Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

GAZA: Ibara ya 99 yatumika; Azimio laandaliwa, Marekani yatumia turufu yake kupinga

Taswira ya chumba cha Baraza la Usalama la UN wakati wajumbe walipokutana 08 Desemba 2023 kwa kikao cha Mashariki ya Kati hususan suala la Palestina kufuatia Katibu Mkuu kutumia Ibara ya 99 ya Chata kuitisha kikao hicho.
UN /Loey Felipe
Taswira ya chumba cha Baraza la Usalama la UN wakati wajumbe walipokutana 08 Desemba 2023 kwa kikao cha Mashariki ya Kati hususan suala la Palestina kufuatia Katibu Mkuu kutumia Ibara ya 99 ya Chata kuitisha kikao hicho.

GAZA: Ibara ya 99 yatumika; Azimio laandaliwa, Marekani yatumia turufu yake kupinga

Amani na Usalama

Marekani imetumia kura yake turufu kupinga rasimu ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo iwapo lingepitishwa, lingetaka kusitishwa mara moja kwa mapigano kwa sababu za kibinadamu huko Ukanda wa Gaza na kuachiliwa huru kwa mateka wote bila masharti yoyote.

Tweet URL

Hatua hiyo imekuja baada ya wajumbe 15 kupiga kura kufuatia kikao cha dharura kilichoitishwa Ijumaa baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kutumia kifungu namba 99 ya Chata ya Umoja wa Mataifa kuitisha kikao cha dharura cha Baraza hilo kutokana na hali inavyozidi kuwa mbaya kwenye ukanda wa Gaza.

Katika barua yake hiyo ya dharura,  moja ya mbinu yenye uthabiti zaidi kwa Katibu Mkuu kwa mujibu wa Chata ya UN, Guterres anasihi Baraza kusaidia kumaliza zahma kwenye eneo hilo la Gaza lililozingirwa na Israeli, kupitia sitisho la mapigano kwa minajili ya kiutu.

Rasimu ya azimio hilo imeandaliwa na Umoja wa Falme za Kiarabu, UAE, ambapo Marekani imeadia kuwa “kuitisha kuweko kwa sitisho la mapigano si suala la uhalisia na kwamba itakuwa ni kichocheo cha janga kubwa zaidi.”

Azimio limejitoa ufahamu wa hali halisi: Marekani

Marekani imesema kuwa ilishiriki kwa nia njema kabisa kwenye kuandaa nyaraka hiyo, amesema Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa nchi hiyo kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Robert A. Wood, kwa lengo la kuongeza fursa ya mateka kuachiliwa huru na misaada zaidi kuingia Gaza.

“Kwa bahati mbaya, takribani mapendekezo yetu yote yalipuuzwa,” na kusababisha “rasimu isiyo na mizania ambayo imejiondoa ufahamu unaohitajika kusongeshe mbele hali  ya sasa huko Gaza katika hali bora zaidi. Na ndio maana tunasikitika kuwa hatukuweza kuunga mkono,” amesema Balozi Wood.

Amesema Marekani imeshindwa kuelewa kwa nini waandishi wa rasimu hiyo hawakujumuisha lugha inayolaani “shambulio la kigaidi na la kikatili la Hamas” dhidi ya Israel tarehe 7  Oktoba.

Balozi Wood amesema alieleza mapema asubuhi kwa nini sitisho la mapigano lisilo na masharti litaweza kuwa hatari na kupatia Hamas nafasi na uwezo wa kushambulia tena.

Sitisho lolote la mapigano litakaloachia Hamas udhibiti, linawanyima wapalestina fursa ya kujenga kitu bora zaidi kwa ajili yao, ameongeza balozi huyo.

Matokeo ya kura

Katka kupiga kura, wajumbe 13 walipiga kura ya NDIO, Marekani ambayo ina kura turufu ilipiga kura ya HAPANA huku Uingereza haikuonesha upande wowote. Na kwa kuwa Marekani imetumia TURUFU, azimio halikupita.

Mwakilishi wa Kudumu wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Dmitriy Polyanskiy, akizungumza baada ya upigaji wa kura amesema diplomasia ya Marekani inaacha nyuma dunia ikiwa na matatizo.

“Iwapo sitisho la mara moja la mapigano linapingwa tena na Marekani, nchi hiyo inawezaje tena kumtazama machoni mshirika wake? Ametoa wito kwa MArekani kufanya chaguo lililo jema na kuunga mkono takwa la kumalizwa kwa ghasia.

Kauliya UAE kabla ya kupiga kura

Akizungumza kabla ya kupiga kura, Naibu Mwakilishi wa kudumu wa UAE kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Mohamed Issa Abushahaba amesema takribani nchi 97 zimedhamini azimio hilo. “Ni wazi katika nia yake – sitisho mara moja la mapigano.”

“Kuokoa maisha hivi sasa lazima iwe kipaumbele kuliko mambo yoyote yale,” amesema mwakilishi huyo.

Israel: Sitisho la mapigano litaongeza utawala wa Hamas Masharikiya Kati 

Balozi Gilad Erdan, ambaye ni Mwakilishi wa Kudumu wa Israel kwenye Umoja wa Mataifa amesema dunia imekuwa ikishuhudia madhara ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Lakini hakuna hata mara moja Ibara ya 99 imetumiwa ja Katibu Mkuu wa sasa wa UN.

Amesema utulivu Mashariki ya Kati utafanikiwa pale tu ‘Hamasi itakapotokomezwa,’ Kuitisha sitisho la mapigano hakutafanikisha hilo, amesema.

Palestine: Lengo si usalama

Riyad Mansour, Mwakilishi wa Palestina ambayo ina hadi ya mtazamaji tu kwenye Umoja wa Mataifa ameelezea madhara ya mashambulizi ya Isreali, akisema makombora yanalenga kuzuia aina yoyote ile ya misaada kufikia wananchi.

“Na sote tunapaswa kujifanya kuwa uvamizi huu haulengi kuharibu wananchi wa Palestina, Ukanda wa Gaza, wakati imezingira na kupiga mabomu watu wetu na kuwanyima mahitaji ya maisha? Amehoji Balozi Mansour.

“Ninazidi kusoma kwenye vyombo vya habari kuwa Israel haina malengo dhahiri ya vita, na tunapaswa kujifanya kuwa hatujui lengo ni kufuta kabisa wenyeji wa Ukanda wa Gazam? Ameendelea kuhoji.

Balozi Mansour amesema iwapo mtu yeyote anasema anapinga uharibfu na kufurushwa kwa wapalestina, basi hao watakuwa wanaunga mkono sitisho la mapigano.

‘Hakuna tena’ mazingira ya kufikisha misaada kwa ufanisi – Guterres

Mapema asubuhi, kikao kilianza kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhutubia wajumbe akishukuru mabalozi hao kwa kuitikia wito wa kuitisha kikao kufuatia barua yake ikitumia Ibara ya 99 ya Chata, akiwaeleza kuwa ameandika kwa sababu ‘hali hivi sasa ni tete kwenye vita kati ya Israeli na wanamgambo wa kipalestina wa Hamas. 

Baadhi ya wafanyakazi wetu wanakwenda kazini na watoto wao ili wafahamu kuwa wataishi au watakufa pamoja- António Guterres, Katibu Mkuu UN

“Kuna hatari kuwa ya kusambaratika kabisa kwa mfumo wa usaidizi wa kibinadamu Gaza, jambo ambalo litakuwa na madhara makubwa.,” amesema Katibu Mkuu.

Amesema utulivu wa umma unaweza kuvunjika, na kuongeza shinikizo zaidi kwenye ukimbizi kwenye mpaka wa Gaza na Misri.

Hofu ya Guterres

Katibu Mkuu amesema hofu yake ni kwamba mapigano hayo yanawza kuwa tishio kubwa la usalama kwenye ukanda mzima na kwamba tayari Ukingo wa Magharibi ambao unakaliwa na Israeli, Lebanon, Syria, Iran na Yemen wameshajikuta kwenye mzozo huo kwa kiwango tofauti.

Amesema kwa mtazamo wake kuna hatari ya vitisho vya sasa kutishia usalama na amani duniani.

Zaidi ya wafanyakazi 130 wa Umoja wa Mataifa wameuawa: “hii ni idadi kubwa vya wtumishi kwenye tukio moja katika historia ya shirika. Baadhi ya wafanyakazi wetu wanakwenda kazini na watoto wao ili wafahamu kuwa wataishi au watakufa pamoja.”

Hata hivyo licha ya mazingira hayo, Katibu Mkuu amesema UN imedhamiria kusalia na kusambaza misaada kwa watu wa Gaza.

Hali ya kiutu inadhoofika.

Zaidi ya wapalestina 17,000 wameripotiwa kuuawa tangu kuanza kwa mashambulizi ya ya kijeshi ya Israeli, wakiwemo zaidi ya wanawake 4,000 na watoto 7,000.

Makumi ya maelfu wameripotiwa kujeruhiwa, na wengi hawajulikani waliko, wakihisiwa kuwa wamefunikwa na vifusi.

Takribani asilimia 85 ya wakazi wa Gaza wamefurshwa makwao; hospitali, shule na maeneo ya UN yameharibiwa au kusambaratishwa kabisa.

Guterres amesema kando ya hayo, kuna hofu ya baa la njaa, akisema nusu ya wakazi wa Gaza kaskazini na zaidi ya theluthi moja ya waliofurushwa huko Kusini mwa Gaza hawana chakula.

Guerres na kulaani mashambulio ya Hamas

Katibu Mkuu amesisitiza pia “kulaani kwake dhahiri na kwa kina” mashambulio ya kikatili ya Hamas tarehe 7 mwezi Oktoba mwaka huu, akisisitiza kuwa amechukizwa na ripoti za matukio ya ukatili wa kingono wakati wa mashambulio hayo.

“Hakuna uhalilishaji wowote wa mauaji kwa makusudi ya watu 1,200, wakiwemo watoto 33, kujeruhi maelfu wengine, na wengine kutekwa nyara,” amesema Katibu Mkuu akiongeza “na wakati huo huo, ukatili uliofanywa na Hamas katu hauwezi kuhalalishwa na adhabu ya jumla kwa watu wa Palestina.”

Soma hotuba nzima ya Guterres hapa