Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ninalaani vikali shambulio la Israel katika kambi ya wakimbizi wa ndani Rafah: Wennesland

Tor Wennesland, Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa wa Mchakato wa Amani ya Mashariki ya Kati
UN Photo/Eskinder Debebe
Tor Wennesland, Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa wa Mchakato wa Amani ya Mashariki ya Kati

Ninalaani vikali shambulio la Israel katika kambi ya wakimbizi wa ndani Rafah: Wennesland

Amani na Usalama

Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati Tor Wennesland amelaani vikali shambulizi la anga la jeshi la Israel jana usiku ambalo limepiga kambi ya wakimbizi wa ndani katika mji wa Rafah Kusini mwa Gaza.

Katika taarifa yale iliyotolewa leo mjini Jerusalem Bwana wennsland amesema “Shambulio hilo limeripotiwa kusababisha vifo vya zaidi ya Wapalestina 35 wakiwemo wanawake na Watoto na kujeruhi makumi ya wengine.”

Ameongeza kuwa “Wakati jeshi la Israel IDF imesema ililenga kituo cha Hamas na kuua wanamgambo wawili wakuu wa Hamas katika shambulio hilo, ninasikitishwa sana na vifo vya wanawake na watoto wengi katika eneo ambalo watu wamesaka makazi.”

Hivyo ametoa wito kwa mamlaka ya Israel kufanya uchunguzi wa kina na wa uwazi kuhusu tukio hilo, kuwawajibisha wale wanaliohusika na makosa yoyote, na kuchukua hatua za haraka kulinda vyema raia.

Pia amezitaka pande zote katika mzozo “lazima zijiepushe na vitendo vinavyotuweka mbali zaidi na kufikia lengo la kukomesha uhasama na kuhatarisha zaidi hali ambayo tayari ni tete katika ardhi na eneo kubwa.”

Wennesland amesisitiza tena wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kusitisha mapigano mara moja na kuachiliwa mara moja na bila masharti mateka wote ili kukomesha mateso ya raia.

Amemalizia taarifa yake kwa kusema Umoja wa Mataifa bado upo imara katika kujitolea kwake kuunga mkono juhudi zote zinazolenga kumaliza uhasama, kupunguza mivutano na kusongesha mambo ya amani katika Ukanda wa Gaza.”