Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi wa mashirika ya kibinadamu washikamana kupaza sauti kuhusu zahma ya Gaza

Vitongoji huko Khan Younis, kusini mwa Gaza, vimegeuzwa vifusi.
© WHO/Christopher Black
Vitongoji huko Khan Younis, kusini mwa Gaza, vimegeuzwa vifusi.

Viongozi wa mashirika ya kibinadamu washikamana kupaza sauti kuhusu zahma ya Gaza

Amani na Usalama

Katika wito wa pamoja, wakuu wa mashirika ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa na mashirika yasiyo ya kiserikali ya kimataifa wamewasihi viongozi wa dunia kusaidia kuzuia kuzorota zaidi kwa mgogoro wa Gaza ambao umesababisha makumi ya maelfu ya Wapalestina wengi wao wakiwa wanawake na watoto kuuawa.

Tangu mashambulizi ya kikatili ya Oktoba 7 mwaka jana yaliyofanywa na Hamas na wanamgambo wengine kusini mwa Israel na mashambulizi ya kijeshi yaliyofuata ya Israel huko Gaza, zaidi ya robo tatu ya wakazi wa eneo hilo wameyakimbia makazi yao, wengi mara nyingi.

Kuna uhaba mkubwa wa chakula, maji na usafi wa mazingira, na mfumo wa afya unaendelea kuharibiwa kwa utaratibu, na matokeo ya janga linaloendelea, wamesema wakuu wa Kamati ya Kudumu ya Mashirika ya Kimataifa (IASC), chombo cha kuratibu mashirika ya kibinadamu duniani.

“Magonjwa yamekithiri. Njaa inakuja. Maji ni katika mteremko. Miundombinu ya msingi imeharibiwa. Uzalishaji wa chakula umesimama. Hospitali zimegeuka kuwa uwanja wa vita. Watoto milioni moja wanakabiliwa na kiwewe kila siku,” wamesema wakuu hao kwenye taarifa yao iliyotolewa jana Jumatano.

Pigo kubwa kwa juhudi za misaada

Hali ni mbaya sana huko Rafah, kusini mwa Gaza. "Rafah, kimbilio la hivi karibuni la zaidi ya watu milioni moja waliofurushwa kwenye makazi yao, wenye njaa na waliopatwa na kiwewe waliojazana katika eneo dogo la ardhi, imekuwa uwanja mwingine wa vita katika mzozo huu wa kikatili," wamesema wakuu wa IASC.

Wameonya kuwa "Kuongezeka zaidi kwa ghasia katika eneo hili lenye wakazi wengi kunaweza kusababisha hasara kubwa. Inaweza pia kusababisha pigo kubwa sana kwa hatua za misaada ya kibinadamu ambayo tayari imeathirika vibaya.” 

Vita nchini Ukraine vimesababisha uharibifu mkubwa wa makazi na miundombinu ya umma.
© EU/Oleksandr Rakushnyak
Vita nchini Ukraine vimesababisha uharibifu mkubwa wa makazi na miundombinu ya umma.

Wafadhili wa kibinadamu wako hatarini

Wakuu wa IASC wameangazia hatari zinazokabili wafanyikazi wa misaada kila siku katika juhudi zao za kusaidia watu walio na uhitaji mkubwa, na kuongeza kuwa wanaweza "kufanya mengi tu endapo watapatiwa fursa."

"Wafanyikazi wa kibinadamu, wenyewe wamehamishwa na kukabiliwa na mashambulizi ya makombora, vifo, vizuizi katika harakati zao na kuvunjika kwa utaratibu wa kiraia, lakini wanaendelea na juhudi za kuwasilisha msaada kwa wale wanaohitaji zaidi," wamesema.

Pia wameongeza kuwa "Lakini wahudumu hao wa misaada wanakabiliwa na vizuizi vingi ikiwa ni pamoja na vizuizi vya usalama na na kufikisha misaada, endapo watapewa fursa wanaweza kufanya mengi tu."

Mambo muhimu

Wakuu hao wamesisitiza kwamba hakuna kiasi cha operesheni za kibinadamu kitakachoziba pengo la miezi ya kunyimwa fursa za misaada ambayo familia huko Gaza zimevumilia.

"Hii ni juhudi yetu ya kuokoa operesheni za kibinadamu ili tuweze kutoa, angalau, vitu muhimu kama dawa, maji ya kunywa, chakula, na makazi kadiri hali ya joto inavyopungua," wamesema.

Kwa ajili hiyo, wamesisitiza haja ya vipengele 10 vya lazimaambavyo ni: 

  • Kusitisha mapigano mara moja 
  • Ulinzi wa raia na miundombinu ya raia 
  • Kuachiliwa mara moja kwa mateka 
  • Vivuko vya kuingia vya kuaminika kwa usaidizi 
  • Hakikisho la usalama na ufikiaji usiozuiliwa 
  • Mfumo unaofanya kazi wa arifa za kibinadamu 
  • Barabara zilizoondolewa vifaa vya milipuko 
  • Na mtandao thabiti wa mawasiliano.

Aidha, wametoa wito kwa shirika la Umoja wa Mataifa linalosaidia wakimbizi wa Kipalestina UNRWA kupewa rasilimali inazohitaji kutoa msaada wa kuokoa maisha na kusitishwa kwa kampeni za kutaka kudhalilisha Umoja wa Mataifa na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayofanya kila liwekanalo kuokoa maisha.

viongozi hao wa kibinadamu waahitimisha tarifa yao ya pamoja wakisema "Tunatoa wito kwa Israel kutimiza wajibu wake wa kisheria, chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu, kutoa chakula na vifaa vya matibabu na kuwezesha shughuli za misaada, na kwa viongozi wa dunia kuzuia janga baya zaidi kutokea.