Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO na IAEA wazindua 'Miale ya Matumaini' kupambana na saratani

Mgonjwa wa saratani akijiandaa kwa tiba ya mionzi
IAEA/Dean Calma
Mgonjwa wa saratani akijiandaa kwa tiba ya mionzi

WHO na IAEA wazindua 'Miale ya Matumaini' kupambana na saratani

Afya

Ikiwa leo ni siku ya saratani duniani, mashirika ya Umoja wa Mataifa ikiwemo la nishati ya atomiki, IAEA, na afya duniani WHO yamezindua programu iitwayo Rays of Hope, au ‘Miale ya Matumaini’ kwa ajili ya kuwezesha nchi wanachama hususan za kipato cha chini na cha kati, kuwapatia wananchi wao huduma za uchunguzi na tiba dhidi ya saratani kwa kutumia miale, huku mradi huo ukianza kwanza na nchi za Afrika.

Taarifa ya pamoja iliyotolewa leo na wakuu wa mashirika hayo imesema hatua hiyo inazingatia ukweli kwamba katika nchi hizo saratani inaua watu wengi ambao wanakosa uwezo wa kupata tiba ya teknolojia ya nyuklia na mionzi.

Mkurugenzi Mkuu wa IAEA Rafael Mariano Grossi amesema uzinduzi umefanyika leo huko Addis Ababa nchini Ethiopia ambao ni mkesha wa mkutano wa viongozi wa nchi wanachama wa Muungano wa Afrika, AU unaoanza kesho mjini humo.

Kati ya nchi 55 wanachama wa AU, 20 kati yao hazina kabisa mashine ya kutibu saratani kwa kutumia mionzi.

“Mamilioni ya watu wanaoishi katika nchi zinazoendelea wanakufa kwa saratani ambayo mara nyingi inatibika na inazuilika. Tuna wajibu wa kimaadili wa kufanya kila tuwezalo kubadilisha mwelekeo huu mchungu,” amesema Bwana Grossi.

Mkuu huyo wa IAEA amesema licha ya kwamba hata katika nchi zingine zinazoendelea kuna shida ya tiba, hali ya ya matibabu barani Afrika bado ni mbaya zaidi.

“Kwa pamoja tena na Rays of Hope ikiongeza shime, IAEA na WHO zimeazimia kuimarisha ushirikiano wao wa muda mrefu kufikia malengo ya pamoja, kuziba pengo la tiba ya saratani duniani na kuchagiza maendeleo kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu ifikapo 2030,” imesema taarifa hiyo ya pamoja ya IAEA na WHO.

Idadi ya vifo duniani

Duniani kote idadi ya vifo inatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 60 katika miongo miwili ijayo, na kufikia milioni 16 kwa mwaka, huku nchi za kipato cha chini na kati, hususan Afrika na kwingineko zikibeba mzigo zaidi wa idadi kubwa ya vifo kuliko nchi Tajiri.

Maeneo ya Rays of Hope 

Mradi wa Rays of Hope unaendeleza uzoefu na utaalamu wa miongo sita wa IAEA katika sayansi ya nyuklia ya kuchunguza na kutibu aina mbalimbali za uvimbe. Mradi pia unalenga kuhamasisha rasilimali fedha na wadau ili kuongeza utashi wa kisiasa katika kukabiliana na saratani ambayo inaweza kutibiwa vyema kabisa na teknolojia ya kisasa ya matibabu.

Halikadhalika mradi huo utachagiza huduma ya tiba dhidi ya saratani kwa kuimarisha upatikanaji wa huduma za mionzi na teknolojia ya nyuklia ambazo ni muhimu katika kubaini na kutibu saratani.
Hatua hii sio tu itaepusha vifo bali pia kuwa na manufaa dhahiri ya kiuchumi na kijamii.

Mradi pia utapatia mafunzo wataalamu ambapo Bwana Grossi amesema “utawezesha kuokoa maisha mengi na kusaidia jamii na uchumi ambavyo vyote vinategemea afya ya watu wake.”

Kwa mujibu wa Bwana Grossi, katika awamu yake ya kwanza, mradi huo utaanza kutekelezwa katika nchi saba ambazo ni Benin, Chad, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Niger, Malawi, Kenya, na Senegal.

Hata hivyo Mkuu wa Idara ya Afrika katika IAEA Shaukat Abdulrazak amesema kipaumbele cha mradi huo katika utekelezaji ni kufuata mahitaji na matakwa ya nchi husika.

Mwaka 2020 pekee watu 700,000 walikufa kutokana na saratani barani Afrika.