Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Biashara ndogo ndogo yakwamua wanawake na vijana kiuchumi Kajiado nchini Kenya

Lucy Oduor (kushoto) na Irene Wambui (kulia) wakiwa katika eneo lao la biashara huko Ngong lililo katika kaunti ya Kajiado nchini Kenya.
UN News
Lucy Oduor (kushoto) na Irene Wambui (kulia) wakiwa katika eneo lao la biashara huko Ngong lililo katika kaunti ya Kajiado nchini Kenya.

Biashara ndogo ndogo yakwamua wanawake na vijana kiuchumi Kajiado nchini Kenya

Wanawake

Wiki hii Ijumaa tarehe 8 Machi 2024, ulimwengu utaadhimisha Siku ya Wanawake Duniani ambapo mwaka huu ina maudhui “Wekeza kwa wanawake: Harakisha maendeleo,” lakini Shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya wanawake, UN Women linasema ni dhahiri kwamba ulimwengu bado unakabiliwa na migogoro mingi, kuanzia mizozo ya kijiografia hadi viwango vya umaskini vinavyoongezeka, ukosefu wa usawa na kuongezeka kwa athari za mabadiliko ya tabianchi. 

Wanawake kote ulimwenguni ni waathirika wakubwa wa changamoto hizi na hivyo kuongeza changamoto zinazozikabili jamii zao, hususani watoto na vijana. Changamoto hizi zinaweza tu kutatuliwa kwa kubuni suluhu zinazowawezesha wanawake. 

Kwa kuwekeza kwa wanawake, tunaweza kuibua mabadiliko na kuharakisha mpito kuelekea dunia yenye afya, usalama na usawa zaidi kwa wote. Nchini Kenya tunakutana na mama mjasiriamali ambaye alianza kwa kufanya kazi na shirika lisilo la kiserikali liitwalo Sime Food, ambalo linahusika na kilimo endelevu, lishe bora, na stadi za biashara ndogo ndogo ili wawe na maarifa na ujuzi unaohitajika ili kupatia familia zao lishe bora mwaka mzima na kuuza masalio ili kusaidia kulipia mahitaji mengine ya kaya. 

Baada ya kupata mafunzo hayo na fedha za kuanzisha biashara zake, Lucy anachochea kinamama na vijana wa kike wajiunge naye katika sekta ya biashara ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Lucy Oduor, Mwanamke mjasiriamali ambaye ni mkaazi wa eneo la Ngong lililoko katika kaunti ya Kajiado nchini Kenya.
UN News
Lucy Oduor, Mwanamke mjasiriamali ambaye ni mkaazi wa eneo la Ngong lililoko katika kaunti ya Kajiado nchini Kenya.

Lucy Oduor ni mkazi wa eneo la Ngong lililoko katika kaunti ya Kajiado nchini Kenya, anaanza kwa kueleza ni kwanini aliamua kuingia katika sekta ya biashara hususan ya kuuza matunda na vinywaji vya matunda hayo.

“Nilipitia changamoto za kiafya nikiwa mama kijana. Nilikuwa nimefungua biashara ya hoteli lakini ikabidi nifunge baada ya kufanyiwa matibabu ya upasuaji. Niliposikia nafuu nikajiunga na shirika la Sime Food na hapo nikapata mafunzo kuhusu lishe bora, ndiposa nikafungua hii biashara ya vinywaji vyenye virutubisho ambavyo vimenisaidia kuwa na afya bora nikatamani watu wengine wapate kugundua umuhimu wa kuwa na lishe bora, na ndiyo maana nikaleta biashara yangu hapa mashinani.”

Kando na biashara zake Lucy pia amewapatia vijana ajira, anasema...

“Nafanya kazi na vijana wote, wa kike na wavulana kwa sababu mosi, watoto wakimaliza shule wanakosa ajira, na ya pili mimi kama mama nilizaa mtoto nikiwa bado msichana mdoggo sana, kwa hivyo kuwahusisha vijana katika biashara ndogo ndogo inawasaidia kujiepusha na vitendo kama vishawishi, mimba na ndoa za utotoni. Pia wakiuza matunda mwisho wa siku wanajipatia kipato ambacho kinawaondoa kwa umaskini.”

Irene Wambui ni mmoja wa vijana, wanasaidiana katika biashara ya kuuza matunda na Lucy akifanikiwa kupanua wigo wa biashara yake siku za usoni, Irene atamiliki mkahawa huu na atajisimamia na kuendeleza biashara yake.

“Nyumbani kwetu tumelelewa na mama pekee, na tulipitia changamoto nyingi mfano hatukuwa na chakula cha kutoshakaya yetu. Pia tuliishi kwenye umaskini na mahitaji ya shule hayakuwa yanapatikana kwa urahisi.  Kwa nafasi hii ya ajira tusidharau kwa sababu sasa nawezakusaidia mamangu kwa mahitaji ya kila siku, Niko na mtoto mdogo ambaye pia namgharamia mahitaji yake yote na tumeweza kuondokana na umaskini.” 

Irene Wambui, kijana aliyeajiriwa na Lucy Oduor katika mojawapo ya biashara zake katika eneo la Ngong lililo katika kaunti ya Kajiado nchini Kenya.
UN News
Irene Wambui, kijana aliyeajiriwa na Lucy Oduor katika mojawapo ya biashara zake katika eneo la Ngong lililo katika kaunti ya Kajiado nchini Kenya.

Irene anatamatisha kwa kutoa wito kwa vijana wenzake.

“Nawaambia vijana kujeni tufanye kazi, tafuta ajira kama hizi ndogo ndogo, zitawasaidia. Tujiepushe na mihadarati, tujiepushe na tabia ya kujiingiza katika Maisha ya uhalifu kwa sababu ukipatikana unazuiliwa gerezani na Maisha yako inaharibika.”