Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hospitali Ukraine lazima zisalie kuwa mahala salama kwa watu wenye uhitaji: UN

Jengo lililoharibiwa huko Avdiivka, Donetsk, Ukraine. (Maktaba)
© UNICEF/Ashley Gilbertson
Jengo lililoharibiwa huko Avdiivka, Donetsk, Ukraine. (Maktaba)

Hospitali Ukraine lazima zisalie kuwa mahala salama kwa watu wenye uhitaji: UN

Amani na Usalama

Mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Ukraine Denis Brown amelaani vikali mapigano yaliyoua, kujeruhi rai ana kuharibu hospitali na miundombinu mingine ya raia katika eneo la Selydove mkoa wa Donetsk nchini Ukraine.

Katika taarifa yake iliyotolewa leo mjini Kyiv Brown amesema “Nimesikitishwa sana na kushtushwa na habari za asubuhi ya leo kutoka mji wa Selydove katika mkoa wa Donetsk, mashariki mwa Ukraine, ambapo shambulio lingine la usiku kwenye mji huu uliokumbwa na vita lilimekatili maisha ya raia zaidi na kuharibu hospitali, nyumba na miundombinu ya kiraia iliyo karibu.”

Ameongeza kuwa taarifa za majeruhi zilizoripotiwa ni za kutisha mwanamke mjamzito, mama na mtoto wake, mtoto wa miezi sita na raia wengine watu wazima na watoto wamepoteza maisha au kujeruhiwa katika shambulio hili la kutisha. 

Wagonjwa wamelazimika kuhamishwa

Brown amesema wasimamizi wa hospitali walilazimika kuwahamisha wagonjwa katikati ya usiku mara ya pili katika miezi michache tu, kwani hospitali hiyo hiyo ilipigwa makombora Novemba 2023.

Ameendelea kusema kwamba “Mashambulizi haya ya mara kwa mara yanayoathiri vituo muhimu vya huduma ya afya ni ukumbusho dhahiri wa athari mbaya ambayo vita ya Urusi dhidi ya Ukraine inaleta kwa raia, haswa wale wanaotafuta matibabu.”

Mwaka huu wa 2024 pekee, Shirika la Afya la umoja wa Mataifa Ulimwenguni WHO, limethibitisha mashambulizi 28 ya kushangaza yaliyoathiri wafanyikazi wa huduma za afya na wagonjwa, hospitali, magari ya kubeba wagonjwa na vifaa kote Ukraine.

Mratibu huyo amesisitiza kwamba “Mashambulizi dhidi ya huduma ya afya ni ukiukaji mkubwa wa sheria ya kimataifa za kibinadamu na ubinadamu na haikubaliki kabisa kwamba raia wanaotafuta matibabu, ambao tayari wanapambana na matokeo ya kimwili na ya kihisia ya ugonjwa au majeraha, wanapaswa pia kukabiliana na vurugu na uharibifu. Hospitali lazima zisalie kuwa kimbilio salama kwa watu wenye uhitaji.”