Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukosefu wa huduma salama za choo unaathiri watoto zaidi - Wakazi Ngong

Utoaji wa huduma safi na salama za kujisafi nchini Kenya kupitia huduma ya vyoo ambavyo wananchi wanaweza kumudu gharama yake.
UNICEF VIDEO
Utoaji wa huduma safi na salama za kujisafi nchini Kenya kupitia huduma ya vyoo ambavyo wananchi wanaweza kumudu gharama yake.

Ukosefu wa huduma salama za choo unaathiri watoto zaidi - Wakazi Ngong

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Wakati hapo jana Novemba 19 dunia imeadhimisha Siku ya choo Duniani. Maudhui yaliyobeba siku hiyo ni ‘Kuongeza kasi ya mabadiliko’. Kampeni hii inazingatia athari za janga la usafi wa mazingira ambalo huwa chanzo cha magonjwa mengi hasa ya kuambukiza. Kwa mujibu wa takwimu za shirika la afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO watu bilioni 3.6 karibu nusu ya watu wote duniani hawana huduma za msingi za usafi na milioni 494 miongoni mwao wanajisaidia haja kubwa katika maeneo ya wazi kwa kukosa huduma ya choo wengi wakiwa ni kutoka katika nchi masikini.  Wakazi wa eneo la Ngong katika kaunti ya Kajiado nchini Kenya wameeleza changamoto zao za upatikanaji wa choo safi na salama.

Eneo hili la Ngong lina mitaa kadhaa ya mabanda ambayo hukumbwa na changamoto kubwa ya kukosekana kwa hudumza muhimu za vyoo. Obadia ni miongoni mwa wakazi anasema changamoto yao kubwa ni utunzaji wa vyoo, “Choo zetu huwa safi, saa zingine sio safi, kwa sababu tunatumia watu wengi”.

Kutokuwepo kwa huduma ya vyoo vya umma imeongezeza changamoto kama asemavyo mkazi mwingine George Wawezi, “Choo hakuna za public, kila mtu anajitengenezea, ukarabati wewe mwenyewe unajishughulikia”.

Jane Waweru ni mmoja wa wale wanaohakikisha hata kama huduma si bora sana lakini inatunzwa,

“Kila mtu akienda, anaenda na maji na anaosha, kwa hivyo hakuna ugonjwa”.

Kwa Mike kuendelea kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa choo ni muhimu sana na hasa kwa afya zao, “Hata sisi tungependa kufurahia hiyo siku ya kusherekea kwa vyoo, kwa vile kuna magonjwa choo isipongarishwa”.

Esther Makori ni mchuuzi wa mboga, anasema mtihani mkubwa ni pale ambapo choo kinakuwa cha jumuiya, “Choo hapa kwetu sisemi kuna usafi sana, kuna wale niwachafu kiasi na kuna wale wasafi, sana sana kama kwa Estates, wanazingatia usafi lakini kwa vijiji hawazingatii. Choo chafu huleta magonjwa kama kuhara kwa sababu watoto wakienda kwa hiyo choo na wasinawe mikono vizuri, lazima wapate ugonjwa wa kuhara, na sio nzuri kwa afya kwa sababu inadhuru afya ya watu. Usafi wa choo hufanya mazingira iwe nzuri, hata hakuwezi kuwa na uchafu. Unajua choo ikiwa chafu, huo mji unakuwa chafu wote. Sasa tuseme customer amekuja kwa biashara yangu, unajua choo ni aja, akiniuliza mahali pakujisaidia, apate choo yangu in chafu, hatarudi kwa kazi yangu. Choo ni kitu muhimu sana, kwa kila mtu sio mimi peke yangu”.

Kwa watoto hatari ya kukosa huduma ya choo inakuwa kubwa zaidi, Alvine ni mama mwenye mtoto mdogo, “Mahali tunaishi hakuna choo, na kama hakuna choo, kuishi bila choo mbaya sana kwa sababu mtoto anaweza athiriwa na uchafu, magonjwa, magonjwa ya kutokuwa na choo na hayo magonjwa yanaweza zambaa mahali kwingi sana. Ni vizuri kama mnaweza mtusaidie, na wale wanaishi mahali hakuna choo, wanaweza jua vile watakaa ndio waweze kuishi vizuri, watoto wao wasigonjeke. Kama saa hii kuna hiyo mvua ya El Nino, mavi inakuwa juu nyingi, uchafu ni nyingi, kwa hivyo tungeomba kama inawezekana mueze kusaidiana kwa wale hawana choo, tusaidiane sisi sote na, serikali tunaomba msaada kutoka kwenu mtusaidie”.  

Dkt. Hellen Nyangweso ni daktari katika kituo cha afya cha Rules anasema watoto wengi huathirika sana kutoka na na uchafu, “Mara kadhaa tunapokea watoto ambao wana ugonjwa wa kuhara kwa sababu ya kuishi ama kula vyakula ama kunyua maji ambayo sio safi. Kwa hivyo mara nyingi tumeweza kutibu wagongwa wa aina hiyo. Mara nyingi huwa wanasema wana ukosefu wa maji safi, ya kupika hata ya kunyua, na pia unapata kuna ukosefu wa choo mahali pale. Labda watu wengi wanatumia choo kimoja, kinakuwa kichafu na hakuna maji ya kukiosha. Kama Ruels, tukipatana na hali kama hiyo huwa tunawaongelesha kuhusu usafi wa kuosha mikono, kunyua maji safi, na kuhakikisha wanaishi katika mazingira safi, na pia kuambia umuhimu wa kuosha vyoo vyao, na pia wahakikishe wanatumia vyoo, ule uchafu wa choo uendi kwenye mazingira. Saa zingine tunakuwa na health talk, na wagonjwa hapa, tunawaambia kuhusu waste education, wanajua hii waste haifai kutupua kwa Barabara, inafaa iwekwe mahali penye itachukuliwa. Siku ya Choo Duniani ni siku ya maana sana, kwa maana choo ni afya njema. Kwenye vijiji, tuweze kusaidia tuone kama changamoto ya choo inaweza tatuliwa namna gani. Siku ya choo ni siku ya maana sana na ningepmba sisi sote tungezingatia.

Na hii ndio maana WHO inayahimiza mataifa yote kuhakikisha huduma ya choo inakuwa ni haki ya msingi kwa kila mtu sio tu kwa kuokoa Maisha bali pia kuhakikisha malengo ya maendeleo ya afya yanatimia ifikapo 2030.