Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mauaji ya mangamizi: Hakuna jamii iliyo salama dhidi ya ubaguzi

Sala na muda wa ukimya katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kumbukumbu ya Umoja wa Mataifa ya Kuwakumbuka Wahanga wa Mauaji ya Holocaust.
UN Photo/Manuel Elías
Sala na muda wa ukimya katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kumbukumbu ya Umoja wa Mataifa ya Kuwakumbuka Wahanga wa Mauaji ya Holocaust.

Mauaji ya mangamizi: Hakuna jamii iliyo salama dhidi ya ubaguzi

Haki za binadamu

Kuelekeea siku ya kumbukumbu ya waliofariki katika mauaji ya maangamizi makubwa au Holocaust dhidi ya wayahudi hapo kesho 27 Januari Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekumbusha kuwa mauaji hayo yaliyoanza mwaka 1941- 1945 yalitanguliwa na maelfu ya miaka ya ubaguzi, watu kufukuzwa, kuhamishwa na kuangamizwa na kwamba vitendo kama hivyo sasa vinaenea ulimwenguni. 

“Leo tunashuhudia chuki ikienea kwa kasi ya kutisha, mara ya kwanza ilikuwa mitandaoni lakini sasa inaenea mpaka mwenye vyombo vya habari. Vitendo vya kukataa kutokea kwa mauaji ya Holocaust na upotoshaji navyo vimeongezeka.”

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia katika hafla ya kumbukumbu ya mauaji ya halaiki ya Umoja wa Mataifa, iliyofanyika katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya kuwakumbuka wahanga.
UN Photo/Manuel Elías
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia katika hafla ya kumbukumbu ya mauaji ya halaiki ya Umoja wa Mataifa, iliyofanyika katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya kuwakumbuka wahanga.

Akizungumza katika maadhimisho yaliyofanyika katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani na kuhudhuriwa na watu mbalimbali kwa njia ya ana kwa ana na mtandaoni wakiwemo manusura na wahanga wa mauaji ya Holocaust Katibu Mkuu huyo amesema ili kushinda vitendo hivyo ni lazima watu wote kutetea kusema ukweli.

“Na kutetea ubinadamu wetu wa kawaida kwa kufanya kazi pamoja, lazima tukabiliane na uwongo na chuki mtandaoni. Ni lazima tuendeleze kutoa elimu ya mauaji ya Holocaust kama sehemu muhimu ya ulinzi wetu dhidi ya ujinga, kutojali, na kutovumiliana.”

Akimnukuu Rabi Mkuu wa Uingereza Jonathan Sacks aliyesema “Chuki iliyoanzia kwa wayahudi haiishii kwa Wayahudi” Katibu Mkuu Guterres ameonya kuwa hakuna jamii iliyo salama dhidi ya kushindwa kuvumiliana na hali huwa mbaya zaidi pale kunapokuwa na ushabiki wa kundi moja dhidi ya jingine. 

“Ubinadamu wetu wa pamoja ndio kiini cha Umoja wa Mataifa. Ubaguzi wa rangi na ubaguzi mwingine wowote ni ukiukaji wa kila kitu tunachosimamia. Umoja wa Mataifa umedhamiria kupambana na ubaguzi kwa namna zote. Kwangu mimi, hii ni ahadi ya maisha yote. Kwa Umoja wa Mataifa, ni dhamira ya msingi.” 

Kambi ya maangamizi ya Auschwitz-Birkenau kusini mwa Poland
Unsplash/Jean Carlo Emer
Kambi ya maangamizi ya Auschwitz-Birkenau kusini mwa Poland

Holocaust iwe onyo la milele

Kwa upande wake Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa - UNGA Dennis Francis akiunga mkono suala la kauli za chuki lililoelezwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Matifa amesema kama jamii haitakiwa kuzoea na kuridhika na vitendo vya kuongezeka kwa kauli za chuki. 

“Leo na kila siku lazima tujitolee tena na kufanya zaidi ya kusema “Kamwe isitokee tena”, lazima tuishi maisha yetu kila siku kwa kauli hii.” 

Rais huyo wa UNGA amesema mauaji ya Wayahudi yanapaswa kuwa onyo milele kwa watu wote kuwa macho dhidi ya chuki, ubaguzi wa rangi, ubaguzi mwingine wowote na kutovumiliana, mitazamo na nguvu zinazoleta mgawanyiko na haribifu ambazo hutafuta kimakusudi kudhalilisha utu na mara nyingi kuwatia wanadamu pepo kwa misingi ya uwongo.

“Katika kumbukumbu ya wale waliopoteza maisha, na kwa heshima ya wale waliookoka, ni lazima tujitahidi kuelekea mustakabali wa pamoja ambao ni salama zaidi, usio na woga, na wenye sifa ya kuheshimiana, kuvumiliana, na maelewano.”

Deniss amehitimisha kwa kusema sasa ni wakati muafaka kwa watu wote kujifunza kuishi pamoja, kwa usawa, kwa utu na heshima kwa wote.

Madada Selma Tennenbaum Rossen na Edith Tennenbaum, walionusurika kutoka Poland, wakihutubia Sherehe za Kumbukumbu ya Maangamizi ya Maangamizi ya Umoja wa Mataifa, iliyofanyika katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kumbukumbu ya kuwakumbuka wahanga.
UN Photo/Manuel Elías
Madada Selma Tennenbaum Rossen na Edith Tennenbaum, walionusurika kutoka Poland, wakihutubia Sherehe za Kumbukumbu ya Maangamizi ya Maangamizi ya Umoja wa Mataifa, iliyofanyika katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kumbukumbu ya kuwakumbuka wahanga.

Mauaji kama hayo yanaweza kutokea tena 

Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk katika ujumbe wake kuhusu kumbukumbu ya mauaji ya Holocaust amesema jamii inapaswa kusaka majawabu ya jinsi gani mauaji haya yalitokea ili kudhibiti kutokea tena. 

“Iwapo hatutafanya, yanaweza kutokea tena. Kama sehemu ya kazi hii, na katika kukabiliana vitendo vya kukanushwa kwa mauaji ya halaiki, ni muhimu kuhakikisha kuna taarifa sahihi za kihistoria za Maangamizi Makubwa ya Holocaust, au Shoah, pamoja na mambo yake yote yanayoogopesha.”

Kamishna Türk amesema Ushahidi unaotolewa na wanusurika wa Holocaust ni muhimu na unaumiza sana. 

Amemzungumzia Simone Veil, ambaye baadaye alikua hakimu na Rais wa Bunge la Ulaya, aliingia katika kambi ya Auschwitz-Birkenau akiwa na umri wa miaka 16. Hadi kifo chake, mwaka 2017, alizungumza na wanafunzi na watu wengine kuhusu ukatili, ugaidi, udhalilishaji na utumwa ambao yeye, familia yake na wengine wengi walilazimika kuvumilia. 

Enzi za Uhai wake Veil alisimulia nyakati za huruma na ujasiri - kukutana na wafungwa wengine ambao mara nyingi ulikuwa wa kugusa moyo sana.

“Ninatoa pongezi kwa ujasiri wa ajabu na masomo muhimu ambayo manusura wengi wametuletea. Nashangaa ujasiri wao. Ninawashukuru kutoka ndani ya moyo wangu kwa ubinadamu wao na kutokuwa na ubinafsi kwa ushuhuda wao.”

Suti Mifuko iliyochukuliwa kutoka kwa wafungwa katika kambi ya mateso huko Auschwitz, Poland.
© Unsplash/Frederick Wallace
Suti Mifuko iliyochukuliwa kutoka kwa wafungwa katika kambi ya mateso huko Auschwitz, Poland.

Mauaji ya Holocaust 

Siku ya Kimataifa ya Kumbukumbu ya Maangamizi ya Wayahudi au Holocaust ambayo kila mwaka huadhimishwa tarehe 27 Januari mwaka huu ni maadhimisho ya miaka 79 tangu kukombolewa kwa kambi ya Auschwitz-Birkenau, ambayo ilikuwa ni kambi kubwa zaidi ya mateso na mauaji ya Nazi.

Wayahudi wapatao milioni sita kati yao watoto wakiwa milioni 1.5 waliuawa na mamilioni ya watu wengine wakiwemo Waroma na Wasinti, Waslavs; watu wenye ulemavu, watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja, LGBTIQ+, wanachama wa mitandao ya upinzani; na wapinzani wengine wa Nazi waliuawa.