Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunahitaji utaratibu wa kimataifa ambao unafanya kazi kwa kila mtu: Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia katika Mkutano wa Usalama mjini Munich nchini Ujerumani.
United Nations/Stephanie Tremblay
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia katika Mkutano wa Usalama mjini Munich nchini Ujerumani.

Tunahitaji utaratibu wa kimataifa ambao unafanya kazi kwa kila mtu: Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres leo katika mkutano wa usalama unaofanyika mjini Munich Ujerumani ametoa wito wa kuwepo utaratibu wa kimataifa ambao unafanya kazi kwa kila mtu. 

Guterres katika hotuba yake amesisitiza wito huo wa amani na utaratibu wa kisasa wa kimataifa akisema utaratibu wa leo wa kimataifa haufanyi kazi kwa kila mtu, "Kwa kweli, ningeenda mbali zaidi na kusema kwamba haufanyi kazi kwa mtu yeyote." 

Akielezea hali ya kimataifa, Katibu Mkuu  amesema  hivi sasa dunia inakabiliwa na changamoto lukuki, lakini jumuiya ya kimataifa imegawanyika zaidi kuliko wakati mwingine wowote katika miaka 75 iliyopita.

Amesisitiza kwamba "Leo hii tunashuhudia nchi zikifanya chochote wapendacho, bila uwajibikaji." 

Ameonya kwamba “Kama Ripoti ya Usalama ya Munich inavyoweka bayana mafanikio ya jamii kupitia ushindani kati ya nchi yanapewa kipaumbele badala ya kuangalia faida kwa wote, kupitia ushirikiano”. 

Ripoti ya Usalama ya Munich huchapishwa kila mwaka kabla ya mkutano na kuchambua masuala muhimu ya sera ya usalama.

Guterres ameongeza kuwa migogoro inaongezeka, inayohusishwa na ushindani na kutokujali.

Hivyo amesisitiza kuwa utaratibu wa kimataifa ambalo linafanya kazi kwa kila mtu lazima lishughulikie mapungufu haya na kutoa suluhisho.

"Ikiwa nchi zingetimiza wajibu wao chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa, kila mtu duniani angeishi kwa amani na utu".

Mgogoro Mashariki ya Kati

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, hali ya Gaza ni janga la kutisha la mkwamo katika uhusiano wa kimataifa.

Hakuna kinachoweza kuhalalisha mashambulizi ya kiholela yaliyoanzishwa na Hamas tarehe 7 Oktoba, Guterres amesisitiza kwa wakuu wa nchi na serikali kutoka duniani kote mjini Munich na kuongeza kuwa “Na hakuna kinachoweza kuhalalisha adhabu ya pamoja ya watu wa Palestina katika hatua za kijeshi za Israeli.

Mashambulizi ya kila upande dhidi ya mji wa Gaza yatakuwa mabaya kwa raia wa Palestina ambao tayari wako kwenye zahma kubwa, ameonya Guterres katika hotuba yake kwa washiriki wa ngazi za juu wa mkutano huo.

"Nimetoa wito mara kwa mara kuachiliwa mara moja na bila masharti kwa mateka wote, na kusitishwa kwa mapigano kwa minajili ya kibinadamu. Huu lazima uwe msingi wa hatua madhubuti na zisizoweza kutenduliwa kuelekea suluhisho la serikali mbili, kwa kuzingatia maazimio ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa.”

Katibu Mkuu António Guterres akitoa hotuba yake katika 'Kongamano la Usalama la Munich' mjini Munich, Ujerumani.
MSC/Marc Muelle
Katibu Mkuu António Guterres akitoa hotuba yake katika 'Kongamano la Usalama la Munich' mjini Munich, Ujerumani.

Ufadhili wa fedha wahitajika

Katibu Mkuu pia amezungumzia changamoto ya fedha duniani akisema “Tunahitaji hatua za haraka katika maeneo mawili mosi: kichocheo cha dola bilioni 500 kila mwaka katika ufadhili wa muda mrefu wa kumudu kwa nchi zinazoendelea kuwekeza katika Malengo ya Maendeleo Endelevu, kama ilivyoidhinishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba mwaka jana.

Tunafanya kazi na kikundi kidogo cha wakuu wa nchi ili kutetea na kufuatilia utekelezaji wake.”

Na pili tunahitaji wakati mpya wa Bretton Woods ili kurekebisha usanifu wa kifedha duniani, ili ulingane na uchumi wa sasa wa kimataifa na iweze kuunda wavu wa kweli wa usalama wa kimataifa, hasa kwa nchi zinazoendelea zinazozama katika madeni.

Mkutano wa kilele wa siku zijazo utazingatia hitaji la marekebisho ya kina ili kufanya taasisi na mifumo hii kuwa ya ulimwengu wote, jumuishi na inayozingatia sheria.

“Hii ni muhimu ili kuunda uchumi wa kimataifa ambao unafanya kazi kwa kila mtu, kila mahali."

Mkutano wa kilele wa siku zijazo kwa changamoto za karne ya 21

Zaidi ya kukabiliana na migogoro ya mara moja, kama vile unaoendelea Ukraine, Sudan au Libya, Guterres amesema “tunahitaji kuimarisha usanifu wa amani na usalama wa kimataifa ili kukabiliana na vitisho na changamoto za leo, kama vile mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi, akili bandia au akili mnemba, au kutumia mtandao kama silaha.”

Ameeleza kuwa Ajenda Mpya ya Amani, ambayo itajadiliwa katika Mkutano wa Kilele wa Siku Zijazo mwezi Septemba mwaka huu, inalenga kusahihisha mifumo ya pamoja ya usalama kwa kuzingatia mtandao na ushirikiano wa kimataifa zaidi kwa ulimwengu kwa ajili ya kipindi cha mpito.

Ziara katika Sinagogi la Ohel Jakob Munich

Jana Alhamisi, siku moja kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Usalama wa Munich, Guterres alitembelea sinagogi la "Ohel Jakob" kwa mwaliko wa Baraza la kimataifa la Kiyahudi, pamoja na Charlotte Knobloch, Rais wa Jumuiya ya Kiyahudi ya Munich na Upper Bavaria na Makamu wa Rais wa zamani wa Kongamano la Kiyahudi la Dunia.

Knobloch na Guterres walipitia "Walk of Remembrance", ambayo ina majina ya Wayahudi zaidi ya 4,500 wa Munich ambao waliuawa wakati wa enzi ya Manazi.

Wakati wa ziara yake katika sinagogi hilo, Guterres alisema kwamba anachukulia vita ya chuki dhidi ya Wayahudi kuwa "wajibu wa kimaadili" wa kila mwanadamu. 

Amesema watu wa Israeli wana haki ya kuishi kwa usalama. Hili halipaswi kutiliwa shaka, hata kama mtu hakubaliani na sera za serikali ya Israel.