Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunawaangusha wakimbizi wa Syria na jamii zinazowahifadhi yaonya UNHCR/UNDP

Kijana mkimbizi wa Syria nchini Jordan anasoma katika kituo kinachofadhiliwa na UNICEF.
© UNICEF/Christopher Herwig
Kijana mkimbizi wa Syria nchini Jordan anasoma katika kituo kinachofadhiliwa na UNICEF.

Tunawaangusha wakimbizi wa Syria na jamii zinazowahifadhi yaonya UNHCR/UNDP

Msaada wa Kibinadamu

Wakati mzozo wa Syria ukiingia katika mwaka wake wa 14, eneo hilo linakabiliwa na hali ya kutisha ambapo mahitaji ya wakimbizi wa Syria na jamii zinazowahifadhi yanaongezeka huku ufadhili wa kuwasaidia wakimbizi hao ukiendelea kupungua umeonya leo Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa haya yanajiri katika wakati mgumu sana na tete katika eneo hilo.

Kulingana na taarifa ya Mkakati wa Kikanda wa 2024 kwa ajili ya mnepo wa 3RP,  jukwaa kuu la kikanda la kusaidia wakimbizi wa Syria na jamii zinazowapokea, mahitaji ya dharura ya zaidi ya wakimbizi milioni 6.1 wa Syria na wanajamii milioni 6.8 wanaowapokea yanazidi kuongezeka bila kufikiwa.

Mwaka 2024, washirika wa 3RP wanakadiria kuwa dola bilioni 4.9 zinahitajika ili kukidhi mahitaji ya kipaumbele ya watu walio katika mazingira magumu na taasisi zilizoathiriwa na mzozo wa Syria huko Uturuki, Lebanon, Jordan, Misri na Iraqi. Uwezo wa mamlaka za kitaifa na za mitaa katika nchi hizi kukabili mahitaji yanayoongezeka unapungua sana huku zikikabiliwa na changamoto zinazoongezeka za mfumuko wa bei, bei ya juu ya vyakula na mafuta, kushuka kwa thamani ya sarafu na ukosefu mkubwa wa ajira, haswa miongoni mwa wanawake na vijana. 

Hii inazidishwa na athari mbaya za vita ya Gaza na kuongezeka kwa shinikizo la mabadiliko ya tabianchi.

Changamoto ya ufadhili

Mwenendo unaendelea wa changamoto ya ufadhili kwa wakati unatisha,umesema Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa 3RP imetoka kutoka kwa ufadhiliwa zaidi ya asilimia 60 kwa wastani  kati ya mwaka 2015-2018 hadi asilimia 40 tu iliyofadhiliwa kwa wastani kati ya  2020-2022. 

Mwaka jana, Umoja wa Mataifa unasema ni asilimia 30 tu ya fedha zinazohitajika zilipokelewa. 

Kupungua kwa viwango vya ufadhili wa kimataifa kwa usaidizi wa kibinadamu na maendeleo kunamaanisha kuwa watu wengi wanaachwa kuliko wale wanaoungwa mkono.

Ayman Gharaibeh, Mkurugenzi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR wa Kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini  amesema “Zaidi ya miaka kumi na tatu na bila ufumbuzi wowote wa kisiasa kuhusu mzozo wa Syria, wakimbizi kutoka Syria wanaendelea kuhitaji ulinzi wa kimataifa na hifadhi huku ufadhili ukipungua, mamilioni ya wakimbizi na wenyeji wao wanazidi kutumbukia katika umaskini na wanakabiliwa na hatari nyingi za ulinzi. Jumuiya ya kimataifa inahitaji kusalia katika mkondo huo kwa kutoa kiwango kinachohitajika cha msaada na suluhu kwa walio hatarini zaidi. Ni lazima tuepuke hali ya kukata tamaa inayotawala.”

Hali Jordan na Uturuki

Nchini Jordan, ufadhili uliopunguzwa unahatarisha huduma kwa walio hatarini zaidi, hasa kaya zinazoongozwa na wanawake na watu wenye mahitaji maalum, kuhatarisha kuzorota zaidi kwa hali ya maisha na kuongezeka kwa mivutano kati ya wakimbizi na jamii zinazowapokea. 

Umoja wa Mataifa unasema Uturuki nayo inakabiliana na changamoto zinazoongezeka kutokana na matetemeko ya ardhi ya mwaka jana na shinikizo la kifedha. 

Ufadhili duni umewaacha watoto na vijana wakimbizi 450,000 bila elimu. Mapungufu ya kiafya, haswa katika chanjo, pia yanaleta vitisho kwa wakimbizi, wakati kaya 346,000 zilizo hatarini zitapoteza msaada wa chakula.

Mkakati wa 3RP unasalia kuwa njia muhimu ya kuratibu na kuwasilisha misaada ya kibinadamu na msaada wa maendeleo. 

Katika mwaka huu wa 2024, washirika wanaendelea kutoa wito wa kuimarishwa kwa juhudi za serikali katika nchi hizo tano zinazoandaa na kupanua mifumo ya utoaji huduma kwa umma ili kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya watu walioathirika kwa huduma bora za msingi, ikiwa ni pamoja na afya, elimu, ulinzi wa kijamii, usafi wa mazingira na udhibiti wa taka na kupanua wigo wa fursa za kiuchumi.

Kazi yetu ni kuokoa maisha na kuleta matumaini

Katibu Mkuu Msaidizi na mkurugenzi wa ofisi ya Kanda ya mataifa ya Kiaranu wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo UNDP Dkt. Abdallah Al Dardari, Mkurugenzi wa Mkoa wa Mkoa wa Mkoa. Ofisi ya Mataifa ya Kiarabu katika UNDP amesema "Lengo letu sio kuokoa maisha tu, lakini wakati mgogoro unaendelea, lazima pia tusaidie watu kudumisha hisia zao za kujitolea na matumaini ya maisha bora ya baadaye. Kazi yetu lazima isaidie kuhakikisha kwamba taasisi za kitaifa na za mitaa zinazohusika na utoaji wa huduma za msingi zinabaki kuwa thabiti zenye uwezo wa kukabiliana na mahitaji yanayoongezeka na kukabiliana na mazingira ya uendeshaji yanayobadilika haraka kwamba jamii haziteseki na kuongezeka kwa mivutano ya kijamii kutokana na ushindani wa rasilimali na kwamba kaya ziendelee kuwa na tija na kuweza kujitegemea.”

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa katika miezi tisa ya kwanza ya 2023 pekee, na licha ya uhaba wa fedha, juhudi za pamoja za washirika wa 3RP zilisasaidia utoaji wa huduma za ulinzi kwa watu milioni 5.4, msaada wa chakula na fedha kwa takriban watu 566,000, pia ulisaidia watu 13,000 kupata ajira na kuanzisha biashara, na kutoa mafunzo kwa zaidi ya wafanyakazi 17,500 wa taasisi za umma za kitaifa.