Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wadau nchini Kenya waitikia wito wa Umoja wa Mataifa wa kumwezesha mtoto wa kike

Ufunguzi wa kituo cha malezi ya watoto wachanga huko Kajiado nchini Kenya ili kuwezesha mama zao kurudi shule.
UN News
Ufunguzi wa kituo cha malezi ya watoto wachanga huko Kajiado nchini Kenya ili kuwezesha mama zao kurudi shule.

Wadau nchini Kenya waitikia wito wa Umoja wa Mataifa wa kumwezesha mtoto wa kike

Wanawake

Mkutano wa 68 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake duniani, CSW68 ulifunga pazia hivi majuzi jijini New York Marekani ukipigia chepuo uwekezaji kwa wanawake na wasichana, na leo tunabisha hodi nchini Kenya wasichana waliokumbwa na ujauzito utotoni na kukatishwa ndoto za kuendelea na masomo au kupata ajira wamepata jawabu la changamoto wanazokumbana nazo pindi wakijifungua watoto wao. 

Changamoto kama vile mahali pa kumwacha mtoto kwa malezi ili aweze kuendelea na shule au kupata ajira. Umoja wa Mataifa unasema kila mtu ana haki ya elimu hata kama amepata changamoto gani maishani. 

Na  ndipo ushirikiano kati ya mashirika ya kiraia lile la “Work for life”, pamoja na lile la “A Pack a Month”, linalohusika na utoaji wa misaada mbali mbali ikiwemo taulo za kike kwa wazazi wenye mahitaji na wasichana wanaokwenda shule walizindua kituo cha malezi ya watoto wachanga nyakati za mchana katika katika eneo la Ngong nchini Kenya. Mradi unaungwa mkono na wadau kadhaa ikiwemo serikali  ya Kenya. 

Neema, si jina lake halisi, ni msichana muathririka wa mimba za utotoni ambaye sasa ana umri wa miaka 19, ndoto zake za kuendelea na masomo zilikatizwa baada ya kupata mimba akiwa na umri mdogo.

“Nilipata mimba kwa wakati ambayo nilikuwa bado ninaendelea na masomo ya msingi. Ilikuwa vigumu sana kwa sababu ilibidi niache shule na baada ya kupata mtoto sikuweza kurudi shule kuendelea na masomo yangu kwa sababu ya unyanyapaa, na hasa kwa sababu nilikosa mtu wa kumuachia mtoto wangu, mama yangu alikuwa na shughuli nyingi kwa hivyo hangeweza kunisaidia.”

Mtoto akiwa katika kituo cha malezi ya watoto wachanga Ngong nchini Kenya kilichofunguliwa ili kuwezesha mama zao kurudi shule.
UN News
Mtoto akiwa katika kituo cha malezi ya watoto wachanga Ngong nchini Kenya kilichofunguliwa ili kuwezesha mama zao kurudi shule.

Msichana huyu ni mkazi wa eneo la Ngong iliyoko katika kaunti ya Kajiado nchini Kenya, Nairobi. Changamoto yake inakabili wasichana wengi, jambo lililochochochea mashirika ya kiraia kubonga bongo na hatimaye nuru ikawaangazia wasichana hao.

Jackline Saleiyan ni kiongozi wa shirika la A Pack a Month, ambaye ni mwanzilishi wa kituo cha malezi ya watoto wachanga kilichofunguliwa hivi majuzi huko Ngong, Kajiado ili kuwezesha mama zao kurudi shule au kutafuta ajira na kuendeleza biashara zao ili waweze kujimudu kimaisha. Anasema alisikitishwa kuona idadi kubwa ya wasichana vigori wanaoacha shule kwa sababu ya changamoto za kijamii… 

“Tulilazimika kuanzisha mradi huu kwa sababu katika eneo la Bunge la Kajido Kaskazini pekee, kati ya wasichana 1500 waliopata Watoto wakiwa wadogo, 168 pekee ndio walipata nafasi ya kuendelea na masomo. Wasichana hao wanapitia machungu sana na dhulma za kijamii na wale ambao wangependa kurudi shule hawana uwezo wa kumudu malezi ya watoto wao. Kupitia mradi huu watweza kuleta Watoto wao asubuhi katika kituo hiki cha malezi ya watoto wachanga na kuenda shule, na jioni watakuja kuchukua Watoto wao.”

Jackline Saleiyan, Kiongozi wa shirika la A Pack a Month, ambaye ni mwanzilishi wa kituo cha malezi ya watoto Ngong nchini Kenya.
UN News
Jackline Saleiyan, Kiongozi wa shirika la A Pack a Month, ambaye ni mwanzilishi wa kituo cha malezi ya watoto Ngong nchini Kenya.

Hatua hii ilikuwa ni nuru kwa Neema ambaye anaeleza ni kwa jinsi gani alipata habari hizi njema za kurejesha matumaini..

“Wakati mmoja nikiwa katika ukumbi wa kijamii, nilikutana na Jackline Saleiyan nikiwa nimeenda kupokea mfuko wa msaada wa kiutu ukiwemo padi za kutumia wakati wa hedhi. Alinieleza kuwa kuna kikundi cha wasichana amabo huwa wanakutana kujadili changamoto zao na akanialika nijiunge nao. Hapo ndo nikapata usaidizi, mosi ya afya yangu ya akili na pia kugundua kwamba sisi tuaweakupata usaidizi Zaidi tukijitolea kurudi shule au kutafuta njia zingine Chanya za kujikwamua kiuchumi.”

Serikali ya Kenya haikukosa mwakilishi katika hafla hii, ikiwakilishwa na Mule Komora Kamishna Msaidizi wa Kaunti ya Kajiado, anasema kwa pamoja watahakikisha watoto wanaozaliwa wamepata haki zao za malezi bora, na mama zao wapate fursa ya kuendelea na masomo yao.

“Tuko hapa kufungua kituo cha Watoto wachanga wenye umri wa miezi 6 hadi miaka 5 ambao watapata malezi bora wakisubiri kuanza shule. Pia Wazazi wao wapate fursa ya kurudi shule. Wito wangu kubwa ni kuomba wasichana wajilinde, waondokane na vishawishi na kutazama Maisha yao ya baadaye. Kosa la kwanza iwe ni bahati mbayá lakini  kurudia kosa ni makosa.”

Mbiriri Mwaura ni Mwakilishi wa serikali ya Kaunti ya Kajiado eneo la Ngong, MCA,  anatoa wito kwa jamii hasa vijana akifafanua kwamba kuteleza sio kuanguka, na kwamba serikali itasimama na wasichana waathirika ili kuhakikisha wametimiza ndoto zao.

“Mradi huu unadhihirisha kwamba tunasimama na wasichana wetu, na kwa vijana wa kiume na wanaume wote, naomba tuachane na wasichana wetu waendelee na masomo, tuondokane na dhulma kwa wasichana. Mimi kama kiongozi nitahakikisha tumefanya kila tuwezalo kuhakikisha wasichana wetu walioacha shule kwa sababu ya mimba za utotoni wamerudi shule, nimeongea na waanzilishi wa kituo hiki na nitarudi kwa serikali kuhakikisha sera za kuwekeza kwa wasichana wetu na Watoto wao zitajumuishwa katika sera za serikali na tutaendelea kuunga mkono miradi yote.”

Picha ya pamoja ya wasichana, watoto, viongozi wa serikali na familia zao wakati wa hafla ya ufunguzi wa Daycare.
UN News
Picha ya pamoja ya wasichana, watoto, viongozi wa serikali na familia zao wakati wa hafla ya ufunguzi wa Daycare.

Ama kweli mradi huu umeleta manufaa kwa wasichana waathirika na watoto wao, wengine wameweza kurudi shule, na sasa Neema anaongeza kuwa hajafa moyo kwani licha ya kutoweza kurudi shule kwa wakati muafaka, mradi huu umemuwezesha kujimudu kimaisha.

“Sasa hivi tuko na daycare ya watoto, unamleta hapa asubuhi na kumuacha na kuenda kazini. Mtoto anapata chakula kizuri chenye virutubisho anacheza na watoto wenzake, na mimi naaondoka kutafuta kibarua. Kwa vile hatulipi chochote hela ninazopata inanisaidia kujmudu kimaisha, kitambo nilikuwa napata shilingi za Kenya mia 2, nalipa daycare mia 1 nabaki na pesa ambazo hazikuwa zinatosha kikidhi mahitaji yetu.”

Samwel Muchiri, Msimamizi wa kata ya Olkeri iliyoko katika kaunti ya Kajiado anatamatisha kwa kutoa shukrani na ujumbe wa matumaini..

“Kwanza kabisa ninawashukuru wote kwa mshikamano wenu na uwekezaji katika mradi huu.  Ni faida kwetu wote, lakini hasa kwa watoto wachanga ambao hawana hatia, na wasichana wetu. Na cha muhimu zaidi ni Kwamba bado kuna matumaini kwa wasichana wetu, bado unaweza kutimiza ndoto zako, unaweza kuwa mtu yeyote muhimu kwa jamii siku za usoni, bado kuna matumaini.”