Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lugha mama ni silaha na urithi wetu lazima kuidumisha: Wakaazi Kenya

Wanawake wa Kimasai na watoto wao, wakaazi wa Kitengela, Kajiado nchini Kenya.
UN News/Thelma Mwadzaya
Wanawake wa Kimasai na watoto wao, wakaazi wa Kitengela, Kajiado nchini Kenya.

Lugha mama ni silaha na urithi wetu lazima kuidumisha: Wakaazi Kenya

Utamaduni na Elimu

Lugha na utamaduni vina muingiliano katika maisha ya kila siku. Hii ni kwa sababu vyote ni vipengele muhimu vya kujieleza katika jamii. 

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO, lugha ina umuhimu mkubwa kwa binadamu na ulimwengu kwa jumla kwani ndio kitambulisho cha jamii, chombo cha mawasiliano, elimu, maendeleo na huleta utangamano. 

Soundcloud

Lugha na tamaduni zinapotea 

Pale lugha inapoadimika, utajiri wa utamaduni nao unapotea. Hilo linajumuisha pia mila, utamaduni, fursa na kumbukumbu vyote vinakuwa hatarini na hususan kwa jamii za watu wa asili. 

Jamii ya Wamasai ni moja ya jamii za watu wa asili ambazo zinaendelea kufuata mila, tamaduni na kuitumia lugha yao katika maisha ya kila siku.  

Teresia Salonik ni mzazi na anaamini kuwa lugha ni silaha muhimu katika jamii ila,”Lugha ya mama sasa hivi kwa wakati huu inaenda ikiisha. Watoto wa saa hii hawajui lugha. Kwa sasa watoto hawakai nyumbani kuna hizi shule za kulala na wakienda huko wakirudi wanaongea kizungu na kiswahili na sisi pia tunalazimika kuzungumza hivyo nayo. Lakini ni muhimu wa kuijua kwani anaweza kuja mtu wa kabila jengine akakuvamia na kitakachokuokoa ni kuzungumza kwa lugha yako endapo unapiga kelele kwa kuitumia.” 

Umoja wa Mataifa kwa kutambua umuhimu wa lugha mama na mchango wake ulitenga siku maalum na sasa una muongo maalum wa lugha mama ukijikita zaidi na lugha za asili zilizo hatarini kutoweka ili kuupa uzito utajiri wa lugha na tamaduni mbalimbali duniani pamoja na matumizi ya lugha nyingi.  

Mvulana wa Kimasai akifurahia utamaduni wao huko Kajiado nchini Kenya.
UN News/Thelma Mwadzaya
Mvulana wa Kimasai akifurahia utamaduni wao huko Kajiado nchini Kenya.

Mamilioni ya watu hawana fursa ya kusoma kwa lugha mama 

Kulingana na shirika la, UNESCO, asilimia 40 ya watu kote ulimwenguni hawana nafasi ya kupata elimu kwa lugha wanayoijua au kuielewa.  

Hata hivyo hatua zimepigwa kutumia lugha nyingi katika elimu ukizingatia umuhimu wake hasa katika hatua za awali za masomo pamoja na matumizi yake katika maisha ya kila siku. 

Katika maisha ya kila siku lugha mama ina nafasi yake kama katika eneo hili la Makueni, ambako wakulima wamekuwa wakipata mafunzo ya mbinu za kisasa za kilimo kupitia lugha mama ya Kikamba kwani ndio jamii kubwa katika kaunti hii iliyoko mashariki mwa Kenya. 

Kennedy Mutua ni muuzaji wa dawa za kilimo na anawafunza wakulima kwa lugha mama na anasema,”Wakulima wengi huku ni wa vijijini.Huku mkulima ukimueleza kwa kiingereza hataweza kukuelewa. Mukiwasiliana na ile lugha mama mutaweza kuwaelewana vizuri. Kama ni dawa utamuelezea umuhimu wake kisha atafahamu. 

UNESCO inaelezea kuwa kiasi cha 43% ya lugha zisizopungua elfu 6 zinazozungumzwa duniani ziko katika hatari ya kusahaulika.  

Ni chache tu ambazo zimepewa uzito kwenye mifumo ya elimu na kutumiwa na umma, kadhalika zinazotumiwa kwenye ulimwengu wa dijitali hazifiki mia moja.Moses Mwinzi ni muuzaji wa mbegu eneo la Makueni na anakiri kuwa matumizi ya lugha mama yameleta tija kwenye biashara yake kwani kwa kawaida,”Tuko na wazee hawaelewi lugha nyengine na pia vijana ambao hawajasoma kwahiyo wanayoelewa ni hii lugha mama. Tunachotaka ni kila mtu akajaribu haya mafunzo kwenye shamba lake. Wakati wanapojisajili tunaangalia kwasababu lazima uandike majina matatu. Kisha tunakagua ni watu wangapi hawaijui hii lugha ndio tuweze kuwasaidia. Mashambani tunajaribu kutumia kiswahili lakini unapata wanaojua lugha mama ndio wengi zaidi. 

Mchango wa kutumia lugha nyingi shuleni 

Jamii zilizo na tamaduni mbalimbali hupata uhai kupitia lugha nyingi wanazotumia ambazo husambaza na kuhifadhi elimu asilia kwa njia endelevu kutoka kizazi hadi kizazi. 

UNESCO inasisitiza kuwa matumizi ya lugha nyingi yanaweza kuijumuisha jamii kadhalika kutimiza malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa yanayojikita katika kutoacha mtu yeyote nyuma. 

Shirika hilo linahimiza matumizi ya lugha nyingi kwenye elimu hasa kwa kuzingatia lugha mama.Mfumo huo unaanza na matumizi ya lugha anayoifahamu zaidi mwanafunzi na kisha anafunzwa nyengine kadri muda unavyoendelea.  

Mbinu hii inamuwezesha mwanafunzi ambaye lugha yake mama ni tofauti na ile inayotumika shuleni kuyaelewa mazingira ya shule katika lugha yake kwanza na hatimaye kushika mapya. 

Kushoto kwenda kulia, Joyce Kampus, Dorcas Naishorua na mamake mzazi wakiwa kwao Kitengela, Kajiado nchini Kenya.
UN News/Thelma Mwadzaya
Kushoto kwenda kulia, Joyce Kampus, Dorcas Naishorua na mamake mzazi wakiwa kwao Kitengela, Kajiado nchini Kenya.

Lugha mama ni jembe halimtupi mkulima 

Helen Koinett ni mkaazi wa Kajiado na anaamini kuwa lugha mama ni sawa na jembe haimtupi mkulima ukizingatia kuwa,”Mtu anapojifungua anakaa na yule mtoto mpaka wakati ule atakapojiunga na shule ya chekechea.Mama ndiye aliye na muda mrefu sana kuliko baba.Kwahiyo lugha mama ina umuhimu sana.Siku hizi kuna changamoto.Watoto wamekumbatia na kuegemea hizo lugha nyengine na kuchukulia kiswahili kama lugha mama yao.Lakini ukiijua lugha ya mama utaweza kufika mbali kwenye jamii.” 

Matumizi ya lugha nyingi yana mchango mkubwa na muhimu katika kuziunganisha jamii ambazo zinaruhusu tamaduni mbalimbali, mitazamo na mifumo ya elimu kufanya kazi sako kwa bako. 

Dorcas Naishorua ni kijana na anaelezea nafasi ya lugha mama kwa vijana wa sasa ambao wakiwa vijijini,”ukizungumza na wanajamii kwa lugha mama,unapata kwamba pia wanakuheshimu,na kukuchukulia kama mmoja wao. Unapowaeleza chochote wanakufahamu vyema katika lugha ya mama tofauti na kiswahili. Kuna wale ambao hawajasoma na wako kati yetu na wapo ambao kiswahili hawakijui na lugha wanaoitambua ni ya mama. Mara nyingi nikija nyumbani nafurahia kuzungumza kwa lugha mama na wananielewa .”