Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ninarudia ombi langu la jana usiku kwa Rais Putin : Rudisha wanajeshi Urusi

Katibu Mkuu António Guterres (kushoto) akitoa maelezo kwa waandishi wa habari kuhusu hali ilivyo sasa nchini Ukraine
UN Photo/Mark Garten)
Katibu Mkuu António Guterres (kushoto) akitoa maelezo kwa waandishi wa habari kuhusu hali ilivyo sasa nchini Ukraine

Ninarudia ombi langu la jana usiku kwa Rais Putin : Rudisha wanajeshi Urusi

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amerejelea wito wake kwa Rais Viladmir Putin wa Urusi kurejesha majeshi yake nchini Urusi. 

Bwana Guterres kupitia katika mkutano wake na waandishi wa habari ameeleza hali ilivyo akisema, “tunaona operesheni za kijeshi za Urusi ndani ya eneo huru la Ukraine kwa kiwango ambacho Ulaya haijaona kwa miongo kadhaa. Siku baada ya siku, nimekuwa wazi kwamba hatua hizo za upande mmoja zinapingana moja kwa moja na Mkataba wa Umoja wa Mataifa. ” 

Mkataba uko wazi ameeleza Guterres : "Wanachama wote wataepuka katika mahusiano yao ya kimataifa kuwa katika tishio au matumizi ya nguvu dhidi ya heshima ya eneo au uhuru wa kisiasa wa nchi yoyote, au kwa njia nyingine yoyote isiyoendana na Malengo ya Umoja wa Mataifa." 

Katibu Mkuu Guterres ameendelea kufafanua kuwa utumiaji wa mabavu kwa nchi moja dhidi ya nchi nyingine ni kukataa kanuni ambazo kila nchi imejitolea kuzisimamia na kwamba hii inatokea sasa katika mashambulizi ya sasa ya kijeshi na kwa hivyo, “ni makosa. Ni kinyume na Mkataba. Haikubaliki. Lakini haiwezi kurejeshwa nyuma.” 

“Ninarudia ombi langu la jana usiku kwa Rais Putin: Acha operesheni ya kijeshi. Rudisha wanajeshi nchini Urusi. Tunaijua hali ya vita.” Amesisitiza Bwana Guterres. 

Umoja wa Mataifa unaingilia kati kusaidia watu 

Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameeleza kwamba huku vifo vikiongezeka, ulimwengu unaona taswira za hofu, huzuni na hofu katika kila kona ya Ukraine, “kila siku watu wasio na hatia - daima hulipa gharama ya juu zaidi. Ndiyo maana Umoja wa Mataifa unaongeza shughuli zetu za kibinadamu ndani na karibu na Ukraine.” 

Na kwa msingi huo, Bwana Guterres ametangaza kwamba Umoja wa Mataifa unatenga mara moja dola milioni 20 kutoka kwenye Mfuko Mkuu wa Kukabiliana na Dharura ili kukidhi mahitaji ya dharura. 

Aidha ameeleza kuwa Umoja wa Mataifa na wadau wake wa kibinadamu wanajitolea kubaki na kusaidia watu nchini Ukraine wakati wao wa mahitaji. 

“Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wanafanya kazi katika pande zote za mstari wa makabiliano, kila mara wakiongozwa na kanuni za kibinadamu za kutoegemea upande wowote, kutopendelea, ubinadamu na huru. Tunatoa msaada wa kibinadamu unaookoa maisha kwa watu wanaohitaji, bila kujali ni nani au wapi.” Amesema.  

Guterres amesisitiza kuwa ulinzi wa raia lazima uwe kipaumbele namba moja. Sheria ya kimataifa ya haki za kibinadamu na haki za binadamu lazima izingatiwe.  

Kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa amehitimisha kwa kueleza kuwa maamuzi ya siku zijazo yataunda ulimwengu wetu na kuathiri moja kwa moja maisha ya mamilioni kwa mamilioni ya watu. “Sambamba na Mkataba, bado hatujachelewa kuokoa kizazi hiki kutokana na janga la vita. Tunahitaji amani.” 

TAGS: Ukraine, Urusi, Russia, Viladmir Putin, Luhansk, Donetsk