Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hofu ya uvamizi wa ardhini Rafah yatanda Gaza - UN

Hali katika Ukanda wa Gaza inazidi kuzorota huku mzozo ukiendelea.
© UNRWA
Hali katika Ukanda wa Gaza inazidi kuzorota huku mzozo ukiendelea.

Hofu ya uvamizi wa ardhini Rafah yatanda Gaza - UN

Amani na Usalama

Gaza, Leo wakati changamoto ya kukatika kwa umeme ikiendelea katika ukanda huo na kwingineko pia mashirika ya Umoja wa Mataifa yamesema mashambulizi ya anga yakiendelea kulenga mji wa kusini mwa Gaza wa Rafah na kusambaa kwa ripoti kwamba vikosi vya Israel vimefanya operesheni ya kijeshi ndani ya jengo la hospitali ya Nasser, wasiwasi juu ya uwezekano wa uvamizi wa ardhini wa mji huo wa mpakani wenye wakazi wengi unazidi kuongezeka.

Jeshi la Israel lilithibitisha leo Alhamisi katika ujumbe wa mtandao wa X kwamba vikosi vyake maalum vilifanya kile walichokiita "operesheni sahihi na ndogo" ndani ya hospitali ya Nasser kusini mwa Gaza, ambacho kituo kikubwa zaidi cha afya kinachofanya kazi katika eneo hilo. 

Kupitia ukurasa wake wa X jana Jumatano, Tedros Adhanom Ghebreyesus, mkurugenzi mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani WHO, alielezea wasiwasi wake juu ya hali inayozidi kuwa mbaya hospitalini.

Mkurugenzi huyo amesema "Ufikiaji wa hospitali unabaki kuwa kizuizi hakuna eneo salama kwa wale wanaohitaji msaada. Misheni mbili za WHO zimekataliwa katika siku nne zilizopita na tumepoteza mawasiliano na wafanyikazi wa hospitali," 

Ametoa wito wa upatikanaji wa fursa ya kibinadamu na ulinzi wa hospitali ndhidi ya wapiganaji wote, akisisitiza kwamba lazima hospital zibaki kuwa mahali salama kwa raia.

Mahema ya watu waliokimbia makazi yao huko Rafah, kusini mwa Gaza.
© UNRWA
Mahema ya watu waliokimbia makazi yao huko Rafah, kusini mwa Gaza.

Rafah hali ni mbaya

Taarifa ya hivi karibuni kutoka kwa shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA, linaangazia "harakati za watu mbali na mji wa mpakani wa kusini kuelekea Deir al Balah na kambi ya wakimbizi ya Nuseirat.”

Mapema wiki hii, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP lilieleza wasiwasi wake kwamba kuhama zaidi kutoka katika jiji hilo lenye watu wengi kwenye mpaka wa Misri kunaweza kuzidisha hali mbaya ya wale wanaotafuta hifadhi huko.

Leo Matthew Hollingworth, Mkurugenzi wa WFP katika eneo linalokaliwa la Palestina, ameelezea mitaa ya Rafah kama ni eneo "lililofurika umati wa watu," akibainisha kuwa kila eneo linalopatikana katika jiji hilo limekuwa makazi ya muda ya wakimbizi wa ndani.

Mji huo sasa una wakazi wapatao milioni 1.5 wa Gaza waliokimbia makazi yao kutokana na vita.

Bwana Hollingworth, akizungumza katika video iliyotolewa kupitia kwenye jukwaa la X, ameangazia hali ya kukata tamaa iliyotawala Rafah, “ambapo watu wanachangamoto ya kupata usaidizi, mafuta na riziki katika hali ya unyevu, baridi, na Maisha duni".

Wakati WFP ikiendelea kutoa misaada kwa wananchi wa Gaza mjini Rafah, mashirika kama vile Action Against Hunger ambayo yanafanya kazi bega kwa bega na wasaidizi wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, yanaonya juu ya kulazimika kusimamisha shughuli kama operesheni za ardhini za Israel zitapanuka hadi Rafah.

Wakati huo huo, mashambulizi makali ya Israel yanaendelea kote Gaza, na kusababisha hasara zaidi ya Maisha ya raia na uharibifu wa miundombinu.

Idadi ya vifo inaongezeka

Wizara ya Afya huko Gaza inaripoti kuwa idadi ya vifo vya Wapalestina sasa imefikia 28,576 na 68,291 wamejeruhiwa tangu Oktoba 7, 2023. 

Na kati ya Februari 13 na 14, Wapalestina 103 waliuawa na wengine 145 kujeruhiwa.

Kwa upande wa Israel imesema wamepoteza maisha ya wanajeshi wake 230 waliouawa na 1,352 kujeruhiwa tangu kuanza kwa operesheni ya ardhini, huku zaidi ya Waisraeli 1,200 na raia wa kigeni wakiuawa wakati wa mashambulizi dhidi ya Israel, haswa wakati wa mauaji yaliyoongozwa na Hamas Oktoba 7 mwaka jana.

Takriban watu 134 wamesalia mateka huko Gaza, kulingana na mamlaka ya Israeli.