Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Haiti: Haki za binadamu zinaendelea kuzorota ghasia za magenge zinavyosambaa

Mwanamke aliyetawanywa hivi karibuni akiwa katika shule na kituo cha michezo cha Gymnasium Vincent Port-au-Prince.
© UNOCHA/Giles Clark
Mwanamke aliyetawanywa hivi karibuni akiwa katika shule na kituo cha michezo cha Gymnasium Vincent Port-au-Prince.

Haiti: Haki za binadamu zinaendelea kuzorota ghasia za magenge zinavyosambaa

Haki za binadamu

Hali ambayo tayari ni mbaya ya haki za binadamu nchini Haiti imezorota zaidi huku kukiwa na ongezeko la ghasia za magenge, ameonya leo Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu Volker Türk.

UTakriban watu 806 ambao hawakuhusika katika vita vikali vya magenge waliuawa, kujeruhiwa, au kutekwa nyara mwezi Januari, mwezi ambao uliokuwa na umwagaji damu zaidi nchini humo katika zaidi ya miaka miwili.

Zaidi ya hayo, Türk amesema baadhi ya washiriki wa magenge 300 waliuawa au kujeruhiwa, na kufanya jumla ya watu walioathirika kufikia 1,108 ikiwa ni zaidi ya mara tatu ya idadi iliyorekodiwa Januari 2023 na kila siku huleta majeruhi zaidi.

Kupelekwa vikosi vya kimataifa

"Sasa, zaidi ya wakati mwingine wowote, maisha ya Wahaiti yanategemea kutumwa, bila kucheleweshwa zaidi, kwa operesheni ya msaada wa usalama wa kimataifa huko Haiti MSS, kusaidia Polisi wa kitaifa na kuleta usalama kwa watu wa Haiti, chini ya masharti ambayo yanazingatia kimataifa kanuni na viwango vya haki za binadamu,” amesema mkuu huyo wa haki za binadamu, akimaanisha ujumbe ulioidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Oktoba mwaka jana.

Washiriki wa genge wanaendelea kugombania udhibiti wa eneo katika mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince, na wamezidisha shughuli zao katika maeneo ya nje ya jiji.

Kukithiri kwa mapigano hayo yanayodumu kwa saa kadhaa katika baadhi ya matukio kunaweza kuashiria kuwa baadhi ya magenge yamepokea silaha mpya hivi karibuni, kwa mujibu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu OHCHR.

Familia ya watu waliohamishwa makazi yao huko Tabarre, Haiti wakusanyika kwenye tovuti.
© UNICEF/Ndiaga Seck
Familia ya watu waliohamishwa makazi yao huko Tabarre, Haiti wakusanyika kwenye tovuti.

Ukatili wa kijinsia kama silaha

Ofisi ya haki za binadamu imesema magenge pia yanaendelea kutumia ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana kama silaha, na kueneza hofu kwa kutumia mitandao ya kijamii kushiriki picha na video za kutisha za watu waliouawa na wanawake kubakwa.

Kuongezeka na kuenea kwa ukosefu wa usalama ambavyo Bwana Türk ameelezea kama mfumo wa machafuko kumesababisha maandamano mitaani dhidi ya serikali na machafuko ya wenyewe kwa wenyewe, yanayoungwa mkono na vyama vya upinzani vya kisiasa, katika angalau miji 24.

Takriban watu 16 waliuawa na 29 kujeruhiwa katika wiki za hivi karibuni, haswa katika muktadha wa mapigano kati ya waandamanaji na polisi.

Hofu kwa watoto

Mkuu huyo wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa pia ameonyesha wasiwasi wake juu ya hali ya watoto, akibainisha kuwa wavulana na wasichana 167 waliuawa na kujeruhiwa kwa risasi mwaka jana.

Baadhi yao waliuawa na magenge au vile vilivyoitwa vikundi vya "kujilinda" kwa msaada wao unaoshukiwa kwa wapinzani, wakati uandikishaji wa watoto katika magenge ulisalia kuwa wa kutisha sana.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF limetoa wito kwa pande zote kuwalinda raia wa Haiti wenye umri mdogo zaidi kutokana na machafuko ya hivi karibuni.

“Watoto na familia tayari wanavumilia mawimbi ya unyanyasaji wa kikatili unaofanywa na vikundi vyenye silaha katika vitongoji vyao, huku kila siku ikileta mambo ya kutisha, kufiwa na wapendwa wao, nyumba kuharibiwa na moto au risasi, na hali ya hofu inayoendelea kila wakati. ”  amesema jana Bruno Maes, Mwakilishi wa UNICEF nchini Haiti, 

Amebainisha kuwa “Raia wa Haiti wanakabiliwa na ukiukwaji mbaya zaidi wa haki za binadamu na vitisho katika historia ya hivi karibuni ya nchi hiyo.” alibainisha.

Les Cayes, jiji dogo ulio kusini mwa Haiti.
© UNICEF/Roger LeMoyne
Les Cayes, jiji dogo ulio kusini mwa Haiti.

Komesheni vurugu

Miaka mingi ya machafuko ya kisiasa, umaskini, matatizo ya kitaasisi na kijamii na kiuchumi, milipuko ya magonjwa, ongezeko la viwango vya utapiamlo, majanga na kuongezeka kwa ghasia za kutumia silaha kumesababisha zaidi ya watoto milioni tatu kuhitaji msaada wa kibinadamu Haiti, na wengine wengi watajiunga nao ikiwa hali itazidi kuzorota umeonya Umoja wa Mataifa.

Kwa vile machafuko hayo tayari yamesababisha kukatika kwa huduma muhimu za kijamii kama vile elimu, afya na ulinzi, afisa wa UNICEF amewataka wadau wote, ikiwa ni pamoja na mamlaka katika ngazi zote, "kukomesha ghasia na kuzingatia kufungua tena kwa usalama na kutoa huduma muhimu za kijamii. kwa watoto ambapo hapo awali hazikuwa na kazi.”