Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Elimu zaidi yahitajika kuepusha mauaji ya kimbari duniani – Bi. Nderitu

Alice Nderitu, Mshauri Maalum wa  Umoja wa Mataifa katika kuzuia mauaji ya kimbari.
UN News
Alice Nderitu, Mshauri Maalum wa Umoja wa Mataifa katika kuzuia mauaji ya kimbari.

Elimu zaidi yahitajika kuepusha mauaji ya kimbari duniani – Bi. Nderitu

Amani na Usalama

Mshauri Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuzuia mauaji ya kimbari, Alice Nderitu amesema anatiwa wasiwasi sana na kile kinachoendelea duniani kutokana na viashiria mauaji ya kimbari na iwapo dunia imejifunza kutokana na kile kilichotokea Rwanda na kule Srebrenica.

Bi. Nderitu akizungumza na Eugene Uwimana, Afisa Mawasiliano wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Rwanda, amesema natiwa wasiwasi sana na nimeandika na kuzunguzma mara nyingi juu ya Gaza, Ukraine, Sudan, Myanmar, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC. Lakini  bado silaha bado zinatengenezwa na zinatumika.

Amesema watu hawaelewi bado umuhimu wa kuzuia mauaji, kwani silaha zinatumika na mauaji yakishatokea watu wanaanza kulalamika wakisema, “mbona hii inafanyika, mbona hii inaendelea.”

Kitabu cha kuelimisha kuhusu mwenendo wa kufanyika mauaji ya kimbari

“Sisi tuna nyaraka iitwayo Framework of Analysis au Mfumo wa Uchambuzi,” amesema Mshauri huyo maalum akiongeza kuwa kitabu hicho kiko kwa lugha ya kiingereza lakini sasa watakifanyia fasiri ili kiweze kusambazwa.

Kupitia kitabu hicho, ofisi yake inaeleza kuwa mahakama ndio inayoamua kuwa tukio lililotokea ni mauaji ya kimbari au la, “sisi wenyewe kazi yetu ni kusema iwapo kunafanyika mpango wa mauaji ya kimbari. Mfano ukiona hawa wanamgambo au vikundi visivyo vya kiserikali vinabeba silaha na si polisi wa serikali, au raia wanabeba bunduki na wanajipanga, hiyo sasa ni mojawapo ya kiashiria. Pia ukiona kama kuna kundi moja la watu limetengwa, na maneno fulani  ya chuki yanasemwa dhidi yao, pengine wao wanafanana na wanyama, au wao hawafai kuishi, sasa hapo unajua kuwa mauaji ya kimbari yanapangwa.”

Alice Nderitu, Mshauri Maalum wa  Umoja wa Mataifa katika kuzuia mauaji ya kimbari akiwa Kigali kwenye kumbukizi, akizungumza na Eugene Uwimana afisa mawasiliano wa ofisi ya mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Rwanda.
UN News
Alice Nderitu, Mshauri Maalum wa Umoja wa Mataifa katika kuzuia mauaji ya kimbari akiwa Kigali kwenye kumbukizi, akizungumza na Eugene Uwimana afisa mawasiliano wa ofisi ya mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Rwanda.

Wapi dunia imekosea hadi viashiria vya mauaji vinaonekana kwingineko?

Bi. Nderitu akiwa nchini Rwanda kushiriki kumbukizi ya miaka 30 ya mauaji ya kimbari nchini humo anaeleza kikubwa ni kwamba dunia haijaweka maanani katika masomo. Kila mwanafunzi duniani kote asome katika historia kulikuweko na mauaji ya kimbari dhidi ya watutsi na walitengwa si kwamba walifanya kosa, bali tu kwa  sababu waliishi.

Nini kifanyike?

Alipoulizwa nini kifanyike? Bi. Nderitu anasema ni lazima watoto wafundishwe kuhusu mauaji ya kimbari. Na pili kesi zilizofanyika Rwanda au duniani kote kuhusu mauaji ya kimbari, uamuzi wake usambazwe kwani mara nyingi watu wau wana wasiwasi kwa sababu hawajui nini kilifanyika.

“Ukiangalia ule  uamuzi wa majaji ndio ukweli kuhusu jambo lililotokea. Sasa ule  uamuzi wa majaji usikae tu kwenye masjala za mahakama, bali zisambazwe.”

Sijaona tembo wanapanga kuua tembo wenzao

Suala lingine ni kukubali kuwa mauaji  ya kimbari yalifanyika. Mwanadamu akifanya mauaji hayo anakuwa amezidi hata wanyama. “Sisi tuliotoka Afrika tuko na wanyama wengi. Mimi sijahai kuona tembo wanapanga mipango ya kwenda kuua tembo wengine. Hata hupati nyuki anapanga kwenda kuua nyuki wengine, hata siafu huwakuti. Sisi binadamu tu tena tunaojina tumepewa akili na Mungu ndio tunapanga kwenda kuua wengine kwa sababu tu eti wana tofauti, na hata kama hawana tofauti.”

Kwa mantiki hiyo suala lingine anasisitiza ni kuwafundisha watu wote, wakiwemo watoto na wafuatwe kokote pale waliko tena duniani kote. “Tuwafundishe wafahamu kuwa binadamu anaweza kufika mahali apangie mwenzake mauaji ya kimbari.”