Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza Kuu lakutana kujadili kura turufu iliyotumika Baraza la Usalama

Kikao Maalum cha Dharura cha Baraza Kuu UN kinakutana kuhusu hali katika Mashariki ya Kati, ikiwemo suala la Palestina.
United Nations Kikao Maalum cha Dharura cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kinakutana kuhusu hali ya Mashariki ya Kati, likiwemo swali la Wapalestina.

Baraza Kuu lakutana kujadili kura turufu iliyotumika Baraza la Usalama

Amani na Usalama

Kipaumbele cha sasa huko Gaza, ukanda wa Mashariki ni kuokoa maisha ya raia, amesema Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hii leo wakati nchi wanachama wamekutana kujadili kitendo cha Marekani kutumia kura turufu kwenye Baraza la Usalama mwezi uliopita.  

Naibu Rais wa Baraza hilo Cheikh Niang kutoka Senegal, amesema  hayo akihutubia kwa niaba ya Rais Dennis Francis kwenye kikao hicho maalum kikibeba maudhui Hali ya Mashariki ikiwemo hoja ya Palestina. 

Balozi Francis kwenye hotuba yake amekaribisha kupitishwa kwa azimio namba 2720 lililopitishwa na Baraza la Usalama mwezi uliopita, ambalo linataka fursa isiyo na vikwazo ya kufikisha misaada ya kibinadamu kwa usalama, na kuweko na mazingira endelevu ya sitisho la mapigano. 

Ametoa wito kwa pande kinzani kwenye mzozo wa Gaza kutekeleza kikamilifu azimio la Baraza la Usalama lililopitishwa tarehe 12 mwezi Desemba, likifuatia kikao maalum cha dharura kilichoitishwa na Baraza hilo. 

Kuhusu ulinzi wa raia, Balozi Francis amesihi nchi zote wanachama “kuzingatia lengo la pamoja wakati wa mjadala wa leo.” 

Makamu wa Rais wa Baraza Kuu UN Cheikh Niang aongoza Kikao Maalum cha Dharura kuhusu hali katika Mashariki ya Kati.
Umoja wa Mataifa Naibu Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Balozi Cheikh Niang akiongoza kikao cha dharura cha Baraza Kuu la UN 09 Januari 2024

Mjadala unafuatia azimio la Baraza Kuu 

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio lenye lengo la kuchagiza ushirikiano zaidi na Baraza la Usalama, kufuatia uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine mwezi Februari mwaka 2022, hali ambayo ilichochea kuitishwa kwa mkutano pindi kura turufu inatumika kwenye Baraza la Usalama. 

Kura turufu hutumiwa na nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama ambao ni China, Ufaransa, Urusi, Uingereza na Marekani, na iwapo mmojawao akipiga kura ya Hapana, azimio linakuwa halijapita. 

Azimio la Baraza Kuu ambalo lilianzisha hoja ya kuchunguza matumizi ya kura turufu ndani ya Baraza la Usalama linamtaka Rais wa Baraza Kuu kuitisha mjadala rasmi ndani ya siku 10 za kazi ili nchi 193 wanachama wa Umoha huo wawe na fursa pana zaidi ya kujadili. 

Lengo la hatua hii ni kupatia fursa nchi wanachama kutoa mapendekezo ikiwemo matumizi ya nguvu za kijeshi ili kusongesha au kurejesha amani na usalama kwenye maeneo yenye mizozo. 

Na kama ilivyo kwa maazimio yote ya Baraza Kuu, yanakuwa na uzito kimaadili na kisiasa lakini hayana nguvu kisheria, tofauti na yale ya Baraza laUsalama. 

Mkutano wa leo Jumanne umekuja baada ya Marekani kupinga kwa kutumia kura yake turufu marekebisho ya rasimu ya azimio iliyowailishwa na Urusi tarehe 22 Desemba, baada ya kupitishwa kwa azimio la mwezi uliopita na Baraza hilo kuhusu Gaza.

Naibu Mwakilishi wa Kudumu Robert A. Wood wa Marekani akizungumza jukwaani wakati wa mkutano wa Baraza Kuu la UN jijini New York.
Umoja wa Mataifa Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Robert Wood akihutubia Baraza Kuu la UN.

Marekani imejizatiti kuona mateka wote wanarejea nyumbani

Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Robert Wood akizungumza kwenye mjadala uo amekaribisha kitendo cha Baraza la Usalama kupitisha azimio namba 2720 la mwaka 2023 tarehe 22 ya mwezi Desemba mwaka jana.

Ijapokuwa Marekani haikupiga kura, amesema ilishirikiana na mataifa mengine muhimu na ‘yenye nia njema’ kukamilisha azimio hilo thabiti. “Kazi hiyo inahusisha diplomasia ya moja kwa moja Marekani inashiriki ili kufikisha misaada zaidi ya kiutu Gaza na pia kusaidia mateka walioko Gaza warejee nyumbani.”

Bila kutaja Urusi, ambayo marekebisho yake yalichochea kura turufu ya Marekani inayojadili na Baraza Kuu hii leo, Balozi Woods amesema moja ya nchi wanachama ilisisitiza kuweka mawazo ambayo ‘yalijitenga na mazingira ya hali halisi.”

Amesema “ilikuwa inachukiza mno” kwamba nchi nyingi zilionekana kuacha kuzungumzia kadhia inayokumba mateka wanaoshikiliwa Gaza na wanamgambo wa kipalestina.”

Marekani imejizatiti kuwarejesha nyumbani mateka wote na “inaendelea na juhudi za kuona kunakuweko na sitisho lingine la mapigano. Aidha amesema kinachokosekana ni matakwa kwa Hamas kuweka silaha chini na kujisalimisha.

“Itakuwa vema iwapo kutakuweko na sauti thabiti ya kimataifa kwa viongozi wa Hamas kufanya kile kinachowezekana kumaliza mzozo ambao waliuanzisha wao tarehe 7 Oktoba 2023,” amesema Balozi Woods.

Mwakilishi wa Palestina Riyad Mansour akiinua bango lililoandikwa 'KOMESHA MOTO SASA!' wakati akihutubia Baraza Kuu la UN .
UN /Manuel Elias Mwangalizi wa Kudumu wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Riyad Mansour akihutubia Baraza Kuu la UN.

Wapalestina wanavumilia ‘ukatili wa kivita’

Mwangalizi wa Kudumu wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Riyad Mansour akizungumza kwenye mjadala huo amesema ‘ninasimama hapa nikiwakilisha watu ambao wanachinjwa, huku familia zao zikiteketezwa, wanawake na wanaume wanapigwa risasi mitaani, maelfu wametekwa nyara, wanateswa na kunyanyaswa, watoto wanauawa, wanakatwa viungo, wanaachwa yatima – wanahofia maisha.”

Amesema “hakuna watu” wanapaswa kuvumilia ghasia za aina hiyo na inapaswa kukoma.

Balozi Mansour amesema hakuna mtu anaweza kuelewa kuwa Baraza la Usalama linazuiwa kuitisha mara moja sitisho la mapigano, wakati nchi 153 kwenye Baraza Kuu zimetaka uwepo wa sitisho hilo, sambamba na Katibu Mkuu wa UN.

Amesema mashambulizi yanayofanywa na Israel hivi sasa ni saw ana “uhalifu wa kivita.”

“Unawezaje kuridhia kukataa ukatili na kutumia kura turufu wito wa kumaliza vita inayotekeleza usaidizi wao? Amehoji.

Palestina kwa muda mrefu imekuwa ikiunga mkono pendekezo la Ufaransa na Mexico “la kusitisha matumizi ya kura turufu iwapo kuna mauaji ya halaiki,  mauaji ya watu wengi, uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita kwa kiwango kikubwa.”

Ameesma mashambulizi dhidi ya wapalestina Gaza, “yamedhihirisha umuhimu wa pendekezo hilo. Kuunga mkono sitisho la mapigano ni maadili pekee, halali na msimami unaoonesha uwajibikaji.”

Katika siku hizi 90 tangu kuanza kwa mapigano, wapalestina 11 wameuawa ndani ya kila saa moja, wakiwemo wanawake 7 na watoto, Balozi Mansour amelieleza Baraza.

“Hii haihusu usalama wa Israel, hii ni uharibifu wa Palestina. Maslahi na malengo ya serikali ya Israel yenye msimamo mkali yako dhahiri na hayaendani na maslahi au malengo ya nchi yoyote inayounga mkono sheria ya kimataifa na amani’” amesisitiza Balozi Mansour.

Usalama katu hauwezi kupatikana kupitia vifo, uharibifu au kukandamizi wananchi wa Palestina, amesema.

Amesisitiza kuwa Palestina iko na itaendelea kuweko huku akitangaza: “Usiitishe amani huku unasambaza moto. Iwapo unataka amani, anza na sitisho la mapigano sasa.”

Balozi Gilad Erdan wa Israeli akizungumza kwenye jukwaa wakati wa mkutano wa Baraza Kuu UN jijini New York.
UN /Manuel Elias Mwakilishi wa Kudumu wa Israel kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Gilad Erdan akihuutubia Baraza Kuu

Hakuna madili, ‘ni upendeleo na unafiki: Israel

Mwakilishi wa Kudumu wa Israel kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Gilad Erdan, alipofika kwenye mimbari ya Baraza Kuu tayari kuhutubia akasema anashangaa ni kwa vipi mateka 136 wa Israel bado wanashikiliwa, akiwemo mtoto ambaye anakaribia kusherehekea mwaka mmoja wa kuzaliwa kwake  na nchi yoyote inataka sitisho la mapigano.

“Hivi chombo kimefilisikaje kimaadili,” amehoji balozi Erdan. “Kwa nini hakuna kelele kali ndani ya ukumbi huu zikitaka mtoto huyu arejeshwe nyumbani na wahusika Hamas wawajibishwe kwa ukatili wa kivita?”

Amesema “licha ya kumomonyoka kwa maadili ya UN,” raia wa Israel bado wamesalia kidete, wakiwa na imani, matumaini na azma isiyotetereka ya kujilinda wao wenyewe.

Amesema UN imegeuka “washirika wa magaidi” na kukosa uhalali wa kuendelea kuweko.

Badala ya kujikita kwenye kuwarejesha mateka nyumbani na kumaliza machungu  yao, UN “imevutiwa zaidi na ustawi wa watu wa Gaza ambao wanaweka madarakani Hamas na kuunga mkono ukatili wake,” amedai Balozi Erdan.

“Mnaapuuza waathirika wote wa Israel,” amesema.

Ameuliza ni kwa vipi Mkataba wa Kimataifa wa kuzuia Mauaji ya Halaiki unatumiwa kama silaha dhidi ya taifa la wayahudi, wakati kitu ambacho Hamas inataka ni kurejelea mauaji ya halaiki au Holocaust.

“Hakuna maadili hapa, ni upendelezo na unafiki,” amesema. Kwa kutaka sitisho la mapigano ni kupatia Hamas kibali cha kuendelea kutawala kwa vitisho.

Amesema kwa kuitisha sitisho la mapigano, Baraza linatuma ujumbe dhahiri kwa magaidi duniani kote. “UN inaashiria kwa magaidi kuwa ubakaji ni silaha ya vita na ni sahihi,” ameongeza Balozi Erdan.

Anna Evstigneeva akizungumza jukwaani wakati wa mkutano wa Baraza Kuu la UN .
UN /Manuel Elias Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Anna Evstigneeva, akihutubia Baraza Kuu.

Marekani inawajibika na maazimio yasiyo na mashiko: Urusi

Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Anna Evstigneeva, amesema Marekani imekuwa inakosea kwa kucheza mchezo usio wa kiaminifu kwa kulinda vitendo vya Israel huko Gaza pale ilipotumia kura turufu kwenye Baraza la Usalama tarehe 22 Desemba 2023.

Amesema kwa kutumia vitisho, Marekani imekuwa ikiipatia Israel leseni ya kuua wapalestina, “ikibariki kitendo kinachoendelea cha kutokomeza wagaza,” na ndio maana Urusi iliwasilisha marekebisho.

Lengo la turufu ya Marekani ilikuwa kupitisha nia ya kuipatia Israel utawala huru na “kwa makusudi kufifisha juhudi za kimataifa chini ya mwamvuli wa Umoja wa Mataifa  na kutekeleza maslahi yake ya kijiografia na kisiasa Mashariki ya Kati,” amesema Balozi Evstigneeva.

Amesema matokeo ya kusikitisha ya hatua hii ni kwamba kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita cha mashambulizi Gaza, Baraza limeweza kupitisha maazimio” yasiyo na mashiko.”

Urusi haikutumia kura turufu kwenye nyaraka zote mbili, badala ya kuzipiga kura ya Hapana, kwa kuzingatia maombi ya wawakilishi wa PAlestina na nchi za kiarabu.

Amesema ombi dhahiri kwa Baraza la Usalama ni sitisho kamilifu la mapigano na kwamba bila sitisho hilo, utekelezaji wa maamuzi ya Baraza kwa Gaza hautawezekana.

Kutazama mjadala wote bofya video hii hapa chini