Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wafurahi kupata vibali vya kazi Jordan

Kamishna Mkuu wa UNHCR atembelea wakimbizi wa Syria katika ofisi ya ajira kambini Za'atari
UNHCR/Claire Thomas
Kamishna Mkuu wa UNHCR atembelea wakimbizi wa Syria katika ofisi ya ajira kambini Za'atari

Wakimbizi wafurahi kupata vibali vya kazi Jordan

Amani na Usalama

Maisha ya wakimbizi wa Syria nchini Jordan yanaanza kupata nuru baada ya serikali ya nchi hiyo kuanza kuwapatia vibali vya kufanya kazi.

Nchini Jordan, hivi sasa maisha ya maelfu ya wakimbizi yamekuwa bora ikiwemo kwa wanawake ambao ni mara ya kwanza kupata fursa ya kuajiriwa katika maisha  yao.

Miongoni mwao ni Sawsan ambaye alikimbia Syria miaka sita iliyopita na sasa ameajiriwa kwenye kiwanda cha nguo cha Jerash kinachotengeneza nguo za kampuni kubwa kama vile North Face na Lee.

(Sauti ya Sawsan- Mkimbizi kutoka Syria)

 “Sitaki kupatiwa msaada. Mtu anapaswa kuwa na utashi wa kuhangaika na kutunza familia na watoto wake. Ni kweli kufanya kazi kunachosha lakini mazingira hapa ni mazuri na tunafurahia.”

Kiwanda cha Jerash kimeajiri wanawake 20 ambao ni wakimbizi wa Syria wakipatiwa ujira wa dola 260 kwa mwezi.

Wafanyakazi wanapatiwa usafiri wa kwenda kiwandani na kurejea nyumbani pamoja na mlo na huduma ya malezi kwa watoto ambao wazazi wao wanafanya kazi kiwandani hapo.

UNHCR ilianzisha kituo cha kwanza kabisa cha aina yake kwenye kambi ya Za’atari ili kusaidia wakimbizi kupata ajira kulingana na stadi walizo nazo, pamoja na kuwapatia mafunzo.

Tangu mwaka jana, serikali ya Jordan imetoa zaidi ya vibali 88,000 kwa wakimbizi wa Syria wanaoishi Jordan, ambapo asilimia 43 wameajiriwa kwenye sekta ya kilimo, asilimia 19 sekta ya ujenzi na asilimia 13 uzalishaji. Asilimia 5 kati yao wote ni wanawake.