Skip to main content

Ni jukumu la kila mtu kuzungumza na kuendeleza kumbukumbu ya Holocaust: Katibu Mkuu wa UN

Ua la waridi lililowekwa kwenye njia ya reli katika Makumbusho ya Auschwitz-Birkenau, nchini Poland.
Unsplash/Albert Laurence
Ua la waridi lililowekwa kwenye njia ya reli katika Makumbusho ya Auschwitz-Birkenau, nchini Poland.

Ni jukumu la kila mtu kuzungumza na kuendeleza kumbukumbu ya Holocaust: Katibu Mkuu wa UN

Masuala ya UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres Jumamosi ya leo akishiriki katika sinagogi ya Park East jijini New York Marekani katika maadhimisho ya kusherehekea ukombozi wa kambi ya mateso ya Auschwitz; amesema ni jukumu la kila mmoja kuenzi kumbukumbu za waliofariki katika mauaji ya maangamizi makubwa au Holocaust dhidi ya wayahudi.

Katika hotuba yake, mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa aamesema kuwa, "maangamizi ya Wayahudi hayakutokea kama somo kwa wanadamu, lakini yalitokea, na kwa sababu yalitokea, yanaweza kutokea tena."

Kuongezeka kwa chuki za kidini na aina zingine za chuki

Bwana Guterres ameonya kwamba "mtu hapaswi kamwe kuruhusu kukata tamaa" na lazima awe macho kila wakati. Na alionya zaidi kwamba leo chuki dhidi ya Wayahudi iko kila mahali na inaongezeka kwa nguvu.

Bwana Guterres ameongeza kuwa hali hiyo hiyo inatumika kwa aina nyingine za ubaguzi wa rangi na chuki: chuki dhidi ya Uislamu, chuki dhidi ya wageni, chuki ya watu wa jinsia moja na chuki dhidi ya wanawake na kuwa vuguvugu la itikadi kali ya Nazi mamboleo linawakilisha tishio namba moja la ukosefu wa usalama wa ndani katika nchi nyingi na ndizo zinazokua zaidi.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alisisitiza kuwa "sumu yao inasonga kutoka pembezoni hadi kwenye mkondo wa kawaida," akitoa mfano wa unyanyasaji wa wengine, kudharau tofauti, kudharauliwa kwa maadili ya kidemokrasia na kutoheshimu haki za binadamu.

Chuki kuenezwa kwenye mtandao

Aidha António Guterres amesema kwamba shabiki wa ubaguzi wa rangi wa zamani sasa ana kipaza sauti kinachoweza kufikia ulimwengu na kuwa "mbaguzi hapo zamani alikuwa anaweza kupata mtu mmoja anayemfahamu, lakini hii leo anapata jamii ya mtandaoni ya mamilioni ya watu wenye nia moja."

Kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa matokeo ya mambo yote hayo ni, "ya kutisha kama ambavyo ni hatari". Na akikumbushia kuwa, siku ya Ijumaa, wakati wa sherehe za kila mwaka za kuwakumbuka waathirika wa mauaji ya maanganizi makubwa dhidi ya wayahudi, katika Baraza Kuu, alizindua ombi la kukomesha chuki.

Wajibu wa viongozi wa dini na serikali

Guterres pia amesema viongozi wa kidini kila mahali wana jukumu la kuzuia utumikaji wa chuki na kumaliza misimamo mikali miongoni mwa wafuasi wao. Zaidi ya hayo, serikali zote zina wajibu wa kufundisha kuhusu maovu ya mauaji ya Holocaust.

Ametoa mfano wa Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Kuelimisha umma kuhusu Maangamizi ya Holocaust, ambao uko mstari wa mbele katika kazi hii muhimu. Na alieleza kwamba kwa kuwa wachache na wachache wanaweza kutoa ushahidi wa moja kwa moja, itakuwa muhimu "kutafuta njia mpya za kupeleka mwenge wa ukumbusho mbele, ndani ya familia na vizazi na ndani ya madarasa."