Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Gaza: UN yaunda jopo huru la uchunguzi wa uwezo wa UNRWA

Ofisi ya UNRWA huko Gaza.
Ziad Abu Khousa
Ofisi ya UNRWA huko Gaza.

Gaza: UN yaunda jopo huru la uchunguzi wa uwezo wa UNRWA

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa umeunda Jopo Huru litakalotathmini iwapo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina, UNRWA linafanya kila liwezalo kuhakikisha haliegemei upande wowote na linachukua hatua haraka pindi ukiukwaji mkubwa wa majukumu yake unapotokea.

Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres ameunda jopo hilo kwa mashauriano na Kamishna Mkuu wa UNRWA Philippe Lazzarini, na litaongozwa na Catherine Colonna, Waziri zamani wa Mambo ya Nje wa UFaransa.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatatu Februari 5, na Msemaji wa Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani inasema Bi. Colonna atashirikiana na mashirika matatu ya utafiti ambayo ni Taasisi ya Raoul Wallenberg ya Sweden, Taasisi ya Chr. Michelsen ya Norway na Taasisi ya Haki za Binadamu ya Denmark.

Jopo hilo litaanza kazi tarehe 14 mwezi huu wa Februari na linatarajiwa kuwasilisha ripoti ya awali kwa Katibu Mkuu Guterres mwisho mwa mwezi Machi, 2024, na ripoti ya mwisho ikitarajiwa kukamilika ifikapo mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka huu, ripoti ambayo itawekwa wazi kwa umma.

Tathmini hii inafuatia ombi la Kamishna Mkuu Lazzarini alilotoa mapema mwaka huu.

Hadidu Rejea za Jopo Huru

Mosi: Kuainisha mifumo na kanuni ambazo UNRWA inatumia hivi sasa katika kuepusha upendeleo na kuchukua hatua haraka pindi kunaibuka tuhuma au taarifa zinazodokeza kukiukwa kwa kanuni. 

Pili: Kujiridisha ni kwa vipi mifumo na kanuni hizo zinatekelezwa au hazitekelezwi na iwapo kila juhudi zilifanyika kuzitumia kwa ukamilifu, kwa kuzingatia operesheni mahususi, mazingira ya kisiasa na kiusalama ambamo UNRWA inafanya kazi.

Tatu: Kutathmini utoshelevu wa mifumo na kanuni hizo na iwapo zinakidhi mahitaji na malengo, ikiwemo uhusiano wake na udhibiti wa hatari na kuzingatia operesheni mahususi, mazingira ya kisiasa na kiusalama ambamo UNRWA inafanya kazi.

Nne : Kupendekeza uboreshaji na uimarishaji, iwapo inahitajika, wa mifumo na kanuni zilizoko au kuundwa kwa mifumo au kanuni mbadala au mpya ambazo zitafaa malengo ya UNRWA kwa kuzingatia operesheni mahususi, mazingira ya kisiasa na kiusalama ambamo UNRWA inafanya kazi.

Jopo litafanya kazi sambamba na uchunguzi unaoendelea

Jopo hili huru litafanya kazi sambamba na uchunguzi unaofanwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uchunguzi, OIOS ya tuhuma dhidi ya wafanyakazi 12 wa UNRWA kudaiwa kuhusika na mashambulizi ya tarehe 7 Oktoba 2023. Umoja wa Mataifa unasema kuwa ushirikiano wa Israel ambayo ndio ilitoa madai hayo, ni muhimu ili kufanikisha uchunguzi huu.

Katibu Mkuu Guterres anasema “madai hayo yanakuja wakati UNRWA, shirika kubwa zaidi la Umoja wa Mataifa kwenye Mashariki ya Kati, linafanya kazi katika mazingira magumu kusambaza misaada ya kuokoa maisha kwa watu milioni 2 walioko Gaza, watu ambao wanategemea msaada kwa uhai wao katika moja ya operesheni kubwa zaidi za kiutu duniani.