Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunashirikiana kukwamua wakazi wa vijijini na hatujali nani anapata sifa- WFP

Kuwezesha wakulima vijijini kutasaidia kuinua kipato cha wakazi wa maeneo hayo na kuondoa tofauti kati ya mijini na vijijini. (Picha@FAO-Tanzania)

Tunashirikiana kukwamua wakazi wa vijijini na hatujali nani anapata sifa- WFP

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Wakazi wa vijijini wanahaha siyo tu kusaka chakula bali pia kujikwamua kiuchumi jambo ambalo mashirika matatu ya Umoja wa Mataifa wameamua kuweka sifa pembeni na kushirikiana ili kuwaokoa.

Mashirika matatu ya Umoja wa Mataifa yanayohusika na kutokomeza njaa na kuchagiza maendeleo vijijini yameazimia kuimarisha ushirikiano wao ili hatimaye kusaidia nchi wanachama kufikia lengo namba 2 la maendeleo endelevu la kutokomeza njaa.

Mashirika hayo ambayo ni lile la chakula na kilimo, FAO, mfuko wa kimataifa wa maendeleo ya kilimo, IFAD na mpango wa chakula duniani, WFP wametia saini makubaliano hayo ya miaka mitano leo huko Roma, Italia na yanaanza kutekelezwa leo.

Makubaliano hayo yametaja maeneo ya usaidizi kwa nchi husika ikiwemo mchakato wa mipango ya kitaifa na serikali pamoja na kuandaa matarajio  ya matokeo na ufanyaji wa tathmini.

Halikadhalika inahusisha uchambuzi wa pamoja wa data, uwajibikaji wa pamoja wa matokeo ya mipango iliyoainishwa na kuendelea kubadilishana huduma, taarifa ikiwemo za matokeo ya mipango husika.

Image
Upatikanaji wa mashine za kilimo ni muhimu kwa ajili ya uzalishaji na maisha ya vijijini. Picha: FAO/Swiatoslaw Wojtkowiak

Akizungumza mpango huo, Mkurugenzi Mkuu wa FAO, José Graziano da Silva amesema ushirikiano ndio njia mujarabu ya kusaidia nchi kufanikisha ajenda 2030 kwa maendeleo endelevu.

Naye Mkuu wa IFAD Gilbert F. Houngbo amesema nyaraka waliyotia saini ni zaidi ya nyaraka ya kisheria kaw kuwa inaonyesha mipango mipya  ya usaidizi halisi na mbinu bunifu za kushikiriana ili kuimarisha matokeo ya kazi zao za kuboresha maeneo ya vijijini na ustawi wa familia.

“Tunafanya kazi pamoja kwa wigo mpana zaidi na kwa ufanisi zaidi kuliko awali, kwasababu mazingira ya kibinadamu hivi sasa yanataka kufanyika jambo hilo. Na hii haijalishi nani anasifiwa alimradi watu wanaohitaji msaada wetu wananufaika. Zama hizi mpya za ushirikiano zinamaanisha kuwa kazi tunayofanya itakuwa fanisi zaidi na itakuwa na athari chanya zaidi kadri tunavyosonga kufanikisha lengo letu la kutokomeza njaa,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa WFP.

FAO, IFAD na WFP kila mmoja ana mamlaka ya aina yake ya kusaidia utaalamu wa kiufundi, usaidizi wa kifedha na misaada ya dharura ya chakula.

Malengo ya maendeleo endelevu, SDG iliyokubaliwa na nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa mwaka 2015 imeweka ukomo wa mwaka 2030 ili kufanikisha malengo 17 ya kijamii, kiuchumi na kimazingira.

 

TAGS: SDGs, FAO, IFAD, WFP