Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katika mkutano wa amani Cairo Guterres asisitiza haja ya misaada endelevu Gaza

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akiwa katika mkutano wa amani mjini Cairo Misri
UN Photo/Eskinder Debebe
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akiwa katika mkutano wa amani mjini Cairo Misri

Katika mkutano wa amani Cairo Guterres asisitiza haja ya misaada endelevu Gaza

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres leo amesisitiza wito wake wa msaada endelevu wa kibinadamu kuwasilishwa Gaza katika hotuba yake kwenye mkutano wa amani wa Cairo Misri.

Rais wa Misri Abdel Fattah El-Sisi amewaita viongozi kutoka eneo hilo na duniani kote katika juhudi za kupunguza uhasama kufuatia uvamizi wa Hamas nchini Israel tarehe 7 Oktoba, na Israel kulipua Gaza na kuzingira kabisa eneo hilo.

Mkutano huo umefanyika siku moja baada ya mkuu wa Umoja wa Mataifa kusafiri hadi kwenye kivuko cha mpaka cha Rafah kaskazini mwa Sinai nchini Misri, ambacho ni kivuko pekee cha mpaka na Gaza kilicho wazi.

"Hapo niliona kitendawili  janga la kibinadamu likitokea kwa wakati halisi nikilishuhudia," amesema Katibu mkuu.

Bwana Guterres amebainisha kuwa mamia ya malori "yaliyojaa chakula na vifaa vingine muhimu yalikuwa upande wa Misri wakati ikivuka mpaka, watu milioni mbili huko Gaza walikuwa wakikosa maji, chakula, mafuta, umeme na dawa.

Leo Jumamosi, msafara wa kwanza uliobeba vitu vilivyohitajika sana ulivuka hadi Gaza.

Malori yaliyobeba misaada ya kibinadamu yakisubiri kuingia Gaza kutoka Misri
UN Photo/Eskinder Debebe
Malori yaliyobeba misaada ya kibinadamu yakisubiri kuingia Gaza kutoka Misri

UN inafanya kazi bila kukoma

"Malori hayo yanahitaji kusafiri haraka iwezekanavyo kwa kiwango kikubwa, endelevu na salama kutoka Misri hadi Gaza," alisema Bw. Guterres, akiongeza kuwa Umoja wa Mataifa unafanya kazi bila kukoma na pande zote kuelekea utoaji wa misaada endelevu katika kiwango ambacho kinahitajika.

Katibu Mkuu amesisitiza kuwa malengo ya muda mfupi lazima yawe wazi, akirudia wito wake wa msaada wa haraka, usio na vikwazo na endelevu wa kibinadamu kwa Gaza, kuachiliwa mara moja na bila masharti kwa mateka wote wanaoshikiliwa na Hamas, na usitishaji mapigano kwa ajili ya masuala ya kibinadamu sasa.

Amesema malalamiko ya wananchi wa Palestina ni ya halali na ya muda mrefu, lakini hakuna kinachoweza kuhalalisha shambulio la kulaaniwa la Hamas ambalo liliwatia hofu raia wa Israel. Wakati huo huo, mashambulizi haya ya kuchukiza kamwe hayawezi kuhalalisha adhabu ya pamoja kwa watu wa Palestina.