Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wananchi wa Gaza 'hawana chaguo'

Wapalestina wanaendelea kuyahama makazi yao kutokana na mzozo unaoendelea.
© UNRWA/Ashraf Amra
Wapalestina wanaendelea kuyahama makazi yao kutokana na mzozo unaoendelea.

Wananchi wa Gaza 'hawana chaguo'

Amani na Usalama

Huko Gaza, ambapo shule mbili zinazosimamiwa na Umoja wa Mataifa zikiwa zimeshambuliwa moja kwa moja mwishoni mwa wiki huku kukiwa na mapigano makali, hali ya raia inaendelea kuwa mbaya huku mvua kubwa ikinyesha katika eneo hilo. 

Ujumbe wa shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA katika mtandao wa X leo Jumatatu, umeelezea hali katika makazi kama "isiyofaa kwa maisha". Ujumbe umesema kwamba watu wa Gaza hawana "chaguo", ukirejea maonyo ya mara kwa mara kutoka kwa wasaidizi wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa kwamba hakuna mahali ambapo ni salama kwa raia huko Gaza. 

Tangu mashambulizi ya kutisha ya Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba ambayo yaligharimu maisha ya watu 1,200 huku karibu watu 240 wakitekwa, mamia ya maelfu ya watu wa Gaza wamekimbia kusini, kufuatia agizo la kuhama lililotolewa na jeshi la Israeli. 

Msafara wa kushangaza

Picha za satelaiti za msafara zimeonesha msafara wa umati wa watu wakitembea katika mandhari ya majengo yaliyobomoka, huku picha zilizopigwa chini zikionesha familia zilizobeba mali zao wakitembea kwa miguu na nyingine imeonesha mwanamke akiwakokota watoto wawili kwenye viti vya gari nyuma yake. 

Jana Jumapili, Tom White, Mkurugenzi wa Masuala ya UNRWA, amesema maeneo 13 ya UNRWA ambako watu walikuwa "wakihifadhi chini ya bendera ya Umoja wa Mataifa" "yamepigwa moja kwa moja" tangu Oktoba 7, wakati "makazi mengine mengi" yalipata "uharibifu mkubwa" – mengi kati yao yakiwa kusini mwa Gaza, ambapo raia walikuwa wameambiwa kuondoka. 

Makumi ya watu wameuawa 

Bwana White anasema kuwa watu 73 wameuawa katika makazi ya UNRWA hadi sasa, "idadi kubwa yao katika eneo la kusini". 

"Ukweli ni kwamba watu wa Gaza hawana pa kwenda kwa usalama na wote wanakabiliwa na tishio la mapigano na hasa mashambulizi ya anga," afisa huyo wa UNRWA anasisitiza kwa masikitiko. 

Kulingana na shirika hilo la Umoja wa Mataifa, zaidi ya wakimbizi wa ndani 880,000 wametafuta hifadhi katika vituo 154 vya UNRWA katika majimbo yote matano ya Gaza. Kati ya watu milioni 2.3 wa Gaza, milioni 1.7 sasa wameyahama makazi yao. 

Hadi sasa, wafanyakazi 104 wa UNRWA wameuawa pamoja na watu wasiopungua 11,000 huko Gaza kulingana na mamlaka ya afya Gaza. 

"Nyumba zimeathiriwa kote katika Ukanda wa Gaza," Bwana White wa UNWRA na kwamba jambo kuu la kuzingatia ni, "Ikiwa watu wako kaskazini au kusini, wako salama?" 

Mafuta 

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric leo akizungumza na waandishi wa Habari amesema, “Wenzetu wa OCHA kuhusu hali ya Gaza wanatuambia kuwa takriban lita 69,000 za mafuta ziliingia Gaza kutoka Misri jana.” 

Mamlaka za Israel zimethibitisha kwamba zitaanza kuruhusu kuingia kwa kiasi cha kila siku cha takriban lita 70,000 za mafuta kutoka Misri, ambayo ingawa ni nzuri, inasalia chini ya mahitaji ya chini kabisa ya shughuli muhimu za kibinadamu. Mafuta yanapangwa kusambazwa na UNRWA.  

“UNRWA pia inatuambia kwamba pamoja na hayo, watasaidia usambazaji wa chakula na uendeshaji wa jenereta katika hospitali, vifaa vya maji na vyoo, makazi, na huduma nyingine muhimu.” Amesema Dujarric.  

Jana Nov 19, UNRWA na UNICEF walisambaza lita 19,500 za mafuta kwa vituo vya maji na usafi wa mazingira kusini mwa Wadi Gaza, na kuwawezesha kuendesha jenereta na kuanza tena kazi yao. Kiasi hicho cha mafuta kinatarajiwa kudumu kwa takriban masaa 24. 

UNRWA pia imeripoti kuwa idadi ya watu waliofariki katika shambulizi lililoipiga shule ya Al Fakhouri huko Jabalia tarehe 18 Novemba ni takriban watu 24, huku wengine wakijeruhiwa. Wakati wa tukio, kituo hicho kilikuwa kikiwahifadhi wakimbizi wa ndani wapatao 7,000 (IDPs). 

Katika taarifa yake ya jana Jumapili, Katibu Mkuu alisema ameshtushwa sana na shule mbili za UNRWA kupigwa chini ya saa 24 huko Gaza. Makumi ya watu na watoto waliuawa na kujeruhiwa walipokuwa wakitafuta usalama katika majengo ya Umoja wa Mataifa. 

Katibu Mkuu alisisitiza tena kwamba majengo ya Umoja wa Mataifa hayawezi kukiuka. Pia alisisitiza wito wake wa kusitisha mapigano mara moja.