Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UDADAVUZI: Je, UN inaunga mkono vipi harakati za Haiti kukabiliana na ghasia na ukosefu wa utulivu?

Wanaume, wanawake na watoto waliotawanywa wakipata hifadhi katika ukumbi wa ndondi mjini Port-au-Prince Haiti baada ya kufurushwa makwao
© UNOCHA/Giles Clarke
Wanaume, wanawake na watoto waliotawanywa wakipata hifadhi katika ukumbi wa ndondi mjini Port-au-Prince Haiti baada ya kufurushwa makwao

UDADAVUZI: Je, UN inaunga mkono vipi harakati za Haiti kukabiliana na ghasia na ukosefu wa utulivu?

Amani na Usalama

Haiti inakabiliwa na ghasia zilizoenea za magenge ya uhalifu, taasisi za nchi hiyo ziko kwenye hatihati ya kuporomoka na raia wake wanakabiliwa na changamoto za kila siku za kuweza kuishi. Hata hivyo, katikati ya janga hili la usalama na kibinadamu, Umoja wa Mataifa unaendelea kutoa msaada muhimu kwa watu walioathirika.

1. Muktadha: uasi na hofu

Ingawa hali nchini Haiti kwa muda mrefu imekuwa na sifa ya uvunjaji sheria, huku magenge ya uhalifu yenye nguvu yakidhibiti sehemu kubwa ya mji mkuu, Port-au-Prince, miezi ya Januari na Februari 2024 imekuwa yenye vurugu zaidi katika miaka miwili iliyopita, huku zaidi ya watu 2,500 wakiuawa, kutekwa nyara au kujeruhiwa tangu mwanzo wa mwaka. Uamuzi wa Waziri Mkuu Ariel Henry, mwezi Machi 2024, kujiuzulu umefanya hali kuwa ngumu zaidi.

Mnamo tarehe 21 Machi, Ulrike Richardson, Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Haiti, alionya kwamba ghasia sasa zinaenea katika maeneo mapya ya mji mkuu, ikiwa ni pamoja na vitongoji ambavyo zamani vilikuwa na amani, kufuatia wiki za mashambulizi ya magenge ya uhalifu yaliyopangwa kwenye magereza, bandari na hospitali. 

Bi Richardson amesema ukiukwaji wa haki za binadamu umesambaa sana; unyanyasaji wa kijinsia, pamoja na matumizi ya mateso na ubakaji wa pamoja dhidi ya wanawake, umekithiri.

Moto unawaka barabarani katika eneo la Cité Soleil huko Port-au-Prince.
© UNOCHA/Giles Clarke
Moto unawaka barabarani katika eneo la Cité Soleil huko Port-au-Prince.

Afisa huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa ameelezea kuongezeka kwa mgogoro wa kibinadamu, ambapo kuna zaidi ya wakimbizi wa ndani 362,000, ukosefu wa maji safi, na kuna chini ya nusu ya vituo vya afya huko Port-au-Prince ambavyo vinavyofanya kazi katika uwezo wa kawaida.

Amesema “Njaa imefikia viwango ambavyo havijawahi kushuhudiwa, kwa mujibu wa tathmini mpya iliyotolewa tarehe 22 Machi na kuungwa mkono na Umoja wa Mataifa”. 

Kulingana na ripoti hiyo, “watu milioni 4.97 wanakabiliwa na shida au viwango vibaya zaidi vya uhaba wa chakula, ikiwa ni pamoja na watu milioni 1.64 wanaokabiliwa na viwango vya dharura".

Watu zaidi na zaidi wanajaribu kuondoka katika mji mkuu, wakihatarisha kupitia njia zinazodhibitiwa na magenge ya wahalifu. Takriban watu elfu 33 walisalia kupata hifadhi katika majimbo hayo mwezi Machi, wengi wao wakielekea Grand Sud, eneo ambalo tayari linawahifadhi zaidi ya watu 116,000 waliokimbia makazi yao.

2. Hatua za kibinadamu: kufikisha msaada ni mtihani

Tangu kuanza kwa mzozo wa hivi karibuni, ulioambatana na safu ya mashambulizi ya magenge ya uhalifu yaliyoratibiwa mwishoni mwa mwezi Februari kote Port-au-Prince, ambayo yalisababisha hali ya hatari na hatimaye kujiuzulu kwa Waziri Mkuu Henry, wafanyikazi wa Umoja wa Mataifa wameendelea kusambaza msaada kwa raia, licha ya hali ya hatari ya usalama.

Watu waliokimbia makwao kutokana na machafuko wakipata hifadhi sasa shuleni Port-au-Prince
© IOM/Antoine Lemonnier
Watu waliokimbia makwao kutokana na machafuko wakipata hifadhi sasa shuleni Port-au-Prince

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP limesambaza milo 160,000 ya chakula cha moto, wakati Shirika la Afya Duniani WHO, limesambaza vifaa muhimu vya afya, na ndege za Shirika la Umoja wa Mataifa la Huduma ya Kibinadamu UNHAS, zimesafirisha takriban kilo 800 za mifuko ya damu. .

Umoja wa Mataifa, pamoja na washirika, wamekuwa wakijaribu kushughulikia ukosefu wa maji safi, kwa mfano, kati ya Machi 16-18 UNICEF na NGO ya kimataifa ya Solidarités iliwasilisha lita 20,500 za maji kwenye maeneo manne ambayo ni makazi ya zaidi ya watu 12,000 waliofurushwa makwao, wakati kati ya tarehe 17-20 Machi shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM liliwasilisha galoni 16,000 za maji kwenye maeneo mawili.

Msaada kutoka kwa shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu na afya ya uzazi, UNFPA, na mashirika yasiyo ya kiserikali washirika, unatolewa kwa waathiriwa wa unyanyasaji wa kijinsia, kwa njia ya simu ya dharura inayotoa usaidizi wa kisaikolojia, na kliniki ya simu ya afya ya ngono na uzazi/ukatili wa kijinsia na unyanyasaji katika moja ya makazi ya wakimbizi wa ndani. 

3. Hatua za kimataifa

Kutafuta njia ya kumaliza mgogoro wa Haiti imekuwa mada ya mikutano kadhaa ya ngazi ya juu ya Umoja wa Mataifa. Mnamo tarehe 21 Machi Baraza la Usalama, chombo cha Umoja wa Mataifa kinachohusika na kudumisha amani na usalama wa kimataifa, lilitoa taarifa kwa vyombo vya habari na kusisitiza wanachama wake kuunga mkono "mchakato wa kisiasa unaoongozwa na Haiti, na kusisitiza haja ya jumuiya ya kimataifa kuongeza maradufu juhudi zake za kutoa msaada wa kibinadamu kwa watu walioathirika na kusaidia polisi wa kitaifa wa Haiti.” Wajumbe wa Baraza la Usalama pia walielezea wasiwasi wao mkubwa juu ya uingwazi haramu wa silaha na risasi nchini Haiti ambavyo bado, walisema, ni sababu ya msingi ya ukosefu wa utulivu na ghasia.

Baraza la Usalama likipitisha azimio kuruhusu kuanzishwa kwa ujumbe wa msaada wa ulinzi wa vikosi vya kimataifa MSS nchini Haiti Oktoba 2023
UN Photo/Paulo Filgueiras
Baraza la Usalama likipitisha azimio kuruhusu kuanzishwa kwa ujumbe wa msaada wa ulinzi wa vikosi vya kimataifa MSS nchini Haiti Oktoba 2023

Mwezi Oktoba 2023, Baraza la Usalama liliidhinisha kutumwa kwa Ujumbe wa Kimataifa wa Usaidizi wa Usalama (MSS) nchini Haiti, kwa ombi la serikali ya wakati huo. Azimio hilo lilipongezwa wakati huo kama la kwanza la kihistoria, ingawa misheni hiyo bado haijatumwa.

4. Ufadhili: Pengo kubwa la kuziba

Wakati huo huo, maafisa kadhaa wakuu kutoka kwa mfumo wa Umoja wa Mataifa wanaendelea kutoa wito wa kuimarishwa kwa ufadhili kwa juhudi za kibinadamu.

Siku ya Alhamisi, Bi. Richardson alibainisha kuwa mpango wa kukabiliana na misaada ya kibinadamu kwa Haiti, ambao unahitaji dola milioni 674, umefadhiliwa kwa asilimia sita pekee. "Muda unaenda," alisema.

Mapema mwezi Machi Cindy McCain, mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP, alionya kwamba juhudi za msaada "zimekwaa kisiki".

Wanawake na watoto wao wakisubiri katika kliniki inayosaidiwa na UNICEF Port-au-Prince, Haiti (Kutoka Maktaba)
© UNICEF/Odelyn Joseph
Wanawake na watoto wao wakisubiri katika kliniki inayosaidiwa na UNICEF Port-au-Prince, Haiti (Kutoka Maktaba)

10-11-2022-UNICEF-Haiti-cholera-01

5. Mustakbali uko njiapanda

Ujumbe wa MSS wa kuimarisha polisi wa kitaifa wa Haiti walio na vitendea kazi duni unatarajiwa kuongozwa na Kenya, huku wanajeshi pia wakiahidiwa na nchi kadhaa za Caribbea. Marekani imeahidi kutoa dola milioni 300, kulingana na duru za vyombo vya habari.

Ingawa huu si ujumbe wa Umoja wa Mataifa, umeidhinishwa na Azimio la Baraza la Usalama.

Hata hivyo, ijapokuwa kuna makubaliano mengi kwamba Haiti inahitaji msaada wa haraka ili kuleta mazingira salama na tulivu, ujumbe huo ulivurugwa na kujiuzulu kwa Bwana. Henry, jambo ambalo liliifanya Kenya kutangaza kwamba inachelewesha kutumwa kwa vikosi vyake, hadi itakapotangazwa serikali mpya ya Haiti.

Kulingana na ripoti za vyombo vya habari, makundi ya kisiasa yanakaribia kuafikiana kuhusu baraza la mpito ambalo litachukua mamlaka ya urais hadi uchaguzi ufanyike. Haijulikani endapo na lini baraza hilo litachukua mamlaka, au ni lini ujumbe wa usalama utaanza kufanya kazi katika ardhi ya Haiti.