Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNRWA kuchunguza madai ya wafanyakazi wake kushiriki mashambulio ya Oktoba 7 dhidi ya Israel

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (Maktaba)
UNHCR
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (Maktaba)

UNRWA kuchunguza madai ya wafanyakazi wake kushiriki mashambulio ya Oktoba 7 dhidi ya Israel

Amani na Usalama
  • Katibu Mkuu ataka uchunguzi ufanyike haraka
  • Watakaobainika wafukuzwe kazi na wafunguliwe mashtaka
  • Marekani yasitisha kwa muda msaada wa fedha UNRWA

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amelitaka shirika la Umoja huo linalohusika na usaidizi kwa wakimbizi wa Palestina, UNRWA, lichunguze haraka madai mazito ya kwamba watumishi wa shirika hilo walihusika kwenye mashambulizi ya tarehe 7 mwezi Oktoba mwaka jana wa 2023 dhidi ya Israel.

Bwana Guterres pia amemtaka Mkuu wa UNRWA Phillipe Lazzarini kuwafungulia mashtaka ya jinai au kuwafukuza kazi mara moja wafanyakazi wowote waliobainika kushiriki au kusaidia mashambulizi ya kikatili yaliyofanywa na Hamas na wanamgambo wengine wa kipalestina siku hiyo.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric amesema kupitia taarifa yake ya kwamba “Katibu Mkuu amechukizwa na habari hizi,” huku akieleza kuwa Katibu Mkuu amepata taarifa kutoka kwa Kamishna mkuu wa UNRWA kuhusu madai dhidi ya wafanyakazi wa shirika hilo.

Uchunguzi wa haraka na huru

Taarifa iliyotolewa na Dujarric imesema uchunguzi wa kina na huru dhidi ya UNRWA utafanyika.

Kamishnna Mkuu Lazzarini pia amesema taaifa zimetolewa na mamlaka ya Israeli kuhusu madai ya kushiriki kwa baadhi ya wafanyakazi wa UNRWA kwenye shambulio hilo la Oktoba 7, 2023.

“Ili kulinda uwezo wa shirika kusambaza misaada ya kibinadamu, nimechukua uamuzi wa kusitisha mara moja mikataba ya wafanyakazi hawa na kuanzisha uchunguzi ili kupata ukweli wa suala husika bila kuchelewa,” amesema Bwana Lazzarini.

“Mfanyakazi yeyote wa UNRWA ambaye amehusika na vitendo hivi vya kikatili atawajibishwa, ikiwemo kufunguliwa mashtaka ya kijinai,” ameongeza.

Amesisitiza msimamo wa UNRWA wa kulaani vikali mashambulizi hayo ya kikatili na kutoa wito tena wa kuachiliwa kwa mateka wote haraka bila masharti yoyote.

Usaliti wa ‘maadili ya msingi’

“Madai haya ya kushtusha yanakuja wakati watu milioni mbili Gaza wanategemea msaada ambao shirika ili limekuwa linatoa tangu kuanza kwa hii vita,” amesema Lazzarini.

“Yeyote ambaye anasaili maadili ya msingi ya Umoja wa Mataifa anasaliti pia wale ambao tunawahudumia Gaza, kwenye ukanda mzima na kokote kule duniani.”

Marekani yasitisha upelekaji fedha UNRWA

Kufuatia madai haya, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema inasitisha kwa muda upelekaji wa fedha nyingine UNRWA wakati huu uchunguzi unafanyika dhidi ya wafanyakazi wake wa UNRWA.

Msemaji wa Wizara hiyo, Matthew Miller kupitia taarifa yake amesema “lazima kuweko na uwajibikaji kwa yeyote aliyeshiriki kwenye mashambulizi hayo ya kikatili.”