Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali ijayo ya Kenya iongeze uwekezaji kwenye hifadhi ya jamii- UNICEF

Mama akifanya kazi akiwa na mwanae, Suba, Kenya.
ILO/Marcel Crozet
Mama akifanya kazi akiwa na mwanae, Suba, Kenya.

Serikali ijayo ya Kenya iongeze uwekezaji kwenye hifadhi ya jamii- UNICEF

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Wakati Kenya ikijiandaa kwa uchaguzi mkuu tarehe 9 mwezi ujao wa Agosti, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF nchini humo linatoa wito kwa serikali itakayoingia madarakani ipatie kipaumbele hifadhi ya jamii ikiwemo kupatia fedha familia zilizo hatarini kama njia mojawapo ya kupunguza umaskini.
 

UNICEF inatoa wito huo wakati huu ambapo mradi wake wa majaribio kupatia fedha famiilia maskini zenye watoto umeanza kuzaa matunda.

Huyo ni Monika Muema, mkazi wa Kaunti ya Kajiado nchini Kenya. Yeye ni bibi na mlezi wa wajukuu watano na binti yake ambaye ni kiziwi. Monika ni mnufaika wa mradi wa UNICEF wa kupatia fedha kaya maskini ambapo kila mwezi hupatiwa takribani dola 17 ili kuweza kulea wajukuu zake akiwemo Alice mwanafunzi wa darasa la 7.

Ukosefu wa fursa za ajira na changamoto itokanayo na COVID-19 ilifanya hali kuwa mbaya zaidi na watoto wakashindwa hata kwenda shule.

Susan Momanyi, afisa wa UNICEF Kenya anasema, “hapa Kenya kaya milioni 1.4 zimeandikishwa kwenye mradi wa hifadhi ya jamii, na hivoy kuacha takribani watoto milioni 12 wanoahitaji huduma hiyo. Ndio  maana UNICEF inatoa wito kwa serikali ijayo ya Kenya kuongeza bajeti kwenye hifadhi ya jamii kwa asilimia 1.7 ya pato lake la ndani, kiwango ambacho ni sawa na nchi zingine za kipato cha kati ili kila mtoto anufaike.”

Sasa hata walimu wa Alice shuleni wanasema wameona tofauti tangu bibi yake aanze kunufaika na mradi wa kupatiwa fedha kwani mahudhurio ni bora halikadhalika sare za shule.