, Private Odhiambo ametaja ni pamoja na usalama katika njia  kutoka mjini Beni kupitia Mbao, Simulike hadi Kamango jimboni Kivu Kaskazini. “Hii njia imefanikiwa kufunguka. Zamani ilikuwa ni njia ambayo haipitiki kirahisi, kwani ilikuwa imeshaota hadi majani. Lakini kwa sasa hivi njia hii inatumika, raia wanaendelea kufanya majukumu yao ya msingi kila siku.” 

Pili ametaja mji wa Mutwanga, watu wameanza kurejea kwenye makazi yao, “tukiangalia ni Desemba tu palikuwa ni pahali ambapo hapakaliki kabisa. Lakini sasa hivi raia wamerejea, wanalima na kuendelea na shughuli zao za kila siku.” 

Tunazingatia kanuni za UN kwenye ulinzi wa amani 

Kwa Private Frederick Urassa Paul, akazungumzia kanuni na taratibu zilizowekwa na Umoja wa Mataifa kwa watendaji wanaofanyia kazi chombo hicho wakiwemo wanajeshi, polisi na raia. “Umoja wa Mataifa unakataza watendaji hao kujihusisha na ukatili wa kingono, au unyanyasaji wa kijinsia ikitaja watoto na wanawake ili kuepusha migogoro kati ya vikosi vya Umoja wa Mataifa na raia. Pia tunapaswa kuheshimu sheria na taratibu, mila na desturi za nchi husika. Sisi ni watanzania tuna sheria, mila na desturi zetu lakini hicho hakipaswi kutukwamisha kufanya kazi DRC kwa kuwa tunapaswa kuheshimu sheria, mila na tamaduni zao.” 

Akizungumzia apendacho ni vile wanakutana na walinda amani kutoka mataifa mbali mbali na kuheshimu tamaduni na mila zao. 

Walinda amani wanawake kutoka Tanzania wanaohudumu kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO wakizungumza na wakazi wa Kivu Kaskazini.
TANZBATT_8/Kapteni Tumaini Bagambo.
Walinda amani wanawake kutoka Tanzania wanaohudumu kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO wakizungumza na wakazi wa Kivu Kaskazini.

Tunafundisha wanawake stadi za kazi ili kuongeza kipato 

Kando ya majukumu ya ulinzi wa amani kwa kufanya doria, walinda amani pia wanashirki katika kutoa huduma za afya. Private Monica Nyagawa ni muuguzi katika hospitali ya TANZBATT_8 yenye makao yake mjini Beni.  

Private Nyagawa anasema “napenda kutoa huduma ya matibabu kwa walinda amani wa Tanzania na wa mataifa mengine.”  

Brigedi ya FIB ina walinda amani kutoka Tanzania, Afrika Kusini na Malawi huku walinda amani kutoka Bangladesh wakiwa na jukumu la kusindikiza doria.  

Mlinda amani huyo anasema anapata faraja pia atoapo huduma kwa raia iwe ni majeraha au magonjwa ya kawaida kwa kuwa mjni Beni wamezungukwa na raia na kwamba “amani si katika kutokuwepo kwa vita bali pia amani ni katika afya bora.”  

Joyce Akany Tweve, mlinda amani kutoka Tanzania akihudumu chini ya bendera ya Umoja wa Mataifa huko DRC.
MONUSCO
Joyce Akany Tweve, mlinda amani kutoka Tanzania akihudumu chini ya bendera ya Umoja wa Mataifa huko DRC.

Private Joyce Tweve ni mtunza kumbukumbu na anasema “pamoja na ulinzi wa amani najifunza kutunza kumbukumbu ambazo ni muhimu pindi ambapo jambo linatokea na linahitaji ufuatiliaji.” 

Koplo Lucas Matiku ni mlinda amani mwandishi wa habari akisema “tumekuwa tukielezea wananchi wa DRC jitihada za MONUSCO na FARDC za kuleta amani na zaidi ya yote ni kwamba vyombo vya habari vikitumika vibaya vinaweza kutowesha amani na vikitumika vibaya vinasambaratisha nchi.” 

Umoja wa Mataifa unapigia chepuo uwepo wa wanawake kwenye ulinzi wa amani na hivyo Private Justina Malengwa anasema, “mimi jukumu langu kubwa ni kukutana na wanawake na kusikiliza changamoto zao, na tunazitatua. Pale tunapokutana nao wanapata imani na pia tunawafundisha stadi mbalimbali za kujipatia kipato ikiwemo kusuka, kufuma na hata mapishi.”