Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Joto na mafuriko huathiri wanawake na wanaume wa vijijini tofauti na kuongeza tofauti ya kipato

Margerita, Mwanamke mkulima nchini Sudan Kusini, anapanda mbegu za zao la mahindi. (Maktaba)
FAO/Jean Di Marino
Margerita, Mwanamke mkulima nchini Sudan Kusini, anapanda mbegu za zao la mahindi. (Maktaba)

Joto na mafuriko huathiri wanawake na wanaume wa vijijini tofauti na kuongeza tofauti ya kipato

Tabianchi na mazingira

Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO limezitaka nchi kuhakikisha zinashughulikia changamoto za usawa wa kijinsia kwenye kupambana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi kwani takwimu zinaonesha kuwa familia hususan za vijijini zinazoongozwa na wanawake zinaathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi ikilinganishwa na zile zinazoongozwa na wanaume.

Utafiti uliopewa jila la Mabadiliko ya tabianchi yasiyo ya haki umebainisha kuwa familia zinazoongozwa na wanawake zinapoteza asilimia nane zaidi ya kipato kutokana na joto na asilimia tatu kutokana na mafuriko ikilinganishwa na zile zinazoongozwa na wanaume, asilimia hizo ina maanisha punguzo la Dola bilioni 37 na bilioni 16 mtawalia kwa nchi za kipato cha chini na cha kati.

Utafiti unapendekeza kwamba ikiwa tofauti hizi hazitashughulikiwa, mabadiliko ya tabianchi yatapanua sana utofauti wa kifedha baina ya wanawake na wanaume katika miaka ijayo.

Akizungumzia ripoti hiyo Mkurugenzi Mkuu wa FAO Qu Dongyu amesema “Tofauti za kijamii kutokana na maeneo, mali, jinsia na umri zina nguvu lakini athari zake hazieleweki vizuri kwa watu wa vijijini wanaoathirika na athari mabadiliko ya tabianchi.”

Utafiti huo umeangazia sera, program mbalimbali ikiwemo za kijinsia vijijini na hatua za kupambana na mabadiliko ya tabianchi ambapo Mkurugenzi huyo wa FAO akaeleza kuwa utafiti huo ni muhimu kwani “Matokeo haya yanaangazia hitaji la dharura la kujitolea zaidi kwa rasilimali za kifedha na kuwa na sera makini kwa masuala ya ujumishi na ustahimilivu katika hatua za kupambana na mabadiliko ya tabianchi duniani na kitaifa”

Miongoni mwa mambo muhimu kadhaa yaliyoelezewa kuhusu maboresho ya kisera, ripoti hiyo imeshauri nchi kuwekeza katika sera na programu zinazoshughulikia udhaifu wa mabadiliko ya tabianchi kwa pande nyingi kwa watu wa vijijini na vikwazo vyao mahususi, ikiwa ni pamoja na upatikanaji mdogo wa rasilimali za uzalishaji.

Pia ripoti hiyo inapendekeza kuunganisha programu za ulinzi wa jamii na huduma za ushauri ambazo zinaweza kuhimiza kukabiliana na hali hiyo na kuwafidia wakulima kwa wale walioshindwa, kama vile programu za usaidizi wa kijamii zinazotegemea fedha taslimu.

Utafiti huu wa FAO ulichambua takwimu za kijamii na kiuchumi kutoka zaidi ya kaya 100,000 za vijijini (zinazowakilisha zaidi ya watu milioni 950) katika nchi za kipato cha chini na cha kati.