Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makumi ya watu wameripotiwa kuuawa katika shambulio kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani Rafah: UN

Hospitali ya Kimataifa ya Kikosi cha Medical Corps huko Rafah, Gaza wamekuwa wadau muhimu wa matibabu
WFP
Hospitali ya Kimataifa ya Kikosi cha Medical Corps huko Rafah, Gaza wamekuwa wadau muhimu wa matibabu

Makumi ya watu wameripotiwa kuuawa katika shambulio kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani Rafah: UN

Amani na Usalama

Makumi ya watu wanaaminika kufariki dunia katika shambulio la Israel la usiku wa kuamkia leo kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani huko Rafah kusini mwa Gaza, likiwa ni tukio la hivi karibuni la kutisha katika zaidi ya miezi saba ya vita kati ya jeshi la Israeli na wapiganaji wa Palestina, wamesema leo wahudumu wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa .

"Taarifa zinazotoka Rafah kuhusu mashambulizi zaidi dhidi ya familia zinazotafuta makazi ni za kutisha," limesema shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, kwenye chapisho lake kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X, baada ya ripoti za shambulio la kijeshi la Israel kwenye kambi ya mahema huko Tal as-Sultan kaskazini-magharibi mwa Rafah, pamoja na makazi mengine kaskazini mwa Jabalia, Nuseirat na mji wa Gaza.

Picha ambazo hazijathibitishwa zilizowekwa mitandaoni zinaonyesha makazi ya watu yaliyoteketea kwa moto na miili iliyoteketea katika eneo la shambulizi la Rafah.

UNRWA imeongeza kuwa pia "Kuna ripoti za vifo vingi ikiwa ni pamoja na watoto na wanawake miongoni mwa waliouawa. Gaza ni jehanamu iliyo duniani. Picha za jana usiku ni ushahidi mwingine wa hilo”.

Wakimbizi wa ndani wakiondoka Rafah kuhofia usalama wao
© WHO
Wakimbizi wa ndani wakiondoka Rafah kuhofia usalama wao

Kulaaniwa kimataifa

Akirejelea maoni hayo na kulaaniwa kwa kimataifa kwa shambulio hilo, Mtaalamu Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya makazi, Balakrishnan Rajagopal, ametoa wito wa "hatua za pamoja za kimataifa kusitisha vita”, siku chache tangu mahakama ya juu ya Umoja wa Mataifa itoe wito wa kukomesha ongezeko la operesheni za kijeshi za Israel katika eneo la Rafah.

Bwana. Rajagopal, mtaalam huru wa haki za binadamu ambaye si mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa ameendelea kusema kwamba "Kuwashambulia wanawake na watoto wakati wanapata hifadhi kwenye makazi yao huko Rafah ni ukatili wa kutisha. Tunahitaji hatua za pamoja za kimataifa kukomesha vitendo vya Israeli sasa."

Katika taarifa yake, jeshi la Israel limekanusha kuwalenga raia kwa makusudi na kusema kuwa shambulio hilo likuwa limepanga kwa ajili ya viongozi wawili wakuu wa Hamas. 

Shambulio hilo lilikuwa "shambulio la anga kaskazini magharibi mwa Rafah ambalo lilimuua Yassin Rabia na Khaled Nagar wote ni watendaji wa Hamas Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na linakwenda sanjari na sheria za kimataifa za kibinadamu”, limesema Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF).

Asilimia kubwa ya wakimbizi wa ndani Gaza wanahishi kwenye mahema
© UNRWA
Asilimia kubwa ya wakimbizi wa ndani Gaza wanahishi kwenye mahema

Hakuna mahali salama na hakuna aliye salama: UNRWA

Katika chapisho tofauti la mtandao wa kijamii shirika hilo la Umoja wa Mataifa pia limeelezea wasiwasi wake kuhusu usalama na hali ya wafanyakazi wenzao huko Gaza ambao mawasiliano yao yamepotea baada ya shambulio la Rafah.

"Hatuna njia ya mawasiliano iliyoanzishwa na wenzetu mashinani. Hatuwezi kuthibitisha eneo walipo na tunajali sana hatma yao, na ustawi wa watu wote waliofurushwa makwao ambao wanaoishi katika eneo hili. Hakuna mahali palipo salama. Hakuna aliye salama.”

Mbali na tishio kubwa la ghasia, wahudumu wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa wamesisitiza kuwa njaa bado ni hatari ya kila siku kwa watu wa Gaza.

Ucheleweshaji wa utoaji wa misaada unaendelea

Onyo hilo linakuja huku kukiwa na takriban kusitishwa kabisa kwa usafirishaji wa misaada ya kuokoa maisha tangu jeshi la Israel lilipokamata kivuko cha Rafah kutoka Misri kuelekea Gaza mapema mwezi huu, ili kujibu shambulio la roketi kwenye kivuko cha Kerem Shalom lililofanyika Mei 5 na kusababisha vifo vya Wanajeshi wanne wa Israeli ambao ni askari wa kikosi cha IDF.

Kulingana na mtandao wa UNRWA bidhaa za misaada ya Umoja wa Mataifa na mafuta yanayoingia Gaza kupitia Rafah na karibu na Kerem Shalom, hakuna malori ya misaada yaliyoingia katika eneo hilo tangu Jumapili iliyopita.

"Misaada ipo, umbali wa makumi ya kilomita kwenye mipaka wakati idadi kubwa ya watu inakaribia kufa njaa, amesema " Mkurugenzi wa Mipango wa UNRWA, Sam Rose, katika chapisho kwenye ukurasa wa X Jumapili jioni.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu na misaada ya dharura OCHA pia imethibitisha changamoto kubwa zinazoendelea za kupokea na kuwasilisha misaada kote Gaza, ikitoa mfano wa ucheleweshaji wa mara kwa mara, ukaguzi wa kiholela na vikwazo vya ufikiaji vinavyowekwa na mamlaka ya Israeli.

Wanafamilia wakikimbia Rafah na kile wanachoweza kubeba
© UNICEF/Eyad El Baba
Wanafamilia wakikimbia Rafah na kile wanachoweza kubeba

Shinikizo la operesheni za misaada

Kati ya tarehe 1 na 23 Mei, operesheni 31 za misaada zilinyimwa ruhusa ya ufikiaji wa watu na 40 zilizuiliwa, ikiwa ni pamoja na "kucheleweshwa kwa muda mrefu, kuwaweka kizuizini wafanyakazi wa misaada, kufyatua risasi za onyo na kulazimisha kufutwa kwa misheni iliyoidhinishwa rasmi", ilisema shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA katika chapisho lake kwenye mtandao wa X jana Jumapili.

"Iwapo chakula na misaada ya kibinadamu haitaanza kuingia Gaza kwa wingi, hali ya kukata tamaa na njaa itasambaa Gaza” limesema Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa WFP pia likionya leo baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kuelezea wasiwasi wake kwamba operesheni ya kibinadamu inakaribia kusambaratika.

"Katibu Mkuu amesisitiza kwamba mamlaka ya Israel lazima kuwezesha uchukuaji salama na utoaji wa misaada ya kibinadamu kutoka Misri inayoingia kupitia Kerem Shalom kwa wale wanaohitaji," amesema msemaji wa Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa katika taarifa iliyotolewa Jumapili, baada ya kuripotiwa kupitishwa kwa misaada na mafuta kutoka Misri hadi Gaza kupitia Kerem Shalom.

"Katibu Mkuu amesisitiza wito wake wa kusitishwa mapigano mara moja na kuachiliwa mara moja na bila masharti kwa mateka wote ili kukomesha mateso ya raia," taarifa hiyo ilibainisha, na kuongeza kuwa Bwana Guterres "amesikitishwa na kutotekelezwa kwa amri za hivi karibuni za Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ kuhusu hali ya Gaza tarifa hiyo ikiongeza kuwa "Maamuzi ya Mahakama ni ya lazima."