Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uamuzi wa Urusi kuhusu Donetsk na Luhansk unatia hofu kubwa:Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (kwenye mimbali0 akiwaeleza waandishi wa habari kuhusu Ukraine. (Picha ya Maktaba)
UN Photo/Manuel Elías
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (kwenye mimbali0 akiwaeleza waandishi wa habari kuhusu Ukraine. (Picha ya Maktaba)

Uamuzi wa Urusi kuhusu Donetsk na Luhansk unatia hofu kubwa:Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema ana wasiwasi mkubwa na uamuzi uliofanywa na serikali ya shirikisho ya Urusi kuhusiana na hali ya maeneo ya Ukraine yaliyojitenga ya jimbo la Donetsk na Luhansk.  

Kupitia taarifa iliyotolewa leo jijini New York Marekani na msemaji wake, Antonio Guterres ametoa wito wa kusuluhishwa kwa amani mzozo wa mashariki mwa Ukraine, kwa mujibu wa Mikataba ya Minsk, kama ilivyoidhinishwa na Baraza la Usalama katika azimio  namba 2202 (2015). 

Katibu Mkuu amesema anauchukulia uamuzi wa shirikisho la Urusi kuwa ni ukiukaji wa uadilifu wa eneo na uhuru wa Ukraine na hauendani na kanuni za Mkataba wa Umoja wa Mataifa. 

Umoja wa Mataifa, kwa mujibu wa maazimio husika ya Baraza Kuu, bado unaunga mkono kikamilifu uhuru, na uadilifu wa eneo la Ukraine, ndani ya mipaka yake inayotambulika kimataifa. 

Taarifa hiyo ya Katibu Mkuu imetoa wito kwa pande zote husika katika mzozo wa Ukraine kuelekeza nguvu zao katika kuhakikisha mapigano yanakomeshwa mara moja, kuhakikisha ulinzi wa raia na miundombinu ya kiraia, kuzuia vitendo na matamshi yoyote ambayo yanaweza kuzidisha hali ya hatari ndani na karibu na Ukraine na kuweka kipaumbele kwenye diplomasia katika kushughulikia maswala yote kwa njia ya amani.