Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Marufuku mpya ya Israeli kwa misaada ya UNRWA Gaza ni hatua mbaya: McGoldrick

Mtto wa kike akiwa amesimama nje ya makazi ya wakimbizi katika mji wa Rafah
© UNICEF/Eyad El Baba
Mtto wa kike akiwa amesimama nje ya makazi ya wakimbizi katika mji wa Rafah

Marufuku mpya ya Israeli kwa misaada ya UNRWA Gaza ni hatua mbaya: McGoldrick

Amani na Usalama

Vikwazo vinavyoendelea vya Israel na marufuku yake mpya ya kuwasilisha misaada kwa shirika kubwa la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalstina UNRWA huko Gaza tayari vina athari kubwa, amesema mratibu wa muda wa Umoja wa Mataifa katika eneo linalokaliwa la Palestina.

Akizungumza katika mahojiano maalum na UN News mratibu huyo Jamie McGoldrick amesema hii ni changamoto kubwa ukizingatoa hali halisi

“Nadhani ripoti ya IPC iliyotoka wiki iliyopita ilionyesha wazi kabisa kuzorota kwa hali na viwango vya utapiamlo hasa katika maeneo ya kaskazini. Na, tumeona kupungua kwa asilimia 70 kwa uwezo wa watu kujikimu. Ukatizaji wowote wa usambazaji wa chakula ambao tayari ni dhaifu sana ni hatua mbaya. Na, tumekuwa na mazungumzo na Israeli ili kuona kama kuna uwezekano wowote tunaweza kupata tena njia ya kupita katika hili na kuona endapo tunaweza kupata malori tunayohitaji kila siku kuingia Gaza. Hivi sasa, hali ni ya hatari sana na sio ya kuaminika. Na inakuwa ni bahati ya kuweza kupata malori 10-15, katika wakati wowote kwa muda wa siku mbili.”

Ameendelea kusema kwamba kuna changamoto kubwa iliyopo baina ya UNRWA na Israel ambayo inahitaji kupatiwa ufumbuzi kwani amesema kwa Wapalestina zaidi ya milioni 1 Gaza hali ni tete na ya kukatisha tamaa. 

“Watu wanaishi kwa chakula cha kidogo sana na mkate kwa sehemu kubwa, na hiyo ni sawa kwa hali ya dharura. Lakini ikiwa ni miezi sita, na unaishi mahali ambapo ni pachafu na kuna huduma duni za maji na usafi , maji kidogo sana kwa kila mtu, karibu lita moja kwa siku na kisha unaishi katika makazi ambayo yamefurika watu pomoni, ndio maana matokeo yake ni changamoto za kiafya zinazoanza kuibuka, yakiwemo maambukizi ya magonjwa ya tumbo, maambukizi ya bakteria, homa ya ini, magonjwa ya kuhara, na magonjwa ya kupumua.”

MacGodrick ametaka hatua za haraka na za maksudi zichukuliwe ili kuwanusuru Wapalestina ambao hivi sasa wako katika harati kubwa ya kuangamia.