Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunapokumbuka waliouawa Rwanda tukumbuke pia kutia saini mkataba wa kuzuia mauaji ya kimbari – UN

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (katikati) na washiriki wengine wakiwasha mishumaa katika hafla ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Tafakari juu ya Mauaji ya Kimbari ya mwaka 1994 dhidi ya Watutsi nchini Rw…
UN Photo/Loey Felipe
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (katikati) na washiriki wengine wakiwasha mishumaa katika hafla ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Tafakari juu ya Mauaji ya Kimbari ya mwaka 1994 dhidi ya Watutsi nchini Rwanda.

Tunapokumbuka waliouawa Rwanda tukumbuke pia kutia saini mkataba wa kuzuia mauaji ya kimbari – UN

Amani na Usalama

Ikiwa ni miaka 29 tangu kufanyika kwa mauaji ya kimbari nchini Rwanda dhidi ya Watutsi, Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa nchi wanachama wa Umoja huo kujiunga na Mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia na Kuadhibu Uhalifu wa mauaji ya Kimbari. 

Bwana Guterres ametoa wito huo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa wakati wa tukio maalum la kumbukizi ya mauaji ya kimbari ya Rwanda, tukio lililofanyika kwenye ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. 

Katibu Mkuu amesema pamoja na kujiunga na mkataba huo nchi wanachama lazima ziunge mkono ahadi zao kwa vitendo akisema kwa Pamoja hebu tuwe thabiti dhidi ya ongezeko la ukosefu wa stahmala. Hebu tuwe macho na tuwe tayari kuchukua hatua. 

Mauaji ya Kimbari Rwanda  

Mauaji hayo yalifanyika kwa siku 100 ambapo zaidi ya watu milioni moja wakiwemo Watoto, wanawake na wanaume waliuawa ambapo Katibu Mkuu amesema “tunaheshimu kumbukumbu ya waliopoteza maisha, wengi wao wakiwa Watutsi, lakini pia wahutu na wengineo waliopinga mauaji ya kimbari.” 

Na zaidi ya yote ni kutoa heshima kwa manusura akisema tunatambua safari ya wanyarwanda kuelekea uponyaji, ujenzi mpya na maridhiano.  

Lakini kikubwa zaidi “tunakumbuka, tena kwa aibu, kushindwa kwa jamii ya kimataifa. Kushindwa kusikiliza – na kushindwa kuchukua hatua. 

Katibu Mkuu amesema mauaji hayo hayakuanza ghafla bali yalipangwa kwa umakini na kutekelezwa kimfumo, hivyo amesema katu tusisahau hatari zitokanazo na utete wa uungwana kwenye jamii zote.  

Rais wa Baraza Kuu la 77 la Umoja wa Mataifa Csaba Kőrösi.
UN Photo/Loey Felipe
Rais wa Baraza Kuu la 77 la Umoja wa Mataifa Csaba Kőrösi.

Utete huo unazingatia ongezeko la kauli za chuki, akisema ni kengele inayolia kwa sauti kubwa kila uchao na kwamba kadri sauti inapoongezeka, vivyo hivyo tishio la kutokea kwa mauaji ya kimbari kwani kauli ya chuki hutangulia na huchochea ghasia.  

Amesema kauli kama hizo za chuki na propaganda vilifungua njia ya mauaji ya kimbari Rwanda ambapo kauli hizo zilitangazwa kwenye Televisheni, redio na  magazeti. 

Sasa kauli za chuki zinapaziwa sauti kwa ukubwa zaidi 

Hii leo spika za chuki ni kubwa kuliko. Kwenye intaneti, uchochezi wa ghasia, uongo, nadharia za kufikirika, kukanusha kufanyika kwa mauaji ya kimbari vinasambaa bila uthibitisho wowote. 

Ni kwa mantiki hiyo anataka mshikamano na ushirikiano zaidi wa kuhakikisha kuna uwajibikaji wa dhahiri na uwazi kwenye zama hizi za dunia ya kidijitali.  

Ametamatisha akisema, “hebu tukumbuke kwa dhati kabisa wanyarwanda wote waliouawa kwenye mauaji ya kimbari kwa kujenga mustakabali wenye utu, ulinzi, haki na haki za binadamu kwa wote.” 

Kilichotokea hakikuwa ajali, kilipangwa - Kőrösi

 

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Csaba Kőrösi akihutubia kwenye kumbukizi hiyo amesihi jamii ya kimataifa kuendelea kuzingatia haki ya kila mtu na kutatua vichocheo vya kauli za chuki mtandaoni na nje ya mtandao.

Ameeleza washiriki kuwa leo ni fursa ya kukumbuka kile kilichotokea pindi madaraka yanapotumika kwa hila na chuki sio tu inapuuzwa bali inachagizwa.

Amesema kilichotokea hakikuwa ajali bali “kilitokana na miaka ya kuchipuka kwa itikadi za kibaguzi na kampeni iliyokuwa na lengo la kutokomeza kimfumo jamii fulani.”

Hivyo amesema Kőrösi amesema hebu na tusimame thabiti dhidi ya aina zote za ubaguzi. Na hebu tuendelee kujikita katika elimu. Kwa kuzingatia kile ambacho kinatuzingira mwaka huu wa 2023, huu ni wajibu wetu. Na hebu tuwe wakweli, hili ndio chaguo letu pekee.