Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chonde chonde msiwarejeshe nyumbani wakimbizi na waomba hifadhi wa Haiti: UNHCR

Kundi la watu waliopoteza makazi katika shule katikati ya Port-au-Prince, katika tovuti ya Jean-Marie Vincent.
© IOM/Antoine Lemonnier
Kundi la watu waliopoteza makazi katika shule katikati ya Port-au-Prince, katika tovuti ya Jean-Marie Vincent.

Chonde chonde msiwarejeshe nyumbani wakimbizi na waomba hifadhi wa Haiti: UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Wakati kukiwa na kuzorota kwa kasi kwa usalama, haki za binadamu na hali ya kibinadamu nchini Haiti, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, leo limetoa mwongozo mpya wa kisheria kuhakikisha kuwa ulinzi wa kimataifa wa wakimbizi unatolewa kwa Wahaiti wanaouhitaji.

 

 

Shirika hilo limesema vurugu za kiholela za magenge nchini Haiti zimesababisha ongezeko la kutisha la ukiukwaji wa haki za binadamu na watu kukimbia makazi yao kwa kiasi kikubwa ndani ya nchi.

Takriban nusu ya watu milioni 11.4 wa nchi hiyo wanahitaji msaada wa kibinadamu limesema shirika hilo. 

Mwongozo huo mpya wa UNHCR unalenga kusaidia mataifa katika tathmini yao ya madai ya hifadhi kwa kuzingatia hali halisi inayowakabili Wahaiti leo hii.

Elizabeth Tan, Mkurugenzi wa kitengo cha ulinzi wa Kimataifa cha UNHCR amesema "Maisha, usalama na uhuru wa Wahaiti vinatishiwa na msururu wa ghasia za magenge ya uhalifu na ukiukaji wa haki za binadamu. UNHCR inayakumbusha Mataifa juu ya umuhimu wa kuhakikisha Wahaiti ambao wanaweza kuhitaji ulinzi wa wakimbizi wa kimataifa wanaupokea. Pia tunasisitiza wito wetu kwa Mataifa yote kutowarejesha watu Haiti kwa lazima, ikiwa ni pamoja na wale ambao wamekataliwa maombi yao ya hifadhi."

Zaidi ya watu 160,000 kwa sasa wamekimbia makazi yao katika eneo la mji mkuu wa Port-au-Prince nchini Haiti.
© IOM
Zaidi ya watu 160,000 kwa sasa wamekimbia makazi yao katika eneo la mji mkuu wa Port-au-Prince nchini Haiti.

Kuhusu mwongozo huo mpya

Katika mwongozo wake mpya, UNHCR inazingatia kwamba, kulingana na Mkataba wa Wakimbizi wa 1951, Wahaiti ambao wanapaswa kuhesabiwa kuwa wanastahiki ulinzi wa wakimbizi wanaweza kujumuisha wanaharakati wa kisiasa, waandishi wa habari, majaji, wanasheria na wengine wanaopigana na rushwa na uhalifu, miongoni mwa makundi mengine yaliyo katika hatari.

Zaidi ya hayo, Wahaiti wanaweza pia kustahiki ulinzi wa wakimbizi chini ya ufafanuzi wa wakimbizi wa kieneo wa Azimio la Cartagena la 1984. 

Chini ya ufafanuzi huu unaotumiwa na nchi nyingi katika eneo hili, “ulinzi wa wakimbizi unapaswa kutolewa kwa watu binafsi walioathiriwa na hali ambazo zinavuruga sana utulivu wa umma nchini na vurugu za jumla katika maeneo yaliyoathiriwa na shughuli za magenge ya uhalifu.”

Kwa mujibu wa UNHCR, nchi zinaweza pia kuzingatia kutoa ulinzi wa ziada au wa muda kwa watu kutoka Haiti, pamoja na mipango mingine ya kisheria ya kukaa, kama vile kuunganishwa kwa familia, visa vya kibinadamu na upatikanaji wa hati. 

Nchi kadhaa za Amerika tayari zinatoa njia hizi mbadala kwa Wahaiti waliofurushwa makwao, kuimarisha ulinzi wao na kuwaruhusu kujumuika katika jamii zinazowakaribisha.

Katikati ya mji wa Port-au-Prince Haiti machafuko yamesababisha kundi kubwa la watu kutawanywa
© UNICEF/Herold Joseph
Katikati ya mji wa Port-au-Prince Haiti machafuko yamesababisha kundi kubwa la watu kutawanywa

Idadi ya wakimbizi waliosajiliwa

Hadi kufikia katikati ya mwaka wa 2023, UNHCR imesema ilirekodi wakimbizi 312,000 wa Haiti na wanaotafuta hifadhi duniani kote. 

UNHCR pia imeona mwelekeo unaohusu watu wa Haiti wanaofanya safari hatari katika bara la Amerika na Caribbea, ambapo safari za baharini huzidisha hatari. 

Changamoto changamano zinazoletwa na jopo la wakimbizi na wahamiaji katika bara la Amerika zinaweza tu kushughulikiwa ipasavyo kupitia hatua za  kina na shirikishi za kikanda.

UNHCR imesema itaendelea kufanya kazi na mataifa mbalimbali ili kuhakikisha upatikanaji wa hifadhi kwa Wahaiti wanaotegemea kanuni na utekelezaji bora wa mwongozo huu.