Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuhuma nzito dhidi ya UNRWA, Katibu Mkuu UN anena, Mkuu wa UNRWA asihi wafadhili

Picha kutoka maktaba, Katibu Mkuu António Guterres akihutubia waandishi wa habari kuhusu Mashariki ya Kati.
UN Photo/Loey Felipe
Picha kutoka maktaba, Katibu Mkuu António Guterres akihutubia waandishi wa habari kuhusu Mashariki ya Kati.

Tuhuma nzito dhidi ya UNRWA, Katibu Mkuu UN anena, Mkuu wa UNRWA asihi wafadhili

Masuala ya UM

Umoja wa Mataifa unachukua hatua za haraka kufuatia tuhuma nzito dhidi ya wafanyakazi kadhaa wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada kwa wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA). Uchunguzi wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uchunguzi wa ndani (OIOS) ulianza mara moja, ameeleza Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kupitia taarifa iliyosambazwa na Msemaji wake usiku wa saa sita Jumapili Januari 28 saa za Marekani.

Kauli hii ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa inakuja huku nchi tisa, zikiwemo Marekani, Uingereza na Ujerumani, zikiwa zimeatanza kusitisha ufadhili kwa UNRWA kufuatia madai kwamba wafanyakazi kadhaa wa Shirika hilo walihusika katika mashambulizi ya kigaidi ya tarehe 7 Oktoba kusini mwa Israel.

Taarifa hiyo imeeleza kwamba kati ya watu 12 waliohusishwa, tisa walitambuliwa mara moja na kuachishwa kazi na Kamishna Mkuu wa UNRWA, Philippe Lazzarini; mmoja amethibitishwa kuwa amefariki dunia, na utambulisho wa hao wengine wawili unachanganuliwa.

Taarifa ya Guterres imesema, “Mfanyakazi yeyote wa Umoja wa Mataifa anayehusika katika vitendo vya ugaidi atawajibishwa, ikiwa ni pamoja na kupitia mashtaka ya jinai. Sekretarieti iko tayari kushirikiana na mamlaka yenye uwezo wa kuwashtaki watu binafsi kwa mujibu wa taratibu za kawaida za Sekretarieti za ushirikiano wa namna hiyo.”

UNRWA pia hapo awali ilitangaza mapitio kamili na huru ya shirika mnamo tarehe 17 Januari.

“Wakati huo huo, raia milioni 2 huko Gaza wanategemea msaada muhimu kutoka kwa UNRWA kwa ajili ya maisha ya kila siku lakini ufadhili wa sasa wa UNRWA hautaruhusu kukidhi mahitaji yote ya kuwasaidia mwezi Februari. Ingawa ninaelewa wasiwasi wao - mimi mwenyewe nilishitushwa na shutuma hizi - naomba sana serikali ambazo zimesitisha michango yao ili, angalau, zihakikishe kuendelea kwa shughuli za UNRWA.” Amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akilenga taarifa kuwa mataifa kadhaa yamejiondoa katika kuifadhili UNRWA.

Matendo ya kuchukiza yanayodaiwa kufanywa na wafanyakazi hawa lazima yawe na matokeo mabaya. Lakini makumi ya maelfu ya wanaume na wanawake wanaofanya kazi UNRWA, wengi katika baadhi ya hali hatari zaidi kwa wafanyakazi wa kibinadamu, hawapaswi kuadhibiwa. Mahitaji makubwa ya watu waliokata tamaa wanaowahudumia lazima yatimizwe.

Mkuu wa UNRWA azisihi nchi kufikiria upya ufadhili

Kamishna Mkuu wa UNRWA Phillippe Lazzarini Jumamosi hii ya Januari 27 amesema kwamba uanuzi wa baadhi ya nchi kusitisha ufadhili yatahatarisha mipango ya shirika ya kuokoa maisha, na kuwataka kufikiria upya.

"Ilitisha" kuona kusimamishwa kwa ufadhili kutokana na madai dhidi ya kikundi kidogo cha wafanyakazi, Lazzarini amesema katika taarifa hiyo ya Jumamosi.

Ameeleza zaidi akisema, "Itakuwa ni kutowajibika sana kuadhibu shirika zima na jamii nzima inayohudumu kwa sababu ya madai ya vitendo vya uhalifu dhidi ya baadhi ya watu, hasa wakati wa vita, kuhama makazi na migogoro ya kisiasa katika eneo hilo."

Kamishna Mkuu wa UNRWA Philippe Lazzarini alipowatembelea wafanyakazi wenzake huko Gaza.
© UNRWA

Bwana Lazzarini amezitaka nchi zilizositisha ufadhili wao kufikiria upya uamuzi wao kabla ya UNRWA kulazimishwa kusitisha mwitikio wake wa kibinadamu.

"Maisha ya watu huko Gaza yanategemea msaada huu na hali kadhalika utulivu wa kikanda." amesema.

Pia amebainisha hatua za mara moja UNRWA ilichukua kwa kusitisha mikataba ya wafanyakazi na kuomba uchunguzi huru wa uwazi.