Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

GAZA: Msafara wa vyakula washambuliwa, wapalestina 234 wauawa mwishoni mwa wiki

Misafara ya chakula iliyokuwa ikisafiri kuelekea Kaskazini mwa Gaza imeshambulia na mikombora.
© UNRWA
Misafara ya chakula iliyokuwa ikisafiri kuelekea Kaskazini mwa Gaza imeshambulia na mikombora.

GAZA: Msafara wa vyakula washambuliwa, wapalestina 234 wauawa mwishoni mwa wiki

Amani na Usalama

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayotoa misaada ya kiutu huko Gaza, Mashariki ya Kati, yameripoti kuwa  kuwa msafara wa malori yaliyokuwa yamebeba vyakula umeshambuliwa kwa kombora leo baada ya mwisho wa wiki uliogubikwa na uhasama na mapigano yaliyosababisha kuuawa kwa wapalestina 234, na hivyo kuzidisha mvutano zaidi kwenye ukanda huo.

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayotoa misaada ya kiutu huko Gaza, Mashariki ya Kati, yameripoti kuwa  kuwa msafara wa malori yaliyokuwa yamebeba vyakula umeshambuliwa kwa kombora leo baada ya mwisho wa wiki uliogubikwa na uhasama na mapigano yaliyosababisha kuuawa kwa wapalestina 234, na hivyo kuzidisha mvutano zaidi kwenye ukanda huo.

Ripoti za kushambuliwa kwa msafara huo zimetolewa na Tom White, Mkurugenzi wa Masuala katika Shirik ala Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina, UNRWA huko Gaza, ambaye kupitia ukurasa wake kwenye mtandao wa X, zamani Twitter, ameambatanisha picha mbili, zikionesha jinsi tela la lori,  lililosheheni vyakula likiwa limeshambuliwa na kitambaa cha hema kilichotumika kulifunika tela hilo kikiwa kimeraruka.

Amesema lori hilo lenye tela lilikuwa linasubiri kuingia Kaskazini mwa Gaza lilipopigwa kwa kombora la Israel kutoka majini.

“Tunashukuru hakuna mtu yeyote aliyejeruhiwa,” amesema Bwana White.

Kwenye picha hizo, maboksi kadhaa yenye misaada yameonekana kusambaa barabarani, lakini haikufahamika haraka kilichomo kwenye maboksi hayo.

Lori lililokuwa limesheheni unga limewasili kaskazini mwa Gaza.
© UNRWA
Lori lililokuwa limesheheni unga limewasili kaskazini mwa Gaza.

WFP nayo yahaha kuingia Gaza Kaskazini, vizuizi kila kona

Harakati za UNRWA kufikia eneo la kaskazini mwa Gaza zimekuja baada ya shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula, WFP kuripoti Ijumaa ya kwamba kwa mara ya tatu limeshindwa kufika kaskazini mwa Gaza.

Mkurugenzi wa WFP eneo la Palestina Matthew Hollingworth amesema waliweza kufikisha misafara minne tu mwezi Januari, sawa na malori 35 yenye shehena kwa ajili ya watu 130,000.

Afisa huyo wa WFP anasema chakula hicho hakitoshelezi kuepusha baa la njaa Gaza, kwani kiwango cha njaa kinazidi kuongezeka Gaza.

Ametumia ukurasa wake kwenye mtandao wa X kuonesha jinsi ilivyo vigumu kwa misafara ya misaada kuingia na kupita eneo lililozingirwa la Gaza baada ya takribani miezi minne ya mashambulizi yasiyokoma kutoka Israel.

Anasema, “kuna uharibifu kila mahali, vifusi, Barabara zimefungwa na vile vile kuna mapigano yanaendelea kwenye maeneo kadhaa ya ukanda huu. Inachukua muda kuratibu, kupita kwenye vizuizi.”

Hadi leo hii, WFP imeshafikishia watu wapatao milioni 1.4 migao ya dharura ya misaada ikiwemo vyakula vya kwenye makopo, unga wa ngano na vyakula vya moto, ingawa bado misaada inahitajika kwa kiasi kikubwa.

Kuna uhaba wa kila kitu

Hali ya changamoto ya kufikisha misaada inaripotiwa wakati UNRWA ikisema kuwa takribani asilimia 75 ya wakazi milioni 2.3 Gaza wamefurushwa makwao tangu Oktoba 7, 2023.

Zaidi ya nusu ya hao waliofurushwa ni watoto ambao wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, maji ,makazi na dawa, limeonya shirika hilo la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina.

UNRWA imeongeza kuwa mapigano makali yanayoendelea kwenye mji wa Khan Younis yanazidi kufurusha watu kuelekea mji wa kusini mwa Rafah ambao tayari “umejaa pomoni.”

Watu wengi huko Rafah wanaishi kwenye makazi ya muda, mahema au maeneo ya wazi.

Kwa mujibu wa ripoti za hivi karibuni kutoka Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA, majengo ya makazi huko Gaza yameendelea kushambuliwa na kuharibiwa na mashambulizi kutoka jeshi la Israel.

Makazi hayo yako kwenye maeneo ya kusini ,mashariki na kati ya mji wa Khan Younis, halikadhalika kitongoji cha Al Sabra cha jiji la Gaza. Hata hivyo OCHA imesema hakuna ripoti za vifo kwenye mashambulizi hayo ya karibuni.

Chakula kinagawiwa kwa Wapalestina waliokata tamaa.
© UNRWA
Chakula kinagawiwa kwa Wapalestina waliokata tamaa.

Wapinga vita

Wakati huo huo, takribani maafisa 800 wa serikali za mataifa ya magharibi mwishoni mwa wiki wamechapisha barua ya wazi kupinga hatua za nchi zao kuunga mkono vita inayoendelea Gaza, wakielezea kuwa ni “moja ya janga baya zaidi la kibinadamu kwenye karne hii.”

Maafisa hao waliotia saini barua hiyo yaaminika ni watumishi wa ngazi ya juu serikalini na wanadiplomasia kutoka Marekani na 141 kutoka nchi za Ulaya zikiwemo UFaransa, Ujerumani, Uingereza na Uswisi.

Wamepinga kuwa serikali zao zimeunga mkono Israel “bila mazingira halisi au uwajibikaji,” na hivyo kusababisha vifo vya makumi ya maelfu ya watu ambavyo vingaliweza kuzuilika,” na “zuio la makusudi la misaada ambalo limeacha maelfu ya raia katika hatari ya njaa na kufa taratibu.”

Hofu yazidi kuongezeka

Taarifa za chapisho la barua hiyo zinakuja, wakati mvutano wa kikanda unazidi kuongezeka kwani Marekani na Uingereza zinashambulia wanamgambo wanaounga mkono Iran huko Iraq na Syria kuanzia Ijumaa iliyopita baada ya wanajeshi watatu wa Marekani kuuawa kwenye shambulio dhidi ya kituo cha kijeshi cha Marekani huko Jordan.

Na huku kukiwa na wito wa sitisho la mapigano Gaza na kuachiliwa huru kwa mateka, hofu inasalia kubwa ya kwamba kinachoendelea kinaweza kuchochea mambo mengine huko bahari ya Sham ambako wapiganaji wa kihouthi wamekuwa wakilenga meli zenye uhusiano na Israel.

Kwenye mpaka wa Israel na Lebanon, mashambulizi na wanamgambo wa Hezbollah yameongeza shaka juu ya utulivu wa kikanda.

Takwimu mpya za vifo kutokana na vita hiyo iliyochochewa na shambulizi la Hamas dhidi ya Israel Oktoba 7, 2023 na kusababisha waisrael 1,200 kuuawa na wengine 250 kutekwa nyara, zinaonesha wapalestina 27,365 wameuwa Gaza na 66,630 wamejeruhiwa, kwa mujibu wa mamlaka za afya Gaza.

OCHA nayo imeripoti kuwa askari 223 wa Israel wameuawa katika mapigano ya ardhini Gaza na wengine 1,296 wameruhiwa, wakinukuu jeshi la Israel.