Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC: Mapigano kati ya FARDC na M23 yafurusha maelfu Kivu Kaskazini

Moja ya maeneo mengi ya wakimbizi wa ndani ambayo yamechipuka huko Kivu Kaskazini ambapo watu milioni 1.2 wamelazimika kukimbia makazi yao. (Maktaba)
© UNHCR/Blaise Sanyila
Moja ya maeneo mengi ya wakimbizi wa ndani ambayo yamechipuka huko Kivu Kaskazini ambapo watu milioni 1.2 wamelazimika kukimbia makazi yao. (Maktaba)

DRC: Mapigano kati ya FARDC na M23 yafurusha maelfu Kivu Kaskazini

Amani na Usalama

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanyotoa huduma za kibinadamu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, yana wasiwasi mkubwa kuhusu kuzidi kuzorota kwa hali ya kibinadamu nchini humo, hususan kwenye mji wa Masisi, jimboni Kivu Kaskazini mashariki mwa taifa hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani hii leo, msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric amesema kuzorota kwa hali hiyo ya kiutu inatokana na mapigano makali yaliyodumu kwa wiki mbili sasa yanayoendelea hivi sasa kati ya jeshi la serikali ya DRC, FARDC na waasi wa kikundi cha M23.

Hadi sasa watu 130,000 wamefurushwa makwao kutoka maeneo mbali mbali ya mji wa Masisi.

“Hali hii ya sasa inachangia katika hali mbaya ya kiutu ambayo tayari imekumba jimbo hilo la Kivu Kaskazini,” amesema Bwana Dujarric.

Ameongeza kuwa watu waliofurushwa makwao wakiwemo wanawake , wanaume na watoto 26,000 hivi sasa wanaishi kwenye mji wa Sake, Kivu Kaskazini na wengine 24,000 walioko mji wa Minova, jimboni Kivu Kusini kwa sasa hawana chakula, maji safi na salama, huduma za afya na malazi.

Usafiri wa barabara kati ya Kivu Kusini na Kivu Kaskazini umeathirika

Mapigano hayo yameathiri pia usafiri wa Barabara kati ya miji ya Sake na Bweremana, ambayo ni Barabara kuu inayounganisha miji ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.

“Hii inahatarisha mji wa Goma kutengwa, mji ambao ni makazi ya watu milioni 2 na kwa sasa unahifadhi wakimbizi 500,000,”  amesema Dujarric akiongeza kuwa hali hiyo itaathiri pia usalama na shughuli za kiuchumi kwenye mji wa Goma.

Kuzidi kudorora kwa usalama mjini Masisi kumezuia watu 630,000 ambao awali walikuwa wamefurushwa makwao washindwe kupata huduma za afya, kama vile misaada ya matibabu kwa wale waliojeruhiwa kwenye mapigano.

Bwana Dujarric amesema uwezekano wa mapigano zaidi Goma ni mkubwa.

“Tunaendelea kusihi fursa ya kufikisha misaada kwa watu wanaohitaji, na pia tunasihi pande zote kwenye mapigano ziheshimu sheria ya kimataifa ya kibinadamu na zichukue hatua thabiti kulinda raia.” Amesema.

Lacroix ahitimisha ziara DRC

Wakati huo huo, Bwana Dujarric amesema kuwa Jean-Pierre Lacroix, ambaye ni Mkuu wa Operesheni za ulinzi wa amani kwenye Umoja wa Mataifa ametamatisha ziara yake nchini DRC akitoa wito kwa kikundi cha M23 kiache mara moja mashambulizi yake huko Mashariki mwa nchi na kiheshimu mpango wa amani wa Luanda.

Ameelezea mshikamano wake na raia walioathiriwa na mapigano na kusisitiza azma ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC ya kutekeleza wajibu wake wa kulinda raia.

Akiwa mji mkuu Kinshasa, siku ya Jumanne, Bwana Lacroix alikuwa na mazungumzo na Rais Félix Tshisekedi ambapo walijadili uimarishaji wa uwepo na uwezo wa jeshi la ulinzi na usalama la DRC huko Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.

Kama tulivyosema awalim walinda amani wa Umoja wa Mataifa kwenye majimbo hayo matatu wanaanza kuondoka kama sehemu ya mpango wa MONUSCO kuondoka taifa hilo la Maziwa Makuu,”  amesema Bwana Dujarric.

MONUSCO ambao ni ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kulinda amani DRC, unaondoka nchini humo kufuatia ombi la serikali, ombi ambalo liliridhiwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.