Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mpango wazinduliwa kuhakikisha mipango miji inatilia maanani masuala ya chakula bora na lishe mijini

Mkuu wa FAO Jose Graziano da Silva.
FAO/Giuseppe Carotenuto
Mkuu wa FAO Jose Graziano da Silva.

Mpango wazinduliwa kuhakikisha mipango miji inatilia maanani masuala ya chakula bora na lishe mijini

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la chakula na kilimo duniani, FAO, José Graziano da Silva amesema masuala ya mipango miji ni lazima yazingatie pia masuala ya chakula na lishe kama njia mojawao ya kufanikisha lengo la kutokomeza nja duniani na lishe bora kwa wote.

Bwana da Silva amesema hayo leo huko Roma, Italia wakati wa uzinduzi wa mfumo wa FAO kuhusu chakula mijini, ukilenga suala la maendeleo endelevu.

Muundo ulioanzishwa leo unalenga kusaidia wapitisha maamuzi katika ngazi mbalimbali ya jinsi gani miji inaweza kuchukua hatua za kuchochea upatikanaji wa ajira, kuimarisha mnyororo wa thamani wa chakula na kupunguza viwango vinavyotia shaka vya upotevu wa chakula mijini.

Amesema “tunapaswa kujumuisha miji kwasababu ndipo ambako idadi kubwa zaidi ya watu itaendelea kumiminika, kuishi, kula na kufanya kazi na ndiko lazima tutekeleze ahadi zetu wa kimataifa kwa kiwango cha mashinani.”

Mkuu huyo wa FAO amebaini kuwa ni katika maeneo ya mijini ambako sheria na kanuni kuhusu vyakula zinatungwa na ndio maana shirika lake linaendelea kushirikiana kwa kina zaidi na miji.

Amesema takribani asilimia 55 ya watu duniani tayari wanaishi mijini na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka na kufikia asilimia 65 mwaka 2050 na kwamba zaidi ya asilimia 80 ya chakula kinachozalishwa duniani wakati huo kitakuwa kinatumika mijini.

“Ukuaji wa miji unaleta changamoto za kipekee katika kuhakikisha kila mtu anapata chakula bora kwa bei nafuu huku akiwa na afya njema bila kutumia kupita kiasi rasilimali zilizopo,” amesema Bwana da Silva akiongeza kuwa kwa hali ilivyo sasa maendeleo ya mijini hayapaswi kutenganishwa na maendeleo vijijini.

Ameema “michakato hiyo miwili lazima iende kwa pamoja badala ya kuona ya kwamba mabadiliko ya ukuaji wa miji ni tofauti na maendeleo vijiini,” amesema mkuu huyo wa FAO akisema ni lazima kuondokana na dhana hiyo ya utenganishaji wa miji na vijiji katika michakato ya maendeleo.

FAO inasisitiza umuhimu wa kusikiliza wakazi wa pande hizo, kutambua mahitaji yao na kuweka miradi ambamo kwayo itasaidia katika uzalishaji wa chakula bora na chenye lishe na hatimaye kupunguza pengo la usawa kwenye upatikanaji wa chakula.