Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC: Watu 450,000 wafurushwa Kivu Kaskazini, UNHCR na UNICEF zatiwa hofu

Watu ambao wamekimbia mapigano na ghasia huko Kivu Kaskazini wanakimbilia Rusayo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
© UNHCR/Blaise Sanyila
Watu ambao wamekimbia mapigano na ghasia huko Kivu Kaskazini wanakimbilia Rusayo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

DRC: Watu 450,000 wafurushwa Kivu Kaskazini, UNHCR na UNICEF zatiwa hofu

Wahamiaji na Wakimbizi

Zaidi ya watu 450, 000  huko Rutshuru na Masisi jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC wamefurushwa makwao katika wiki 6 zilizopita kufuatia mapigano yanayozidi kushamiri kati ya jeshi la serikali na makundi yaliyojihami.

Hali hii imetia hofu mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na la kuhudumia watoto, UNICEF.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi kwa njia ya video kutoka Kinshasa, mji mkuu wa DRC, Mwakilishi wa UNHCR nchini humo Angele Dikongue-Atangana, amesema makali ya mapigano hayo yanachochewa zaidi na ufinyu wa misaada ya kibinadamu kwa wahitaji, hasa kutokana na kuweko kwa vizuizi kwenye barabara kuu.

Wakiwa wamekatiliwa mbali na misaada muhimu ya kibinadamu, takriban watu 200,000 waliokimbia makazi yao kwa sasa wamekwama.

“Cha kusikitisha ni kwamba, watu zaidi ya 100,000 wanatarajiwa kutofikiwa na misaada iwapo mwelekeo wa sasa wa migogoro utaendelea,” amesema Bi. Dikongue-Atangana.

Naye Grant Leaity, Mwakilishi wa UNICEF nchini DRC akizungumza pia kutokea Kinshasa, amesema kukithiri kwa ukatili kunaleta athari mbaya kwa maisha ya watoto ambao wanakabiliwa na idadi kubwa ya ukiukwaji mkubwa wa haki zao. 

Visa vya ukiukaji wa haki dhidi ya watoto kati ya Julai na Septemba mwaka huu wa 2023, vimeongezeka kwa asilimia 130 na kufikia 2018 huku matukio mengine yakiripotiwa katika nusu ya kwanza ya mwaka.

Bwana Leaity amesema watoto wanazidi kukabiliwa na hatari ya kutumikishwa vitani na makundi yenye silaha, huku kukiwa na kesi zaidi ya 450 zilizothibitishwa kuanzia Julai hadi Septemba, ongezeko la asilimia 50 ikilinganishwa na nusu ya kwanza ya mwaka. 

Ametamatisha kwa kusema UNHCR na UNICEF wanatoa wito kwa dharura kwa wahusika wote mashariki mwa DRC kukomesha ghasia ambazo zinaathiri zaidi raia na kwamba  tunasimama kwa umoja katika dhamira yetu ya kupunguza mateso ya wale walioathiriwa na mgogoro, lakini jumuiya ya kimataifa inapaswa kuchukua hatua haraka na kwa ukarimu ili kuhakikisha kuwa rasilimali za kutosha zinakusanywa.”

Kwa mujibu wa Mwakilishi huyo wa UNICEF, uchangiaji wa ombi la usaidizi DRC bado unasuasua.

Kwa mwaka huu wa 2023, Mpango wa Kukabiliana na Kibinadamu ulioratibiwa, unaojumuisha mahitaji ya kifedha ya UNHCR na UNICEF, ni dola bilioni 2.3, lakini hadi leo, umeafadhiliwa kwa asilimia 37 pekee.