Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

'Hatuwezi kuwatelekeza watu wa Gaza': wakuu wa mashirika ya UN na mashirika yasiyo ya kiserikali

Timu za UNRWA zinafanya kazi usiku kucha kusambaza chakula kwa Wapalestina waliokata tamaa.
© UNRWA
Timu za UNRWA zinafanya kazi usiku kucha kusambaza chakula kwa Wapalestina waliokata tamaa.

'Hatuwezi kuwatelekeza watu wa Gaza': wakuu wa mashirika ya UN na mashirika yasiyo ya kiserikali

Msaada wa Kibinadamu

Wakati mapigano makali na mashambulizi ya makombora yaliendelea huko Khan Younis kusini mwa Gaza usiku wa kuamkia leo Jumatano, wasaidizi wakuu wa Umoja wa Mataifa na wakuu wa mashirika yasiyo ya kiserikali wameonya juu ya ‘matokeo mabaya’ ya kutofadhili shughuli za Shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA ambalo linashutumiwa kushirikiana na wanamgambo wa kipalestina wa Hamas.

Licha ya madai "ya kutisha" ya kwamba wafanyakazi 12 wa UNWRA walihusika katika mashambulizi ya kigaidi yaliyoongozwa na wanamgambo wa Hamas dhidi ya Israeli tarehe 7 Oktoba, 2023 "tunapaswa kutozuia shirika zima kutekeleza wajibu wake wa kuhudumia watu wenye mahitaji makubwa", imesema taarifa ya pamoja ya mashirika ya misaada ya kibinadamu ikiongozwa na Umoja wa Mataifa ikijulikana kama Kamati ya Kudumu ya Mashirika ya Kimataifa (IASC).

Jopo hilo la IASC, linaloongozwa na mkuu wa Umoja wa Mataifa wa misaada ya dharura Martin Griffiths limeeleza kwenye taarifa hiyo kwamba “Kuinyima fedha UNRWA ... kutasababisha kuporomoka kwa mfumo wa utoaji misaada ya kibinadamu huko Gaza, na athari kubwa za kibinadamu na haki za binadamu katika eneo hilo zima la Palestina."

Tangu mashambulizi ya Israel na uvamizi wa ardhini kuanza baada ya wanamgambo wa Kipalestina kuwaua takriban watu 1,200 katika jamii za Israel na kuwachukua mateka zaidi ya 250, mamia kwa maelfu ya watu wameachwa bila makazi na “Wapo ukingoni kukumbwa na baa la njaa”, wamesema Wakuu wa IASC, 

Bofya hapa kusoma taarifa hiyo ya pamoja iliyosainiwa na wakuu wa mashirika 14 ikiwemo ya UN na wadau wake. 

Majukumu ya UNRWA

UNRWA lililoanza shughuli zake mwaka 1949 ni shirika kubwa zaidi la misaada huko Gaza ambao jukumu lake kuu ni katika elimu, huduma za afya na linatoa msaada wa kuokoa maisha kwa zaidi ya watu milioni mbili katika Ukanda huo.

Mustakabali wake uko hatarini baada ya wafadhili kadhaa wakuu kusitisha fedham wakisubiri uchunguzi wa madai ya Israel kwamba wafanyakazi 12 kati ya 30,000 wa shirika hilo walihusika katika mashambulizi ya Oktoba 7.

Uchunguzi umeanza

Wakuu wa IASC wamesema kuwa uchunguzi kamili na wa haraka tayari unaendelea na unafanywa na Ofisi ya Huduma za Uangalizi wa Ndani (OIOS) - chombo cha juu zaidi cha uchunguzi katika mfumo wa Umoja wa Mataifa. 

UNRWA pia imetangazwa kufanyika kwa mapitio huru ya shughuli zake.

“Maamuzi ya Nchi Wanachama mbalimbali kusitisha fedha kwa ajili ya UNRWA yatakuwa na matokeo mabaya kwa watu wa Gaza,” taarifa ya IASC iliendelea kueleza. “Hakuna chombo kingine chenye uwezo wa kutoa kiwango na upana wa msaada ambao watu milioni 2.2 wa Gaza wanahitaji kwa dharura.”

Katika chapisho lake la hivi karibuni la shughuli za kibinadamu, ofisi ya uratibu wa misaada ya Umoja wa Mataifa, OCHA, ilibainisha kuwa idadi ya waliofariki Gaza tangu kuanza kwa mashambulizi ya makali ya Israel sasa imeongezeka hadi 26,751, kulingana na mamlaka ya afya ya enclave.

Uhasama umeendelea kuwa "hasa mkubwa" katika mji wa kusini wa Khan Younis, OCHA iliripoti jana Jumanne, "huku mapigano makali yakiripotiwa karibu na hospitali ya Nasser na Al Amal, na ripoti za Wapalestina wanaokimbilia mji wa kusini wa Rafah, ambao tayari umejaa watu wengi, licha ya ukosefu wa njia salama”.

Operesheni za ardhini na mapigano kati ya wanajeshi wa Israel na makundi yenye silaha ya Palestina pia ziliripotiwa katika sehemu kubwa ya Gaza, OCHA ilibainisha. 

Pia kuna amri mpya za watu kutakiwa kuhama zilizotolewa kwa vitongoji vilivyoko magharibi mwa Gaza siku ya Jumatatu na Jumanne, ikiwa ni pamoja na Kambi ya Wakimbizi ya Ash Shati, Rimal Ash Shamali na Al Janubi., Sabra, Ash Sheikh 'Ajlin, na Tel Al Hawa.

“Agizo hilo jipya lilihusisha eneo la kilomita za mraba 12.43…Eneo hili lilikuwa makazi ya Wapalestina 300,000 kabla ya mapigano kuanza tarehe 7 Oktoba na, baadaye, makazi 59 yenye wastani wa wakimbizi wa ndani 88,000” OCHA ilisema.

Maeneo ya makazi yanazidi kupungua

Kwa mujibu wa ofisi ya uratibu wa misaada ya Umoja wa Mataifa, maagizo mengi ya kuwahamisha watu yaliyotolewa na jeshi la Israel yaliyoanza tarehe 1 Disemba yanachukua jumla ya kilomita za mraba 158, sawa na asilimia 41 ya Ukanda wa Gaza. “Eneo hili lilikuwa makazi ya Wapalestina milioni 1.38 kabla ya Oktoba 7 na, baadae, lilikuwa na makao 161 yanayohifadhi wastani wa wakimbizi wa ndani 700,750.” 

Hadi kufikia Januari 30, wanajeshi 218 wa Israel wamethibitishwa kuuawa na 1,283 kujeruhiwa, limesema jeshi la Israel.

Wiki iliyopita pia imeshuhudia "idadi kubwa ya wanaume wa Kipalestina" wakizuiliwa na jeshi la Israel katika kituo cha ukaguzi huko Khan Younis "huku wengi wao wakiwa wamechukuliwa, wamevuliwa nguo zao za ndani, na wamezibwa macho ", taarifa ya OCHA iliripoti.

Idadi ya watu walio katika mazingira magumu kaskazini na kati ya Gaza wanazidi kutoweza kufikiwa kwa sababu ya "mienendo inayoongezeka ya kunyimwa na kuwekewa vikwazo", ofisi ya uratibu wa misaada ya Umoja wa Mataifa iliripoti. "Sababu ni pamoja na kucheleweshwa kupita kiasi kwa misafara ya misaada ya kibinadamu kabla au katika vituo vya ukaguzi vya Israeli na kuongezeka kwa uhasama katikati mwa Gaza. 

Vitisho kwa usalama kwa wafanyakazi wa kibinadamu na maeneo yao ya kazi vimeripotiwa mara kwa mara, na hivyo kuzuia utoaji wa misaada ya kuokoa maisha na kusababisha hatari kubwa kwa wale wanaohusika katika jitihada za kibinadamu."