Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Njia ya kisiasa yahitajika kuitoa Gaza kwenye janga la kibinadamu: Türk

Volker Türk, Kamishina Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa akihutubia wanahabari mjini Geneva.
UN Geneva/Daniel Johnson
Volker Türk, Kamishina Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa akihutubia wanahabari mjini Geneva.

Njia ya kisiasa yahitajika kuitoa Gaza kwenye janga la kibinadamu: Türk

Amani na Usalama

Kamishina Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk leo  alikaribisha wito wa Baraza la Usalama wa kusitishwa kwa mapigano huko Gaza ambapo "madaktari wanawafanyia upasuaji watoto wanaopiga mayowe bila ganzi, wakitumia simu za rununu kwa mwanga,” kabla ya kuziomba moja kwa moja pande zinazozozana kuweka silaha zao chini.

Akizungumza mjini Geneva, Kamishna Mkuu huyo amezitaka pande husika kwenye mzozo "kuunda fursa ya kisiasa kwa ajili ya njia ya kutoka kwenye hali hii ya kutisha inayoighubika Gaza".

Bwana Türk amelaani kulengwa kwa raia katika muda wa wiki tano zilizopita za uhasama na akahimiza uwajibikaji kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.

Amesisitiza kwamba mashambulizi yanayoelekezwa kwa "hospitali, shule, masoko na maduka ya mikate pamoja na adhabu ya pamoja katika hatua ya kuzingirwa kunakofanywa na Israel huko Gaza ni marufuku chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu.”

Vile vile amesema pia ni marufuku "Kulenga makombora ya kiholela kuelekea kusini mwa Israeli kunakofanywa na vikundi vyenye silaha vya Palestina, utekaji nyara na matumizi ya raia kama ngao katika baadhi ya maeneo kutokana na operesheni za kijeshi". 

Türk ameweka bayana kwamba "Niko katika upande wa kila raia, awe Palestina au Muisrael ambaye amejeruhiwa, au ambaye anaishi kwa hofu".

Usitishaji mapigano watakiwa sasa

Akizungumzia kuhusu hali mbaya ya kibinadamu katika eneo hilo la Gaza baada ya kutoa taarifa kwa mataifa wanachama na waandishi wa habari mjini Geneva, Bwsana. Türk ameangazia pia vifo vingi vya wagonjwa katika hospitali ya Al-Shifa Gaza iliyozingirwa na kuongezeka kwa mashambulizi dhidi ya huduma za afya katika Ukanda huo. 

Amesema Tangu tarehe 7 Oktoba, mashambulizi 137 kama hayo yamerekodiwa na shirika la afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO.

Mkuu huyo wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema “Watu waliolazimishwa kuhamia kusini kutokana na mashambulizi ya mabomu na mapigano ya Israel chinichini, wakiwa wamebeba wanafamilia wazee, na watoto waliojeruhiwa wakati mwingine, wakitembea polepole kwenye barabara iliyojaa mabomu, na wale ambao hawawezi kusonga mbele bado wamekwama kaskazini mwa Gaza.”

Amesisitiza kuwa kusitisha uhasama ili kutoa fursa kwa hatua za kibinadamu, kama inavyotakiwa na azimio nambari 2712 la Baraza la Usalama lililopitishwa jana Jumatano usiku, ni muhimu sana, na amezitaka pande zinazohusika "kutekeleza mara moja, wito huo wa Baraza la Usalama”.

Uharibifu mkubwa unaonekana katika ukanda wa Gaza kufuatia mashambulizi ya anga ya Israel tarehe 10 Oktoba 2023.
WHO
Uharibifu mkubwa unaonekana katika ukanda wa Gaza kufuatia mashambulizi ya anga ya Israel tarehe 10 Oktoba 2023.

Hakuna tena mahala salama

Kamishna Mkuu ameunga mkono mpango wenye vipengele 10 uliowasilishwa Jumatano na mkuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura Martin Griffiths, hasa kuhusu hitaji la kutoa mafuta kwa malori ya misaada, hospitali, maduka ya kuoka mikate na mitambo ya kuondoa chumvi kwenye maji.

Kwa kuzingatia maoni ya Bwana Griffiths,  Kamishina Türk ameonya kwamba mapendekezo ya kile kinachoitwa "eneo salama hayawezi kutekelezwa kwa sababu eneo hilo si salama tena wala na wala haliwezekani kukalika kwa idadi kubwa ya watu wenye uhitaji".

Uchunguzi wa uhalifu wa kivita

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hitaji la haki na uwajibikaji, amesema kuandika na kuchambua ushahidi wa ukiukwaji wote ni mchakato mrefu na muhimu. 

Amesisitiza umuhimu wa kuifikia Israel na ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa kwa ajili ya ufuatiliaji huru.

Ambapo amesema mamlaka za kitaifa "zinapothibitisha kutokuwa tayari au haziwezi kufanya uchunguzi, na panapo na simulizi zinazopingwa kuhusu matukio muhimu uchunguzi wa kimataifa unaweza kuitishwa”.

Alipoulizwa kuhusu kisa cha hospitali ya Al-Shifa, ambayo imeshambuliwa na jeshi la Israel wiki hii, amesema “kulikuwa na kauli zinazokinzana juu ya matukio hayo, ambayo yangehitaji uchunguzi huru wa kimataifa ili kujua nini hasa kinatokea" .

Vikosi vya ulinzi vya Israel vilivamia hospitali hiyo vikidai kuwa Hamas wameanzisha kituo chake chini ya hospitali hiyo  madai ambayo yamekanushwa na na wahudumu wa afya katika hospital hiyo.

Hatari ya mzozo kusambaa

Bwana Türk pia amesisitiza kwamba mgogoro "unasambaa zaidi ya Gaza, na hali inawezekana kulipuka katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa, ambapo mashambulizi ya walowezi dhidi ya Wapalestina na matumizi ya njia za kijeshi katika operesheni za kutekeleza sheria yanaongezeka.”

Baada ya kurejea kutoka katika ziara ya kanda hiyo wiki iliyopita, mkuu huyo wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa pia amesema anungana na "hisia za kina za wasiwasi wa wengi juu ya hatari ya mzozo huo kusambaa katika eneo pana la Mashariki ya Kati, ikiwa mwelekeo wa sasa utaendelea”.

Ameonya dhidi ya mtego wa ubaguzi zaidi, akisisitiza kwamba "kila mmoja wetu anahitaji kujitahidi kutafuta msingi na suluhisho la pamoja."