Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya watu 800 wameuawa Mashariki mwa DRC kati ya Februari na Juni 2022- UNHCR

Angela N'Habimana mwenye umri wa miaka 67 akiwa na mjukuu wake aitwaye Réponse kwenye kituo cha kijamii cha Kiwanja katika eneo la Rutshuru jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC baada ya kukimbia mashambulizi kwenye makazi yao.
© UNHCR/Sanne Biesmans
Angela N'Habimana mwenye umri wa miaka 67 akiwa na mjukuu wake aitwaye Réponse kwenye kituo cha kijamii cha Kiwanja katika eneo la Rutshuru jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC baada ya kukimbia mashambulizi kwenye makazi yao.

Zaidi ya watu 800 wameuawa Mashariki mwa DRC kati ya Februari na Juni 2022- UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Hali ya usalama huko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC inaendelea kuzorota ambapo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, linasema mauaji na uporaji wa mali za raia vinaendelea na kwamba kati ya mwezi Februari na mwezi uliopita wa Juni zaidi ya watu 800 wameuawa katika mashambulizi kutoka vikundi vilivyojihami.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo ,msemaji wa UNHCR Matthew Saltmarch amesema, “tunasikitishwa na tuna wasiwasi mkubwa kutokana na idadi kubwa ya vifo na machungu ya raia ikiwemo raia kulazimishwa kukimbia makwao kutokana na mashambulizi ya kikatili kwenye majimbo ya Mashariki mwa DRC.”

Hali  hii haipaswi kuendelea kupuuzwa

Majimbo hayo ni Kivu Kusini na Ituri ambapo akifafanua zaidi amesema kuwa hali hiyo isiyovumilika inaendelea kupanuka na katu haipaswi kuendelea kupuuzwa.

Akichambua takwimu amesema, “mwezi huu pekee mashambulizi ya mfululizo kutoka waasi jimboni Ituri yamesababisha vifo vya watu 11 na nyumba 250 kuporwa mali na kisha kuteketezwa moto. Na Kati ya Februari na Juni mwaka huu UNHCR na wadau wamerekodi zaidi ya vifo vya watu 800 kutokana na mashambulizi ya kutumia silaha na mapanga kwenye jamii mbalimbali jimboni Ituri.”

Mabinti wakiwa wametoka kuteka maji mjini Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Congo
© UNICEF/Scott Moncrieff
Mabinti wakiwa wametoka kuteka maji mjini Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Congo

Cha kusikitisha ni kwamba takribani ya watu 715 kati ya hao waliokufa walikuwa wamesaka hifadih kwenye maeneo ya wakimbizi wa ndani au waliuawa wakati wanarejea nyumbani baada ya kukimbia ghasia.

Zaidi ya watu 20,700 wamefurushwa  makwao kutokana na mashambulizi ambayo pia yamechochea uhaba wa chakula jimboni Ituri, jimbo ambalo lina rutuba kubwa na maendeleo yamedumaa kutokana na miongo kadhaa ya mapigano ya kikabila na hivyo kukosesha familia mbinu za kipato.

Makazi ya Kashuga yalisambaratishwa na waasi

Jimboni Kivu Kaskazini, makazi ya wakimbizi wa ndani ya Kashuga yaliyoko mjini Masisi yalisambaratishwa mwezi Juni baada ya watu waliojihami kuvama na kuua watu wanane na wengine saba walijeruhiwa.

Bwana Saltmarsh amesema katika wiki za karibuni mapigano kati ye jeshi la DRC, (FARDC) na waasi wa kikundi cha M23 jimboni Kivu Kaskazini yamefurusha zaidi ya watu 160,000 kwenye maeneo ya Rutshuru na Nyiragongo.

“Kupangwa upya kwa jeshi la serikali kwenye mzozo huu kumejenga ombo la mamlaka na utete wa usalama kwenye majimbo ya Ituri na Kivu Kaskazini.  Mashambulizi yaliyoratibiwa vyema na vikundi vya wanamgambo vilivyojihami vinanyanyasa raia kila uchao majimbo ya mashariki,” amesisitiza msemaji huyo.

Familia za wananchi wa Kongo zikipata hifadhi katika uwanja wa kanisa katoliki huko Drodro, Ituri.
© UNHCR/John Wessels
Familia za wananchi wa Kongo zikipata hifadhi katika uwanja wa kanisa katoliki huko Drodro, Ituri.

Mashambulizi yanakwamisha shughuli za UNHCR

Amefafanua kuwa mashambulizi ya kila  uchao  yanakwamisha operesheni za UNHCR kufikisha misaada kwa jamii zilizo hatarini wakati huu ambapo ombi la shirika hilo la usaidizi kwa DRC limefadhiliwa kwa asilimia 19 pekee kati ya dola milioni 225 zinazohitajika.

“Tunatoa wito kwa wadau wote kukomesha ghasia hizi zisizo na maana ambazo zinalazimu watu kukimbia makwao. Tunatoa wito wa kuheshimiwa kwa sheria za kimataifa za kibinadamu na za usaidizi wa kibinadamu,” amesisitiza.

Zaidi ya watu milioni 5.6 nchini DRC ni wakimbizi wa ndani na hivyo kufanya idadi kubwa zaidi ya wakimbizi wa ndani siyo tu barani Afrika bali pia duniani.