Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuhusu Ukraine: Ni wakati muafaka wa kurudi kwenye njia ya mazungumzo - Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya sasa ya Ukraine. (22 Februrai 2022)
UN Photo/Mark Garten)
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya sasa ya Ukraine. (22 Februrai 2022)

Kuhusu Ukraine: Ni wakati muafaka wa kurudi kwenye njia ya mazungumzo - Guterres

Amani na Usalama

Niseme wazi: uamuzi wa Urusi kutambua kile kinachoitwa "uhuru" wa maeneo fulani ya mikoa ya Donetsk na Luhansk ni ukiukaji wa uadilifu wa eneo na uhuru wa Ukraine. Amesema Katibu Mkuu Antpnio Guterres jioni hii ya Jumanne wakati akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.  

Bwana Guterres ambaye amelazimika kukatisha “ziara ya nje ya nchi  ikiwa ni pamoja na mkutano muhimu sana wa viongozi wa Afrika ili kurejea makao makuu ya Umoja wa Mataif,.” amesema, “ulimwengu wetu unakabiliwa na mzozo mkubwa zaidi wa amani na usalama duniani katika miaka ya hivi karibuni  bila shaka katika kipindi changu kama Katibu Mkuu.” 

Aidha Katubu Mkuu Guterres ameeleza kuwa ulimwengu unakabiliwa na wakati ambao alitumaini kuwa hautakuja. Amesema amesikitishwa sana na matukio ya hivi punde kuhusu Ukraine ikiwa ni pamoja na ripoti za kuongezeka kwa ukiukaji wa usitishaji mapigano katika njia zote za mawasiliano na hatari halisi ya kuongezeka zaidi. 

“Ninajali sana usalama na ustawi wa wale wote ambao tayari wameteseka kutokana na vifo vingi, uharibifu na kufurushwa. Hatua hiyo ya upande mmoja inakinzana moja kwa moja na kanuni za Mkataba wa Umoja wa Mataifa na haiendani na kile kinachoitwa Tamko la Mahusiano ya Kirafiki la Baraza Kuu ambalo Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ICJ imetaja mara kwa mara kuwa linawakilisha sheria za kimataifa.” Amesema Guterres. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameendelea kueleza kuwa tukio hili la hivi sasa ni pigo la kifo kwa Makubaliano ya Minsk yaliyoidhinishwa na Baraza la Usalama na kwamba kanuni za mkataba wa Umoja wa Mataifa si orodha ya vyakula kusema mtu anaweza kuchagua kimoja bali nchi wanachama zimezikubali zote na lazima zitumike zote. 

Pia Bwana Guterres ameeleza kuwa ana wasiwasi kuhusu upotoshaji wa dhana ya ulinzi wa amani na hivyo anawasihi wote wajiepushe na vitendo na kauli ambazo zinaweza kuipeleka hali hii hatari kwenye ukingo. 

“Uongezaji wowote wa ziada wa kijeshi wa Urusi nchini Ukraine utazidisha mvutano. Ni wakati muafaka wa kurudi kwenye njia ya mazungumzo.” Ameeleza Bwana Guterres. 

Zaidi ameeleza kuwa ni lazima kukutana na kukabiliana na changamoto hii pamoja kwa ajili ya amani, na kuokoa watu wa Ukraine kuondokana na janga la vita na hapo akatoa ahadi kuwa yeye pamoja na ofisi yake wanajitolea, “kikamilifu kwa jitihada zote za kutatua mgogoro huu bila umwagaji zaidi wa damu. Ninarudia: Ofisi zangu nzuri ziko na hatutalegea katika kutafuta suluhu ya amani. Umoja wa Mataifa na mfumo mzima wa kimataifa unajaribiwa. Ni lazima tushinde jaribio hili.”