Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhakika wa chakula duniani uko mikonini mwa wanawake:Mashirika ya UN

Mwanamke akichambua majani ya Moringa katika kisiwa cha Tristao Guinea
© UN WOMEN/Joe Saad
Mwanamke akichambua majani ya Moringa katika kisiwa cha Tristao Guinea

Uhakika wa chakula duniani uko mikonini mwa wanawake:Mashirika ya UN

Wanawake

Katika siku ya kimataifa ya wanawake mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa yamepaza sauti ili kuhakikisha pengo la kidijitali linazibwa ili kutoa fursa za wanawake kushamiri na kufikia uwezo wao kila kona na kila nyanja na hususan wanawake wa vijijini.

Mashirika yanayohusika na mifumo ya chakula kwenye Umoja wa Mataifa lile la chakula na kilimo FAO , mfuko wa kimataifa kwa ajili ya maendeleo ya kilimo IFAD na mpango wa chakula duniani WFP yamehimiza kuinua uwezo wa kidijitali wa wanawake wa vijini na kushughulikia vikwazo wanavyokabiliana navyo katika kupata fursa za teknolojia ili waweze kuwa wachangiaji sawa katika mifumo ya uzalishaji wa chakula.

Kwa mujibu wa mashirika hayo ufikiaji jumuishi wa teknolojia na elimu ya kidijitali ni muhimu katika kupunguza kukosekana kwa usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake na wasichana wa vijijini.

Katika hafla maalum ya kuadhimisha siku hii ya wanawake mashirika hayo yamesema  yanatambua kuwa ingawa uwezo wa kidigitali peke yake hauwezi kutatua changamoto zote hasara zinazohusiana na masuala ya kijinsia ambazo wanawake wanakabiliana nazo, lakini ikiwa watapewa fursa za ufikiaji sawa wa teknolojia ya kidijitali na elimu, wanawake wanaweza kuwa na jukumu tendaji na kubwa zaidi katika mifumo ya kilimo.

Teknolojia ya simu za mkononi inawasaidia wanawake wa vijijini katika maeneo kama Guatemala
UN Women/Ryan Brown
Teknolojia ya simu za mkononi inawasaidia wanawake wa vijijini katika maeneo kama Guatemala

Tunapowekeza kwa wanawake vijijini tunawekeza katika mnepo:FAO

Naibu mkurugenzi mkuu wa FAO Beth Bechdol katika ujumbe wake amesema "Ni kweli, inakatisha tamaa kusherehekea siku ya kimataifa ya wanawake katika wakati ambapo tunarudi nyuma kwenye usawa wa kijinsia na tunaona mapungufu ya kijinsia katika sayansi, teknolojia na uvumbuzi".

Ameendela kusema kwamba "Tunapowekeza kwa wanawake wa vijijini, tunawekeza katika mnepo, katika mustakabali wa jamii zetu na katika kuunda ulimwengu jumuishi zaidi na wenye usawa ambao hakuna anayeachwa nyuma."

Tusipochukua hatua wanawake wataendelea kubaki nyuma:IFAD

Kikundi cha Amaati kinawawezsha wanawake wa kijijini nchini Ghana kupitia kilimo cha mazao ya asili kama fonjo
© Amaati Group
Kikundi cha Amaati kinawawezsha wanawake wa kijijini nchini Ghana kupitia kilimo cha mazao ya asili kama fonjo

IFAD shirika ambalo limewekeza zaidi katika Maisha na mustakbali wa wakulima vijijini kupitia makamu wa rais msaidizi wa idara ya mkakati na maarifa wa IFAD Jyotsna Puri aimesema "Bila kuongezeka kwa upatikanaji wa teknolojia ya kidijitali na uvumbuzi, wanawake na wasichana wa vijijini wataendelea kukumbana na vikwazo na hasara za kijamii na kiuchumi, na hivyo kufanya iwe vigumu kwao kushiriki kikamilifu katika ukuzaji uchumi wa vijijini,".

Puri amesisitiza kuwa "Ukosefu wa usawa wa kijinsia na mgawanyiko baina ya mijini na vijijini utazidi kuwa mbaya zaidi endapo hatutounda jamii zilizo jumuishi zaidi na zenye ustawi kwa kila mtu."

Uhakika wa chakula uko mikononi mwa wanawake:WFP

Naye naibu mkurugenzi mtendaji wa WFP, Valerie Guarnieri  akisistiza umuhimu wa machango wa wanawake katika uhai wa dunia huu amesema "Uhakika wa chakula kwa kaya na jamii uko mikononi mwa wanawake. Ni kupitia uwezeshaji wa wanawake pekee ndipo tunaweza kujenga ulimwengu ambapo hakuna mtu anayelala njaa,”.

Akaenda mbali zaidi na kuhimiza kwamba “Kuweka rasilimali mikononi mwa wanawake ni jambo lisilohitaji akili nyingi, na kwa hili linakuja na uhamishaji wa maarifa na ujuzi ikiwa ni pamoja na ujuzi wa kidijitali kuwasaidia wanawake hawa kutambua na kufikia uwezo wao kamili. Sasa hiyo ndiyo aina ya mabadiliko ya kweli ambayo sote tunaweza kuyaunga mkono.”